WATANZANIA kwa muda wamesahau kujadili maumivu ya Bajeti ya Mwaka Mpya wa Fedha wa 2007/8. Wamepunguza kuizumgumzia Taifa Stars na safari yake ya Ghana. Kinachonenwa sasa ni kifo cha Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Amina Chifupa aliyefariki dunia Jumanne wiki hii jijini Dar es Salaam. Katika makala haya waandishi wetu ELIZABETH MJATTA na INNOCENT MUNYUKU wanazungumzia mengi na matarajio aliyokuwa nayo Amina katika uhai wake.
Mwanasiasa huyo machachari aliyekuwa jasiri mdogo kuliko wote bungeni ambaye alipata nafasi hiyo kupitia tiketi ya Umoja wa Vijana wa CCM.
Siku chache kabla ya kuhudhuria Mkutano wa Tano wa Bunge mwaka jana, Amina alifanya mahojiano na gazeti dada la RAI.
Alifika chumba cha habari kwa ajili ya mahojiano maalumu yaliyochukua takribani saa 2. Akiwa amevalia suti yake nyeusi, hereni ndefu za dhahabu kwenye masikio yake, mkufu wa dhahabu ulioshika vema shingo yake, bangili mikononi mwake vilitosha kumpendezesha nyota huyo aliyezimika ghafla.
Kama ilivyokuwa hulka yake, Amina alisema mengi ya msingi kwa kujiamini na hata alipoulizwa juu ya nini kilichompa ujasiri wa kuapa kwa mbingu bungeni kwamba atawafichua wauza dawa za kulevya hakuonekana kujuta.
“Sikuogopa hata kidogo…ninaamini kuwa mimi ni kiongozi hivyo siwezi kuogopa kusema ukweli,” alisema Amina.
Lakini hakuishia hapo akaongeza: “Kama mtu ni mwoga hafai kuingia bungeni, hatuwezi kuwaacha vijana wa Tanzania wakiangamia kwa matumizi ya dawa za kulevya.”
Alitumia fursa hiyo kuzungumzia namna alivyojisikia vibaya baada ya baadhi ya magazeti na watu mbalimbali kuhoji uwezo wake mara alipotangaza kujiingiza katika siasa.
“Siku ya kuapishwa bungeni ilikuwa kazi ngumu kwangu. Pamoja na kuwa mzungumzaji mzuri nilikuwa mwoga nikaona kitu cha ajabu. Nadhani hilo lilitokana na ukweli kwamba baadhi ya magazeti yalishanibeza.
“Baada ya kula kiapo nikaanza kupata ‘vinoti’ vya kunipongeza, mmoja wao alikuwa Kapteni John Komba aliyesema ‘mwanangu umenitoa aibu’.”
Alipoanza kutoa hoja zake bungeni, Amina alionyesha dira njema kwa kuigusa jamii moja kwa moja. Alizungumzia umuhimu wa kuwasaidia wanawake wajawazito na udhibiti wa malaria nchini.
Akawa gumzo kwa walio wengi na hata yale maneno ya kejeli kwamba hakuwa na dira njema zikaanza kuyeyuka. Akavaa koti la umakini na huku akijenga matumaini kwa vijana nchini.
Amina hakuishia katika siasa pekee aliingia kila mahala kwa lengo la kujenga jamii bora. Alihimiza ustawi wa watoto yatima, uendelezwaji wa michezo na sanaa kwa ujumla.
Alikuwa bega kwa bega kuisadia timu ya soka ya taifa (Taifa Stars) lakini pia alikuwa mbioni kuanzisha ligi ya taifa kwa vijana.
Jumatano wiki hii wakati wa kuuga mwili wa marehemu, Ruge Mutahaba ambaye ni mmoja wa wakurugenzi wa Clouds FM ambayo Amina alipata kufanya kazi ya utangazaji, alitaja sifa kubwa ya Amina kuwa ni king’ang’anizi.
“Siwezi kupata lugha rahisi kuelezea ujasiri wake…nitatoa mfano wakati nilipomweleza kuwa anatakiwa kufanya kazi kwa siku sita na kupumzika siku moja akagoma.
“Akatoa wazo kwamba anahitaji kuanzisha kipindi cha taarabu,” anasema Mutahaba na kuongeza kuwa hakuwa na namna ya kumzuia.
“Tukampa nafasi na kweli alifanya vizuri sana katika kipindi hicho cha taarabu na kikubwa zaidi ni kwamba alikuwa mbunifu.”
Naye mtangazaji maarufu nchini, Taji Liundi anayejulikana pia kama ‘Master T’ anamwelezea Amina kuwa mmoja wa wasichana waliokuwa na moyo wa kuthubutu.
“Alikuwa mwenye ujasiri na kuamini kuwa anao uwezo wa kufanya mambo mapya yenye faida kwa jamii.
“Alipenda kuelekezwa kwa kila jambo alilolifanya hata kama alijua kuwa anaweza akalifanya mwenyewe.
“Lakini nasikitika kwamba Amina amefariki dunia bila amani moyoni. Ameondoka wakati mgumu akiwa na msongamano wa mawazo. Hili linaniumiza sana,” anasema Taji.
Wakati fulani alipotembelea kituo kimoja cha watoto yatima jijini Dar es Salaam, Amina aliwahi kumwaga machozi baada ya kuona mazingira waishio watoto hao.
Mapenzi yake kwa watoto yalijionyesha pia wakati akiendesha kipindi cha watoto katika redio.
Katika kipindi chake hicho, alikuwa akipingana sana na baadhi ya wazazi waliokuwa wakifanya matendo mabaya kwa watoto wao. Alikemea unyanyasaji wa watoto.
Lilipokuja suala la mada ya kujadili daima aliibuka mshindi kutokana na uwezo wake wa kujenga hoja na kukubalika. Huo ukawa msingi wa umaarufu wake.
Maelfu ya watu waliofika kuuga mwili wake walionyesha kuwa tayari kuna pengo kubwa katika jamii. Kwamba matarajio na misingi mizuri aliyokuwa ameanza kuijenga Amina bila shaka sasa inakwenda upogo.
Wapo wanaoendelea kushangaa kipaji cha binti huyo kwani katika umri wake mdogo aliweza kufanya mambo makubwa katika jamii tofauti na umri wake.
Amina sasa hatunaye ameshazikwa kijijini kwao Luhanjo-Lupembe Wilaya ya Njombe na kilichobaki sasa ni kuenzi mema yake.
Licha ya kuwa na msimamo katika kupambana na dawa za kulevya, alikuwa mtetezi wa wanawake, vijana, watoto na wanafunzi.
Katika michango yake bungeni. Kwa muda mfupi aliokaa bungeni tangu ale kiapo mjini Dodoma, Desemba 28, 2005, Amina amejipambanua na kuwa miongoni mwa wachangiaji mahiri bungeni, licha ya uchanga wake kisiasa.
Lakini pia alikuwa na mvuto katika jamii na ndiyo maana haikushangaza pale habari zake zilipokuwa zikipewa umuhimu mkubwa katika vyombo vya habari nchini.
Pamoja na hilo, Mei 6 mwaka huu, Amina alianza kuwa kwenye wakati mgumu baada ya kuripotiwa kuwa ametalikiwa na mumewe Mohamed Mpakanjia.
Mpakanjia alikaririwa na vyombo vya habari akisema kuwa ametengana na mkewe huyo aliyedumu naye katika ndoa kwa miaka mitano na kubahatika kupata mtoto mmoja wa kiume.
Kwa bahati mbaya sana mara baada ya taarifa hiyo ya talaka, zikaja taarifa kwamba Amina amelimwa talaka kutokana na kujihusisha kimapenzi na Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe wa Chadema.
Siku tatu baada ya habari za talaka kuripotiwa, baba yake Amina alizungumza na waandishi wa habari kwenye Ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) Dar es Salaam akisema kuwa suala hilo ni la kisiasa na kwamba CCM inao utaratibu wake wa kutatua mambo yake.
“Masuala yote yanapitia katika mkondo wake. Wazazi hatutaki kuharibu pensheni yetu, si mnajua kuwa siku hizi watoto ndio pensheni?” alisema Mzee Chifupa.
Lakini wanahabari wengi walishangazwa na hatua ya Mzee Chifupa kuitisha kuzungumza katika mkutano huo kwani jana yake Amina aliahidi kuzungumza yeye.
Waandishi walikuwa na shauku ya kukutana na Amina ana kwa ana kwani wiki moja kabla ya kuthibitishwa kwa taarifa za kutalikiwa, anadaiwa alisambaza ujumbe wa maandishi katika simu za mkononi.
Inadaiwa kuwa ujumbe huo ulikwenda kwa baadhi ya watu wanaoaminika kuwa karibu na Naibu Waziri mmoja aliyemtuhumu kusababisha kuvunjika kwa ndoa yake.
Ujumbe ulisomeka hivi: “Alichounganisha Mwenyezi Mungu binadamu hawezi kukitenganisha. Nakuheshimu sana kama kiongozi wangu, Mwenyekiti wangu, Naibu Waziri, M-NEC, M-CCM, mkubwa wangu kiumri, mbunge na kadhalika.
“Nimesikitishwa sana na jitihada za kutaka kuvuruga ndoa yangu, nakutakia kila la heri, lakini usisahau malipo ni hapa hapa duniani na kila mwenye kufanyia wenzake mabaya na yeye hulipwa kwa ubaya.
“Nampenda sana mume wangu na ntailinda ndoa yangu kwa gharama yoyote cko tayari kumpoteza, mi ni zaidi ya mwanamke. Asante sana, kila la heri na kazi njema katika kulifanikisha hilo, wizara
yako nyeti sana, ina mambo mengi sana. Bye.”
Kuna wakati ikasemwa kwamba kuachika kwake kulikuja baada ya Naibu Waziri mmoja kudaiwa kwenda kumchomea utambi kwa mumewe. Baada ya tukio hilo, Amina alitoa ahadi ya kumtaja mbaya wake jambo ambalo halikutimia.
Yapo madai kuwa Naibu Waziri huyo alikuwa na mipango ya kumpaka matope katika siasa kutokana na nia aliyoitangaza ya kutaka kugombea uenyekiti wa taifa wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM).
Amina pia alikuwa ameomba ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC), kupitia Kundi la Vijana katika Uchaguzi Mkuu wa CCM unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Juni 22, mwaka huu, Amina aliuliza bungeni kwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, akitaka kufahamishwa hatua gani zinazochukuliwa na Serikali katika kudhibiti uvujaji wa mitihani. Liliulizwa kwa niaba yake na Mbunge wa Muleba Kaskazini, Ruth Msafiri (CCM).
Amina aliyezaliwa Mei 20 mwaka 1981 alikuwa mcheshi na katika moja ya mikakati yake alipata kutamka kuwa ipo siku atajitumbukiza katika kinyang’anyiro katika jimbo.
Hakuishia katika kulitamani jimbo. Alipata kusema pia kuwa anaamini anao ubavu wa kuwa rais wa nchi katika miaka ijayo. Kauli hiyo aliitoa wakati alipohojiwa katika kipindi cha Jahazi cha Radio Clouds FM Mei mwaka huu.
Alisema wanasiasa wengi dunia huwa na ndoto ya kupanda ngazi hadi kufikia urais.
Aliongeza kuwa maisha ya kila mwanadamu huenda kwa malengo. Kwa hakika yaweza kusemwa kuwa maisha ya Amina yalikwenda kwa utaratibu wa kufikiria mambo chanya daima.
Pamoja na hayo, atakumbukwa kwa tukio lililomsibu bungeni mwaka jana wakati alipoagizwa na Spika kutoka nje ya ukumbi wa Bunge kutokana na kuvaa suti ya kike na kofia ya pama bila glovu kwa mujibu wa kanuni.
Friday, October 12, 2007
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment