na innocent munyuku
HII imekuwa staili ya maisha ya kila siku. Hakuna maendeleo zaidi ya kushikiana bakora kwenye klabu za soka.
Kila unapokanyaga ni mbigili mtindo mmoja. Hadithi ni zile zile, mikwaruzano ndani ya klabu za soka bongo. Yanga na Simba ndizo zinazoongoza.
Mwandika Busati kwa muda mrefu amekuwa shuhuda wa hizo vurugu. Hakuna linalokwenda sawia badala yake ni watu kuumana kwa maslahi yao binafsi.
Yanga msimu huu moto umewaka. Mafahari wanapimana ubavu na wapambe wao pembeni wakisubiri matokeo. Wanachogombea ni ulaji na kujaza matumbo yao.
Kila kukicha hakuna maendeleo zaidi ya kuwasha moto wa mgogoro. Wanaoendesha masuala hayo wanajua wanachotaka na hakika wanakipata.
Mzee wa Busati hushangazwa na mambo haya. Kwamba inawezekanaje waseme wana mapenzi na klabu wakati wanaziangamiza?
Nani atakuwa mwokozi wa haya malumbano? Nani atafanikisha mema ndani ya klabu hizo? Hivi kweli kuna ulazima wa malumbano haya au ni laana ya kipekee?
Mwandika Busati sasa hana shaka tena kuamini kwamba Yanga na Simba ni makaburi ya wachezaji. Hakuna vitalu huko badala yake kumejaa misumari ya moto.
Waliojaa huko kwa kofia za uongozi hawana lolote kwani tambo zao zinatokana na kulishwa mabaya kutoka kwa wapambe wao wanaokaa vijiweni na kupanga mizozo.
Na kwa akili zao huwaza kwamba Tanzania inao ubavu wa kwenda Kombe la Dunia. Nani ataifikisha Tanzania huko wakati wachezaji wamelelewa kwenye migogoro?
Dira yao ni kupanga mbinu za kupambana na migogoro na si kuleta ufundi dimbani. Hilo si kosa lao kwani ndivyo mfumo ulivyo. Wala hakuna haja ya kuwalaumu hao ndiyo makuzi yao.
Kwa mfano timu hizo mbili hazina utaratibu mzuri wa kuleta makocha. Leo kaja huyu kesho kaletwa mwingine. Bila shaka kuna tatizo zaidi ya uendawazimu.
Hakuna umakini katika timu hizo na ndio maana kuna mengi yanafanyika kihuni na kiholela. Kila mwenye ulimi basi anayo fursa ya kutoa tamko hata kama tamko hilo ni pumba.
Midomo ya wapambe huwawezesha kupata ngwenje za kuvimbisha matumbo yao. Vitambi vinakuzwa kwa majungu na uzandiki. Husemwa kila linalowezekana ili wapate shibe. Hakuna lolote la kujenga soka.
Wenye akili zao hubaki wakicheka kwani wakati mwingine si busara kujibizana na wendawazimu. Waache wawehuke na matokeo yataonekana hivi pumbe.
Kama soka imewashinda jaribuni mashindano ya urembo au masumbwi. Kama mpira wa miguu umewashinda jaribuni riadha au kurusha tufe na kama ubavu mnao kajiungeni na wacheza gofu na tenisi.
Mzee wa Busati anatoa ushauri huo kutokana na ukweli kwamba kama kweli hao wanaojiita wadau wa soka wana nia ya kuinua mchezo huo mbona uozo ni ule ule?
Kila kukicha ni mizozo na mitafaruku. Kila uamkapo ni kelele za kugombea madaraka kwenye klabu hizo. Hii maana yake nini?
Tusidanganyane kwamba hao waliopo wana upeo wa kuweka mambo sawa. Kama upeo wanao basi wanaharibiwa na wapambe jambo ambalo ni hatari katika maendeleo ya soka nchini.
Hivi hakuna wa kuamka na kusema sasa yatosha? Kwa staili hii tusahau kuuza wachezaji wetu ng’ambo ya nchi na kama watauzwa basi wataishia Uarabuni ambako baada ya miezi michache huishia kuuza maduka ya Waarabu.
Kuna haja gani basi kujiita wadau wa Yanga na Simba wakati mwaleta mabaya klabuni? Dira za maendeleo hazimo. Kilichopo ni uhuni na uzushi wa migogoro.
Hakuna shaka kwamba huu ni mwanzo wa mwisho wa Simba na Yanga. Hakika huu ni ukomo ili ziibuke timu nyingine ambazo bila shaka zinaweza kuleta mageuzi.
Huu ni utabiri wa Mzee wa Busati na kama utatimia itakuwa neema kwa wapenda soka. Kwamba badala ya kugeukia Arsenal na Manchester United au Liverpool wataketi kuzishangalia timu za nyumbani.
Mwandika Busati anafikia ukomo kwa juma hili ambalo limeanza kwa wengi kubaki na madeni ya sikukuu. Idd el fitr imewatafuna na sasa mji umebaki kama pilipili.
Wasalaam,
Monday, October 15, 2007
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment