na innocent munyuku
IKITOKEA binadamu akatoa maneno ya vichekesho na yasiyo na maana basi huyo ataitwa majinuni. Huyu hupachikwa kofia hiyo kwa sababu hana akili sawa sawa.
Pahala pengine mtu wa aina hiyo hutajwa kuwa ni punguani, mwendawazimu, kichaa ama wakati mwingine huitwa bahau.
Yawezekana mtu wa aina hiyo asifikie hatua ya kuvua nguo hadharani na kusomba kila akionacho lakini ukweli ni kwamba wapo binadamu ambao katika utendaji wao wa kazi hawana tofauti na vichaa wanaozagaa mitaani.
Ukiona dereva anayevunja sheria za usalama barabarani kwa kupenda mwendo kasi katika eneo lililokatazwa basi huyo ni punguani.
Hali kadhalika kwa muuguzi na daktari kutenda yasiyotarajiwa katika fani yao hapo watakuwa wamejihalalishia kuitwa vichaa au wendawazimu.
Mzee wa Busati leo wiki hii ameona ni vema kuwekana sawa katika majukumu ya kila siku kwenye klabu za soka.
Usiposikia moto wawaka Yanga basi ni Simba au kwenye vyama vya soka ndani ya Tanzania. Huko ni vurugu mtindo mmoja.
Huko utakutana na mahuluti kwa maana ya mchanganyiko wa watu wenye mawazo tofauti. Huyu anawaza begi mwingine anafikiria sanduku.
Kwa maana hiyo hata wanapoketi kwenye mikutano na kuleta mjadala, hakuna linalokwenda sawia. Hayaendi sawa kwa sababu kila mmoja la lwake.
Kuna msemo maarufu kwenye klabu hizo za soka. Kwamba uongozi umepinduliwa. Hii ni staili ya miaka mingi nchini. Kundi fulani la kihuni linajikusanya na kutangaza maasi.
Hilo si kwa Simba pekee bali hata Yanga. Kwa maneno mengine jambo hilo lipo kwenye ndimi za wanachama wa klabu hizo kama ilivyo sala ya ‘Baba Yetu’ kwa Wakristo.
Ni heri kwao wanaojiita wanamapinduzi wakaja na fikra pevu za kujenga klabu na soka kwa ujumla. Wangeleta mageuzi chanya na si hasi kama wafanyavyo sasa.
Kwa mtazamo wa Mzee wa Busati kinachofanywa kwenye klabu hizi ni uhuni usiokuwa na mfanowe. Ubabaishaji uliojaa simulizi za lege lege.
Mwenye Busati pengine aulize, kwa mfano hili fukuto la Simba kati ya kina Rubeya na Dalali nani ananufaika nalo? Kelele kibao na ghasia ambazo zingeweza kuzuilika.
Leo twaimba wimbo wa kuijenga Tanzania katika medani ya soka. Miezi michache nyuma sifa ziliwaelemea wachezaji wa timu ya taifa waliokuwa wakisaka tiketi ya kwenda fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika nchini Ghana.
Bendera na fulana zikachapishwa kwa wingi, wenye bahati zao msimu huo ukawa wa mavuno. Wakajaza pochi zao kwa ngwenje kwa kuuza sura za kina Mapunda na Henry Joseph.
Ingawa safari ya Ghana imeota mbaya ukweli wa mambo ni kwamba mshikamano ule wa mashabiki wa soka haukuwa na maana nyingine zaidi ya mapenzi kwa timu yao ya taifa.
Wabongo wamezoea kuzililia Simba na Yanga lakini siku ile Msumbiji ilipomaliza ndoto ya Stars kwenda Ghana, waliungana kwa kilio na majonzi. Huo ni mshikamano wa dhati.
Taswira hapo ni kwamba walio wengi wanapenda soka lakini wanakwamishwa na utawala hasa katika ngazi za klabu. Huko kuna mbigili na magugu sugu.
Anachosema Mzee wa Busati ni kwamba wahuni waliojaa kwenye klabu za soka nchini ndio wanaosababisha kukwama kwa uundaji wa timu ya taifa makini.
Hivi mwatarajia kuwe na timu ya taifa yenye ubora wakati huko chini ni vurugu tupu? Nani kawafunda hayo?
Uhuni na uzandiki unaoendelea katika soka hivi sasa hauna lolote la maana zaidi ya kuua mwelekeo mwema wa soka.
Soga na porojo zinazoendelea katika klabu za soka hazina budi kukomeshwa kwa maslahi ya taifa. Vinginevyo tukubali kuendelea kuwashabikia wenzetu wa ng’ambo.
Endeleeni kuvuruga ili mbaki kuvaa fulana za wachezaji wa ughaibuni huku wa kwenu wakikaa vijiweni kusubiri mia mbili ya kahawa.
Lakini Mzee wa Busati kabla hajafikia ukingoni pengine aweke mambo hadharani kwamba kwenu nyie mnaovuruga mambo ya soka msije kurusha ngumi siku mtakapoitwa majinuni.
Msihamaki wala kushika panga kwani hiyo ni halali kwenu. Kuitwa wehu ni zawadi mwafaka kwenu na wahuni wenzenu wanaowarubuni kuharibu mambo.
Mwandika Busati katoa mwanga. Wapo wengine wenye uwezo wa kuasa ni heri wakafanya hayo ili taifa lisiwe la mabahau.
Wasalaam,
Monday, November 12, 2007
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment