na innocent munyuku
KAMA ningetakiwa kuwataja wanamuziki wa reggae wenye dira njema ya maelekeo nchini basi nisingesita kumweka Ranking Boy kundini.
Hivi karibuni mwanamuziki huyo amefanya mahojiano na Mtanzania na kuweka wazi mikakati yake na vikwazo katika muziki huo nchini.
Ranking Boy ambaye si mzungumzaji lakini mahiri jukwaani ashikapo maikrofoni upole na ‘ububu’ wake hauonekani. Anatema cheche za ajabu akitoa elimu na burudani.
Ana mambo mengi anayoyaandaa mojawapo ni kuipua albamu yake mpya mapema mwezi ujao. Albamu hiyo ameipachika jina la More Than Dread.
“Natarajia albamu yangu ya More Than Dread itakuwa sokoni mapema Desemba na itatoka pamoja na video yake,” anaeleza Ranking Boy.
Mwanamuziki huyo mbali na kuimba reggae anamudu pia raga na midundo dance hall huku akiwa na uwezo wa kutumia ala mbalimbali.
Alianza kujikita katika fani ya muziki mwaka 1998 na baada ya siku chache akahamishia makazi yake nchini Kenya na Uganda akifanya kazi zake za muziki kwa miaka minne nje ya Tanzania.
Ni katika kipindi hicho, Ranking Boy alifanikiwa kufyatua single nne ambazo ni Medicine, Matatizo, Fiesta na Ghetto.
“Nyimbo zangu kwa kweli zinajieleza kwa mfano wimbo wa Matatizo nimesema ukweli juu ya hali halisi ya maisha ya kila siku,” anasema na kisha kuongeza:
“Kila kukicha nchi inaendelea kuwa masikini na watu kwa hakika wanataabika…kwa hiyo nimejaribu kuelezea hali hiyo katika wimbo wangu huo.”
Anasema baada ya kuishi nje ya Tanzania kwa takribani miaka minne aliamua kurejea nchini kuendelea na shughuli zake za muziki wa reggae.
“Mwaka jana nikatua nchini kwa lengo la kuendeleza muziki wa reggae. Nikaja na wimbo wa Fire Ban Dem Head. Nashukuru kwamba single hii ilifanya vizuri na redio nyingi wameendelea kuupiga.
“Kufanya vizuri kwa wimbo huo kukanipa nguvu sana na ndio maana si rahisi kusema kuwa naweza kukata tamaa,” anasema mwanamuziki huyo ambaye tayari ana albamu nyingine ya Dad Fred.
Ranking Boy kwa sasa anaandaa kuzindua mradi maalumu wa muziki wa reggae aliouita Reggae Search utakaodumu kwa mwaka mmoja.
“Lengo la mradi huu ni kuwakusanya wasanii wachanga wa muziki wa reggae na kuwapa dira mpya.
“Muziki wa reggae lazima tukubali pia unahitaji fikra mpya. Hatuwezi kuishi kama walivyoishi wanamuziki wa kale mambo yamebadilika,” anasema na kuongeza:
“Lakini hii haina maana kwamba tunakwepa misingi ya muziki wa reggae hapana. Ninachosema ni kwamba tuwe tayari kwa mabadiliko.”
Anasema anaamini kuwa kuwa na vijana wadogo katika reggae kutawezesha muziki huo kuwa na uhai hasa katika Afrika.
“Mpango wa kuwasaka vijana umeshaanza na hii naweza kusema kuwa ni project ya Afrika Mashariki nzima.
“Kwanza tutawafundisha hao wachanga na baadaye kuwapa muda wa kutunga nyimbo na hapo tutaangalia wimbo gani bora. Lengo hapa ni kuleta ushindani,” anasema.
Anaeleza kuwa anafarijika kuona kuwa wadau wake kutoka Uganda na Kenya wanatoa ushirikiano mzuri na hivyo anaamini kuwa mradi huo wa reggae utazaa matunda mema.
“Ushirikiano unatia moyo kwa kiasi kikubwa, watu wana mwamko sana. Naweza kusema kuwa sasa reggae inakwenda katika neema zaidi kuliko miaka ya nyuma.”
Lakini anasisitiza kuwa kuna haja ya wanamuziki wa reggae kwenda mbele na kuacha imani kwamba lazima kuiga kila jambo la waliopita.
“Kila kizazi kina mambo yake. Ya kale ni kama mwongozo kwamba wenzetu walifanya nini na sisi kazi yetu ni kuboresha.
“Nitatoa mfano kwamba enzi za kina Kalikawe si za sasa na kama mimi sasa nakuja na mtindo wa Bongo Jamaica.
“Bongo Jamaica ni mtindo mpya ambao ni mchanganyiko wa vionjo kutoka Jamaica na ukanda wa Afrika Mashariki. Nami muda wangu ukimalizika watakuja wengine na vionjo vyao,” anasema Ranking Boy.
Hata hivyo, bado anasisitiza kuwa kazi kubwa ya muziki wa reggae ni kuleta mapinduzi ya fikra.
“Huu si muziki wa porojo, muziki wa reggae lazima ulenge mabadiliko katika jamii na si malumbano au hoja ambazo hazina kichwa wala miguu.
“Reggae ilete mijadala yenye ufumbuzi na si kujadili mambo ambayo hayana suluhisho,” anasema Ranking Boy.
Pamoja na hilo, Ranking Boy anasema kuwa katika muziki wa reggae nchini kuna kikwazo ambacho hakina budi kuondolewa.
Anasema tatizo kubwa miongoni mwa wanamuziki hao ni kukosa ushirikiano wa dhati.
“Inashangaza sana na binafsi jambo hili linanikera kwamba hatuna ushirikiano wa kweli. Huo ni uwazi kwamba hatuna umoja.
“Kila mmoja yuko kivyake na hii maana yake ni kwamba mipango mingi itavurugika na tutabaki kulalama.”
Pamoja na yote hayo, msanii huyo ana faraja kuona kuwa muziki wa reggae kwa kiasi kikubwa unakubalika nchini.
“Zamani ilionekana kama kuimba reggae ni kuhamasisha uvutaji bangi lakini sasa mambo yamegeuka hata watu wazima wanapenda reggae,” anaeleza Ranking Boy.
Wednesday, November 7, 2007
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment