Friday, January 19, 2007

Tunahofu juu ya ukimwi lakini kemikali nazo ni tishio

na innocent munyuku
WARSHA nyingi zimefanyika juu ya ugonjwa wa ukimwi. Mada mbalimbali zimetolewa kuhusu ugonjwa huo unaoangamiza mamilioni ya watu sehemu mbalimbali duniani. Lakini wakati tunawaza kuhusu ukimwi, walio wengi hawajaona hatari ya chemikali zenye sumu zilizozagaa katika nchi zinazoendelea.
Kemikali hizo kwa kiasi kikubwa zimeendelea kuwaangamiza maelfu katika nchi mbalimbali barani Afrika ambako kwa miaka mingi zimekuwa zikitumika katika kilimo, mifugo na mambo mengine.
Mamilioni ya tani ya kemikali hizo zilizozagaa barani Afrika zimekuwa zikidhuru maisha ya watu kutokana na uelewa mdogo wa watu wake ambao wengi wao hawajapewa elimu ya kutosha kuhusu ubaya wa dawa hizo hasa pale zinapotumika isivyo.
Hivi karibuni ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa ufadhili wa GTZ, WWF na AGENDA iliandaa warsha kwa waandishi wa habari wa ndani na nje ya nchi juu ya usalama wa kemikali na mpango wa uondoshaji wa dawa barani Afrika (ASP). Warsha hiyo ilifanyika kwenye Hoteli ya Paradise mjini Bagamoyo.
Katika mada yake Mkemia Mkuu wa Serikali, Dk. Ernest Mashimba alisema kemikali ni muhimu katika maisha ya watu lakini pia ni hatari kwani sumu hizo mara nyingi zimesababisha maafa au uharibifu wa mazingira na wakati mwingine kuharibu ngozi.
ÒDawa hizi ziko sehemu mbalimbali na ni muhimu katika maisha ya kila siku lakini zina madhara makubwa kama hazitatumika ipasavyo.
ÒChangamoto kubwa tuliyonayo ni kuwa na elimu juu ya kemikali kwa sababu ni muhimu kuwa na ufahamu na uelewa wa kutosha kuhusu dawa hizi.Ó
Kwamba kwa vile wengi hawana elimu ndio maana utunzaji wake umekuwa wa hovyo huku watu wengine wakiyatumia kinyume cha makusudio.
Inakadiriwa kuwa kwa mwaka zaidi ya tani milioni 500 huzalishwa katika viwanda katika nchi zilizoendelea na kusambazwa katika nchi zinazoendelea ikiwamo Tanzania na kwa bahati mbaya matumizi ya dawa hizo ni madogo.
Kwa maana hiyo kemikali hizo zimekuwa zikiharibu mazingira na kubadilisha hali ya hewa na wakati huo huo kuharibu maji, vyakula vinavyotumika kwa binadamu na wanyama pia.
Yapo magonjwa yatokanayo na matumizi mabaya ya kemikali hizo kama vile saratani ya ngozi, upofu, kuharibu akili, kansa ya damu, kutoka mimba au kujifungua kabla ya muda.
Inasemekana kuwa kemikali zimekuwapo katika uso wa dunia kwa zaidi ya miaka 200 iliyopita na katika tani milioni 500 zinazozalishwa kila mwaka, aina kati ya 70,000 na 100,000 ziko sokoni huku aina mpya kati ya 1,500 na 2,000 zikiendelea kuota mizizi sokoni kila mwaka.
Kemikali hizo kwa hali ilivyo sasa wazalishaji wakubwa barani Ulaya na Marekani ndio wanaoendelea kunufaika kutokana na mauzo. Kwa mfano Marekani hupata kiasi cha dola trilioni 1.6 kwa mwaka.
Pamoja na ukweli kwamba kemikali zimekuwa zikisaidia kudhibiti magonjwa mbalimbali na kukuza mimea mashambani, bado Afrika inaangamia kutokana na madhara makubwa ya kemikali hizo. Waathirika wakubwa katika jamii ni watoto, wajawazito na wazee.
Huu ni mzigo kwa bara la Afrika kwani sasa hivi taratibu zinafanywa kupata pesa za kutosha kwa ajili ya kuzikusanya kemikali hizo na kuzirejesha barani Ulaya ili ziharibiwe.
Tanzania imeshapata dola za Marekani milioni 6.7 kutoka kwa wahisani mbalimbali lengo likiwa kuhakikisha sumu hizo zinakusanywa kwa uangalifu mkubwa na kuzisafirisha kwenda Ulaya. Ikumbukwe kuwa sumu hizo ni zile ambazo zimebaki katika ardhi ya Afrika bila matumizi kwa muda mrefu.
Mfano Septemba 11 mwaka huu nchini Ivory Coast watu 10 walipoteza maisha na zaidi ya 100,000 wakihitaji uangalizi wa madaktari kutokana na athari za kemikali zilizomwagwa.
Upo uwezekano pia kuwa janga kama hilo linaweza kutokea katika eneo jingine ndani ya Afrika kutokana na ukweli kwamba bado watu wake hawajapata elimu ya kutosha juu ya kemikali kama hizo.
Katika Tanzania utatifi uliofanywa kati ya mwaka 1998-2000 umebaini kuwepo kwa maghala 325 ya kemikali sehemu mbalimbali nchini. Si ajabu yakabainika maghala mengine yenye kemikali zisizofaa.
Tatizo kama hili halipo Tanzania pekee, nchini Mali, Morocco, Ethiopia na Afrika Kusini ziko katika shida hii. Uzito wa tatizo hili umelifanya bara la Afrika kuwa katika mkakati wa makusudi kuhakikisha kuwa linafikia ukomo.
Hatuwezi kuendelea kuhatarisha maisha ya Waafrika kwa kuziachia kemikali hizi zisizofaa ziwepo katika maisha yetu ya kila siku.
Kama alivyowahi kusema mtoa mada mwingine katika warsha hiyo, Wolfgang Schimpf kutoka GTZ kwamba kukosekana kwa elimu ya utunzaji wa kemikali kutasababisha madhara makubwa na kwamba ipo haja ya kudhibiti hali hiyo.
Lakini akaonya kuwa si jambo sahihi kumwaga au kutupa kemikali hizo baharini kwani huko ni kuharibu maisha ya viumbe hai vinavyotegemea maji hayo.
Dawa kama DDT, Aldrin, Chlordane, Dieldrin, Endrin, Heptachlor, Hexachlobenzene (HCB) zimekuwa zikitishia uhai wa Afrika na kwa maana hiyo, ulazima wa kuwapa Waafrika elimu unabaki kuwa changamoto kwa wakazi wake.
Tangu miaka ya 1960 kumekuwa na kesi mbalimbali juu ya madhara ya matumizi ya kemikali katika uso wa dunia. Kwa mfano kati ya mwaka 1960-1963 katika mji wa Minamata nchini Japan, watu 1,714 waliathirika na Methyl Mercury kati ya hao 267 walifariki dunia.
Mwaka 1974 kulipuka mtambo wa kemikali kulisababisha kusambaa kwa cyclohexane katika eneo la Flixborough, England. Katika tukio hilo watu 28 walipoteza maisha. Kulipuka kwa mtambo wa nuklia Chernobly, nchini Ukraine mwaka 1986 kuliangamiza maisha ya watu 1,000.

No comments: