na innocent munyuku
KATIKA maisha ya binadamu wapo majasiri na kundi jingine la watu wenye hofu huku wengine wakibaki kuwa ÔvuguvuguÕ hawajulikani wako upande upi.
Ujasiri ninaomaanisha hapa ni ule wa kusema jambo bila kigugumizi kama alivyofanya mwimbaji Easter Bugado maarufu kama Zurry Chuchu.
Wiki iliyopita nilisoma gazetini habari ya mwanadada huyo kwamba amejitangaza kuwa mwenye virusi vya ugonjwa wa ukimwi.
Kauli yake hiyo ilinivuta na sikuona kama nitakuwa natenda haki kwa kuiacha habari hiyo itokee sikio la pili bila ya kumpa salamu za pongezi msanii huyo.
Naam anastahili pongezi kwa kuwa amekuwa wazi kusema ana virusi vya ukimwi tofauti na wasanii wengine na hata watu wengine katika nyanja mbalimbali.
Uwazi wa Zurry ni wa kuigwa kwani kwa kujiweka wazi kiasi hicho, atakuwa anaokoa maisha ya watu wengi katika jamii inayomzunguka.
Kauli ya msanii huyo inanifanya nimkumbuke Mkurugenzi wa TOT Plus, Kapteni John Komba ambaye Mei 28 mwaka 2002 alisema kuwa baadhi ya wasanii wake wamefariki kwa ugonjwa wa ukimwi.
Kapteni Komba alitoa kauli hiyo mjini Bagamoyo katika risala yake baada ya kundi hilo kuhitimu mafunzo ya sanaa katika Chuo cha Sanaa cha Bagamoyo.
ÒKatika kipindi cha miaka 10 ya uhai wa TOT zaidi ya wasanii 15 wamefariki kwa ukimwi,Ó alisema Kapteni Komba wakati huo.
Nilimwona kuwa shujaa anayestahili kuigwa kwa kuthubutu kwake kuvunja ukimya.
Komba aliitoa kauli hiyo mbele ya mgeni rasmi William Lukuvi wakati huo akiwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu.
Lukuvi ambaye alikuwa akimwakilisha aliyekuwa Waziri Mkuu Frederick Sumaye aliposimama na kutoa hotuba yake alisisitiza kuwa lazima wasanii wawe mstari wa mbele kuupiga vita ukimwi.
Ninapoyatafakari hayo narejea kumwona Zurry kuwa msanii anayepaswa kuigwa kwani kufanya hivyo kutasaidia kupunguza maambukizi.
Tuwe wazi kusema kama tumeathirika ili kuwasaidia wengine ambao hawajaathirika. Tusione aibu kujitangaza na huu uwe utaratibu wa kudumu.
Kukaa kimya na kuufanya ukimwi kuwa ugonjwa wa siri ni kuendeleza maambukizi ambayo yangeweza kuepukika.
Tuseme ili wengine wajihadhari na kuacha tamaa ya kufanya mapenzi. Ni nani leo hii atasimama na kuomba tendo la ngono kwa mtu ambaye ameshajitangaza kuishi na virusi vya ukimwi?
Licha ya kwamba kila mmoja anayo nafasi ya kuushambulia ukimwi, si vibaya tukaanza kujiweka wazi kama alivyofanya Zurry.
Hata hivyo, bado ipo haja ya kuyakumbuka maneno ya Lukuvi kwamba wasanii wawe mstari wa mbele kutunga nyimbo za kuielimisha jamii kuhusu ugonjwa huo.
Tuache habari ya kusifia wanawake wazuri au kusifia pombe kama wafanyavyo baadhi ya wasanii wa muziki wa kizazi kipya maarufu kama bongofleva.
Tujiweke kando na malumbano na majungu katika vikundi vya sanaa na badala yake muda huo tuutumie kuwapa somo raia wengine juu ya kuepukana na janga la ukimwi.
Ya nini kuimba juu ya mavazi mazuri au mambo mengine yasiyofaa wakati ndugu zetu wanaangamia?
Kuna raha gani kukata mauno jukwaani na vivazi vya aibu wakati kuna maelfu wanakufa kwa sababu pengine walikosa elimu juu ya ugonjwa huo?
Wasanii simameni sasa na kuwakemea wasiotaka mabadiliko. Hakuna kulala kwani vita hii ni pana.
Tumieni vipaji vyenu kuliokoa taifa linalozidi kuandamwa na watu wasiokuwa tayari kuacha tabia chafu zinazozidi kuufanya ukimwi ukithiri.
Alichofanya Zurry ni cha kuungwa mkono na ni heri kumwona kama shujaa aliye tayari kuwaokoa watu wake.
Kamwe asitengwe Zurry, asilani! Asibaguliwe kwa kunena ukweli. Pia asiandamwe kwa ÔvijembeÕ na badala yake tufuate moyo wake wa kishujaa wa kujitangaza kwa uwazi.
munyuku@gmail.com
0754 471 920
Thursday, January 18, 2007
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment