na innocent munyuku
SIKU zinasonga mbele na kinachohesabiwa sasa ni namna ya kuhitimisha mwaka kwa nguvu za Mola.
Hakuna mwenye uhakika wa moja kwa moja kama ataiona Januari Mosi ya mwaka 2008. Badala yake wengi wanaendelea kupiga dua, waendelee ndani ya dimba wasikalishwe benchi.
Mwandika Busati naye yu katika sala akiomba kwa nguvu zote ili auone mwaka mpya kwani kapanga mengi ya neema kwa mwaka ujao.
Tukiachana na dua za mwaka mpya, Mzee wa Busati juma hili anakuja na dukuduku lake ambalo kadri siku zinavyoyoma ndivyo anavyoumia kwenye mtima.
Limekuwa jambo la mazoea sasa kwa mtu fisadi, mshenzi au tapeli kuitwa ‘msanii’. Hilo ndilo jina la ubatizo kwa watu wa jamii hiyo.
Kwamba watu waongo wenye upande hasi katika kaya zetu huitwa ‘wasanii’. Hili jambo kwa hakika linakera nafsi hasa ya Mzee wa Busati.
Linakera kwa sababu hakuna njia nyepesi ya kuliezea hili zaidi ya ukweli kwamba wasanii nchini wanadhalilishwa na kupakwa matope.
Ajuavyo Mzee wa Busati ni kwamba tafsiri rahisi ya msanii ni mtu mwenye ustadi wa kuchora, kuchonga, au kutia nakshi.
Lakini pia pahala pengine, msanii hutajwa kuwa ni mtu mwenye ufundi wa kutunga na kutoa mawazo yake kama vile kwa kutoa shairi, hadithi au tamthiliya.
Leo hii sifa hizo nzuri zimetoweka na wajuzi wameamua kuwapaka matope wasanii kwa kuwahusisha na yasiyofaa.
Tapeli na wasio makini katika jamii huitwa wasanii. Wahuni na wababaishaji leo hii wamepewa jina la usanii. Hii maana yake nini?
Huku ni kudhalilishwa, wasanii wamevuliwa nguo na hakuna anayeonekana kujali. Wamepakwa matope nao kwa unyonge wao ni kama waliokubali hali hiyo.
Hivi kwanini basi waongo na matapeli wasiitwe wahandisi, madaktari, wauguzi, walimu au marubani. Iweje msanii ndiye apakwe tope? Huku ni kudhalilishana.
Mzee wa Busati analia na hili kutokana na ukweli kwamba kuna upotoshaji wa makusudi katika hadhi ya wasanii nchini na pengine duniani kote.
Twawafunda nini vijana wetu wanaochipukia? Tunawalea kwa mtindo gani? Makuzi yao twayapotosha kwani kuna hatari jinsi wanavyokua wakakosa hamu ya kujiingiza katika sanaa.
Hawatakubali kwa sababu tayari wameshanasa vichwani mwao kwamba wasanii ni watu wa hovyo wasio na mwelekeo mwema katika jamii.
Watakimbia kwa vile wamefundishwa kwamba msanii si lolote. Watabaki kufifisha vipaji vyao na hii maana yake ni kwamba jamii itakosa wabunifu na waburudishaji.
Lakini pengine kuna haja ya wasanii kutoa tamko la kulaani hali hii ambayo sasa imezoeleka ndani ya kaya zetu. Amkeni mseme kwamba wasiendelee kugusa mboni za macho yenu.
Msikae kimya manake kimya chenu kitachukuliwa kuwa tayari mmeridhia kuchafuliwa kwa kiwango cha hali ya juu. Itasemwa kwamba ndivyo mlivyo kwani hakuna pahala mmewahi kukemea jambo hilo.
Vinginevyo Mzee wa Busati anaelekea ukingoni akiangalia namna Wanamsimbazi wanavyoendelea kuvutana kwa kile kinachosemwa kwamba kusafisha uongozi.
Simba wa Yuda na Mwenyekiti wake na wengine wanne wamepigwa chini kwa madai ya ‘kutafuna’ fedha za chama na ulegevu wa timu katika Ligi Kuu Tanzania Bara.
Hao wamesomewa tuhuma 10 na hivyo wanachama 271 kuridhia kupigwa chini kwa Simba wa Yuda na bosi wake. Wamesimamishwa lakini je, hiyo ni suluhu ya mambo ndani ya Simba?
Hofu ya Mzee wa Busati ni kwamba isije ikaja kesi ambayo itaendelea kuvuruga klabu hiyo yenye mashabiki tele ndani ya Tanzania.
Msije mkajikuta mmekwamba sehemu kwenye mto wenye mamba wenye njaa kwani huko hakuna salama hata kidogo. Huo utakuwa mwisho wenu wa kila kitu.
Mnachokifanya sasa ni kuanza kutafunana. Mtawatafuna sita baadaye saba hadi 10 mwishowe mtajitafuna na kumalizana na huo utakuwa mwisho wenu.
Kwamba moto huu uliowashwa Msimbazi usije unguza kila kitu na kuyaacha mahame.
Wasalaam,
Monday, November 5, 2007
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment