Monday, October 8, 2007

Mapatano pwani, baharini ni uvuvi

na innocent munyuku

JUMA la kula na kusaza limeanza. Wenye matumbo na nguvu ya kushika tonge wajiandae. Wajiweke kwa ajili ya kutafuna vinono wakati wa Sikukuu ya Idd el Fitr.

Mzee wa Busati naye anaomba uhai afike mwisho wa juma aungane na wengine katika ulaji la unywaji. Kwa masela siku kama hiyo hawana haja ya kuumiza vichwa manake kila nyumba huwa huru kukaribisha wageni.

Badala ya kula chips dume na maji ya kwenye mifuko ya plastiki siku hiyo ni kutafuna vipapatio vya kuku, pilau na vinywaji vyenye ubora. Mambo ya shangwe hayo.

Wiki hii Mzee wa Busati anaingia ulingoni akiwa na maswali kibao yenye mshangao pia kuhusu kauli ya kiungo wa zamani wa Yanga, Sekilojo Chambua.

Chambua kalalama kwenye vyombo vya habari kwamba uongozi wa Yanga haujatekeleza ahadi zake kwake baada ya kustaafu kuichezea timu hiyo kwa takribani miaka 10.

Nyota huyo alipoamua kupumzika kuichezea Yanga akaahidiwa mema kama vile kulipiwa pango la nyumba kwa mwaka mzima, kununuliwa kiwanja na kusomeshwa ukocha nje ya nchi.

Miaka minne sasa imepita tangu ahadi hizo zitolewe na kwa mujibu wa Chambua hakuna lililotekelezwa. Waliotia saini barua ya ahadi kwa mwanasoka huyo wameingia mitini na kukaa kimya.

Ni habari ya kusikitisha kuona kwamba mchezaji aliyeitumikia timu kwa moyo wake wote akilipwa mshahara na posho hafifu anapewa ahadi hewa kama hizo.

Mzee wa Busati hakika angeishangaa Yanga kama wangetimiza ahadi hizo. Angeshangaa kwa sababu kwa uzoefu wa klabu za Kibongo suala la masilahi kwa wachezaji limekuwa sugu.

Vinara wa klabu daima wamekuwa wenye kupenda sifa kuliko utekelezaji wa masuala muhimu kwa wanaojenga klabu.

Chambua bila shaka ana haki ya kudai kilichoahidiwa kwake na klabu. Waliohusika kumfanyia uhuni mwanasoka huyo waanikwe na ikibidi wachapwe bakora ili uwe mfano kwa wengine.

Husemwa kwamba mapatano kwa kawaida hufanyika pwani ukishaingia habarini ni uvuvi tu hakuna mjadala mwingine labda kama kutatoka dhoruba.

Kwa maana hiyo Yanga inapaswa kutekeleza kilichoandikwa kwenye barua ya ahadi kwa Chambua na si kumletea longolongo.

Kwani kulikuwa na ulazima gani wa kumpa moyo Chambua kama mlijua kuwa mlichoahidi hakitekelezeki? Au mwalitaka kumwiga tembo?

Chambua mbali na kupewa ahadi hewa anadai pia malimbukizo ya mishahara yake na hadi leo hakuna kiongozi wa Yanga anayesimama kutetea haki ya mwanasoka huyo. Wamelala na bila shaka hata majalada hayapo.

Mwandika Busati hasiti kusema kuwa kuna uhuni umefanyika. Dhuluma imedhihirika na watu wanapaswa kuwajibika katika hili.

Anachosema Mzee wa Busati ni kwamba anayolalamikia Chambua yawezekana yametokea kwa wachezaji wengi wa Yanga na klabu nyingine.

Haya ni mambo ambayo yameendelea kwa muda mrefu. Wahusika wamekaa kimya na hivyo kuhalalisha ubaya wa hali hiyo kwa kiwango cha kutisha. Matokeo yake wachezaji hugeuka kuwa ombaomba.

Nani atasimama na kuweka mambo sawia? Hata katika hili twamsubiri Masiha? Kwanini hekima isitumike kuondoa dhuluma hii?

Waungwana daima hutimiza ahadi zao hata kama walifanya makosa katika tamko la awali. Hutekeleza walichosema na kama waliteleza hujipanga upya.

Kwamba Chambua apewe alichoahidiwa na wala hakuna haja ya kwenda njia ndefu apewe chake atulie.

Mzee wa Busati anaelekea ukomo wa Jumanne hii akitoa salamu kwa wadau wake. Kwa waliojaliwa kufunga Ramadhan endeleeni kupata neema.

Kila jema liwakute katika maandalizi ya kumaliza mfungo lakini msije mkaleta balaa kwa kuzidisha kipimo cha furaha siku ikifika.

Wasalaam,

No comments: