na innocent munyuku
KATIKA jamii nyingi za Kiafrika tohara ni mpango maalumu unaowalenga vijana wa kiume.
Mpango huo huwakusanya wahusika na kuwekwa jando ambako ni sehemu ya kufanyiwa tohara na kisha kupewa mafundisho kwa ajili ya maisha yao ya siku zijazo.
Hapa watafundwa juu ya ujasiri, uzalishaji mali na malezi kwa familia zao. Yaweza semwa kwamba jando ni pahala penye kutoa elimu kwa vijana.
Lakini kabla ya kuwekwa jando, huja maandalizi kwa ajili ya shughuli hiyo. Jando haliji kwa pupa kama kifanyavyo kimbunga. Mambo hupangwa yakanyooka.
Kutokana na umakini wa maandalizi hayo, ndio maana Waswahili wakaja na msemo kwamba tohara ya Ijumaa huanza Alhamisi. Kwamba kila jambo lafaa liwe na maandalizi badala ya papara.
Mzee wa Busati juma hili ameona anene juu ya hulka ya wadau wa soka nchini ambao kila uchao wamekuwa na ndoto ya kufika Kombe la Dunia lakini wanakwama kutokana na sababu mbalimbali.
Si mara moja au mbili washika kalamu na wenye uwezo wa kujenga hoja wameshasema juu ya vikwazo vilivyoko katika soka nchini.
Wameshahubiri juu ya nidhamu, programu endelevu, miradi na kubwa ni umuhimu wa kutambua kuwa soka nchini haiwezi kukua kama hakuna vitalu vya soka.
Mbaya zaidi ni kwamba wenye mamlaka katika uendeshaji wa mpira wa miguu nchini hawana jipya kwenye bongo zao.
Wamebaki kupiga porojo na kusahau kuwa pasipo vitalu vya soka mambo yatakwenda upogo.
Hao wamekaa kwenye viti wakisubiri kufika paradiso bila kuonja mauti. Wanahubiri na kuamini hadithi za Alfu Lela U Lela.
Wanaishi maisha ya kufikirika zaidi kuliko uhalisi wa mambo. Matokeo yake ni kwamba soka badala ya kupanda chati inageuka kuwa konokono kwenye sakafu iliyojaa chumvi. Vipaji vya soka vinapukutika.
Wamebakia kuamini ulozi kwenye viwanja vya soka na suala la maandalizi kwa miaka 50 ijayo hawanalo kwenye mipango yao. Wanawaza ya leo na si kesho.
Huko kwenye kusaka uchawi wameenea na idadi yao inaridhisha. Wamejaa tele kiasi kwamba hawaoni tena mwanga. Wamebaki gizani na wako radhi kuomba fedha kwa wafadhili eti kwa ajili ya kamati za ufundi.
Kamati ambazo wachezaji na viongozi waandamizi watalishwa madudu kama si kulala makaburi siku chache kabla ya mechi muhimu. Huo ndio mpira wetu!
Mzee wa Busati hasemi kwa ubaya bali kauli yake imetokana na kukerwa na haya magugu na mbigili kwenye soka.
Walau hivi karibuni wadau walipewa vidonge vya kule Bwagamoyo kwenye kile kilichoitwa semina elekezi ya wiki moja kwa klabu 14 za Ligi Kuu Bara.
Wakati wa kufunga semina hiyo, huku Mkurugenzi wa Maendeleo ya Soka wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), Ashford Mamelodi akizitaka klabu kuachana na ndumba.
Alichosema Mamelodi siku hiyo ni kwamba makocha na viongozi wa soka nchini wanao wajibu wa kujifunza masuala ya ufundi na uongozi.
Mamelodi ambaye ni Mkurugenzi wa Maendeleo wa FIFA Kanda ya Afrika, aliwataka washiriki wa semina kuyafanyia kazi yote waliyojifunza kwa maslahi ya timu zao na soka kwa ujumla, huku wakiweka kando masuala ya imani za kishirikina au ndumba katika mpira wa miguu.
Akasema semina hiyo haitakuwa ya maana kama waliyojifunza hawatayafanyia kazi.
“…matarajio ni kubadilika kuanzia sasa, kuanzia masuala ya utawala hadi ufundi huku mambo ya kishirikina yakiwekwa kando,” alisema Mamelodi.
Hakuishia hapo, kiongozi huyo akaweka wazi kwamba klabu kongwe kama Simba na Yanga zafaa ziwe mfano wa kuigwa.
Kwamba timu hizo sharti zionyeshe dira ya mabadiliko na kuachana kabisa na mambo ya kishirikina dimbani. Huo ndio mtazamo wake ambao bila kigugumizi unaungwa mkono na Mwandika Busati.
Hii maana yake ni kwamba kama klabu za Ligi Kuu zitakuwa na mwelekeo sahihi hakuna shaka timu nyingine zitaiga ufundi huo.
Mpira wa miguu haupelekwi kwa ndumba bali ufundi na kupanga dira ya maendeleo. Huo ndio ukweli kuhusu soka.
Tanzania imejaa vijana wenye vipaji vya hali ya juu katika soka. Hata hivyo, vipaji hivyo vitaibuka kama viongozi wa soka watafuata utawala bora.
Vipaji hivyo vitavuma na kutamba kimataifa kama kutakuwa na mpango mzuri katika maandalizi ya mashindano na mgawanyo wa kazi na pia kuachana na migogoro.
Kuendelea na mtazamo wa kizamani ni ni kuifukia soka kaburini. Yafaa basi samaki akunjwe angali mbichi.
Mzee wa Busati anaamini kwamba kama maandalizi yatakuwa makini hakuna shaka kwamba Tanzania itatoa wachezaji wengi wazuri watakaotamba kimataifa.
Hilo linawezekana kama tutakubali na kutambua kuwa tohara ya Ijumaa huanza Alhamisi. Acheni papara kuweni na mipango ya maandalizi.
Wasalaam,
Sunday, November 25, 2007
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment