Thursday, January 18, 2007

Zemkala: Vichwa sita vyenye upeo wa juu

Na Innocent Munyuku

UZOEFU unaonyesha kuwa watu wengi waliotimiza ndoto zao katika maisha hawakuwa na shaka na wanachowazia. Walijipanga na kuhakikisha kuwa mipangilio yao ya maisha inakuwa kama walivyokusudia. Lije jua au mvua.

Hivyo ndivyo ilivyo kwa wasanii wa ngoma na nyimbo za asili ya Tanzania wanaojulikana kama Zemkala. Ni kundi linaloundwa na wasanii sita ambao bado umri wao haujavuka miaka 30. Wangali na damu mbichi katika kueneza mila na utamaduni wa Mtanzania katika nchi mbalimbali duniani.

Wanaounda kundi hilo ni Yuster Nyakachara, Havintishi Baraza, Fadhili Mkenda, Yusuf Chambuso, Maulid Mastir na Kasembe Ungani.

Kwa mujibu wa kiongozi wa kundi hilo, Yusta Nyakachara, walianza kupata uhai mwaka 2002, waanzilishi wakiwa Ungani na Mkenda ambao walijieungua kutoka katika kundi lililowahi kuvuma wakati la Sisi Tambala. Wasanii wengine walijumuika na Zemkala wakitokea Splendid Theatre.

Katika miaka minne ya uhai wa kundi hilo, Zemkala imefanya mambo mengi ndani na nje ya nchi kwa kulitangaza taifa katika maonyesho ya sanaa kila lilipopata nafasi ya kufanya hivyo.

Cha kufurahisha kuhusu wasanii hawa ni kwamba si rahisi kujua kama wamepeana majukumu tofauti jukwaani. Hawana mzaha wawapo katika pilikapilika za kuleta burudani huku kila mmoja akijaribu ‘kuivaa’ kazi ya msanii mwingine.

Chambuso ni hodari katika kupiga ngoma nane, lakini usishangae kumwona akiziacha ngoma hizo na kujiunga na wachezaji ambao ni Yusta na Havintishi ambao ni mahiri katika kulishambilia jukwaa.

Si Chambuso tu mwenye hulka hiyo, Mastir ambaye ni kiboko ya njia katika kupiga marimba, hasiti kuacha marimba hayo na kuwavaa mashabiki akiwaonyesha uwezo wake mwingine wa kucheza na kuruka sarakasi na baadaye atamweka pembeni Chambuso naye kuanza kupiga ngoma tena kwa ustadi mkubwa kabisa. Wakati huo filimbi yake inakwenda pamoja na mirindimo ya drums kutoka kwa Mkenda.

Lakini uhondo huo unakuwa haujakamilika pasipo kumhusisha Ungani. Huyu ni kinara katika kupiga ngoma ndogo maarufu kama jembe. Mara chache utamwona akicheza lakini uso wake wa tabasamu na umakini utakufanya mara kwa mara kuangalia namna anavyokwenda vyema na wapigaji wa vyombo vingine.

Tangu kuundwa kwa kundi hilo, wameshazuru Sweden, Msumbiji, Kenya na Zanzibar katika kufanya maonyesho mbalimbali kupitia matamasha ya sanaa. Huko kote wameacha sifa njema na kujizolea mashabiki lukuki.

Unapowauliza katika maonyesho hayo ni lipi ambalo wanalikumbuka zaidi hawasiti kulitaja onyesho la mjini Kisumu kiasi cha miaka miwili iliyopita. Kwa nini wanalikumbuka? Swali kama hilo linawafanya wote waangue kicheko kinachofuatiwa na maelezo kutoka kwa Yusta.

“Kule katika siku ya kwanza ya maonyesho yetu tulipata wakati mgumu sana. Unabadilisha nguo hapo ili uvae za kuingilia jukwaani unasikia mtu pembeni yako akisema ‘cheki hiyo bonge ya raba lazima tutoke nayo.

“Sasa katika mazingira hayo unapanda jukwaani pasipo umakini, kwani unawaza kuibiwa viatu au vifaa vingine,” anasema Yusta.

Lakini baada ya kulalamika kwa waandaaji wa shughuli hiyo mambo yakabadilika siku iliyofuata. “Hata hivyo, bado ikawa adhabu kwetu…ni sawa tulipewa ulinzi wa kutosha lakini shughuli ilikuwa pevu,” anakumbuka Mastir.

Kwamba kwa vile onyesho lao lililotangulia walivipiku vikundi vingine kutoka nchi nyingine, walijikuta wakiwa na mashabiki wengi ambao kila walipopanda jukwaani walilazimisha waendelee kutoa burudani pasipo kupumzika.

“Kwa hakika ilikuwa hali ngumu na kama tusingekuwa na mazeozi ya kutosha hali ingekuwa mbaya sana, unacheza jukwaani kwa dakika 60 lengo likiwa kumaliza kiu ya watazamaji wako,” anasema Yusta.

Mbali na ushujaa wao jukwaani, Zemkala wamepikwa katika msimamo wa kulinda na kujivunia utamaduni wa Mtanzania na Mwafrika kwa ujumla. Maneno yao yamejawa na hamasa kama ya Dk. J Aggrey ambaye anasifika sehemu nyingi duniani kwa kujivunia ngozi yake nyeusi.

Dk. Aggrey alipata kukaririwa akisema kuwa kama angelikwenda mbinguni na Mungu angelimwuliza kama anataka kurejea duniani kama mtu mweupe angeligoma. Na kwamba kama angeulizwa kwa nini hataki kurudi kama mtu mweupe, angesema bado ana kibarua cha kufanya kama mtu mweusi na anajivunia rangi hiyo na kwamba kama kuna asiyejivunia rangi yake basi huyo hastahili kuwa na pumzi ya uzima.

Unaweza kuwataja Zemkala kuwa ni wasanii wasio na aibu kutangaza ngoma za asili ya Tanzania. Wamefanikiwa kuchanganya ngoma za makabila tofauti katika maonyesho yao kote walikopata nafasi ya kufanya hivyo.

Lengo ni kwamba ifike siku Tanzania ijulikane kupitia ngoma zake kama walivyofanikiwa Wakongo au mataifa ya Afrika Magharibi.

Wanashangaa kuona hadi hii leo baadhi ya Watanzania hasa vijana wanakataa kucheza ngoma za asili na badala yake kukimbilia disko na kuiga utamaduni wa Kimagharibi.

“Huu ni msimamo wetu kwamba lazima tuitangaze Tanzania kwa kutumia ngoma na nyimbo zetu,” anasema Yusta. “Lazima nia iwepo na wengine naamini watafuata nyayo zetu katika kujivunia mambo yetu ya asili.”

Katika jitihada zao hizo za kuing’arisha Tanzania kimataifa, wameshaanza kupenya kibiashara katika bara la Ulaya na Marekani Kaskazini.

Meneja wa Zemkala, Jotham ‘Gota’ Warioba, amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa kundi hilo linasonga mbele kwa hali na mali.

Amelidokeza gazeti hili kuwa ameshaanza mazungumzo na kampuni moja ya inayojishughulisha na usambazaji wa muziki nchini Ujerumani ili kuingia nayo mkataba wa kibiashara.

Kampuni hiyo ina matawi sehemu mbalimbali barani Ulaya na kusambaa hadi Marekani Kaskazini. Hata hivyo, hakuwa tayari kuitaja kwa vile kuna mambo ya msingi wanayotakiwa kuwekana sawa kabla ya kuutangazia umma.

“Wameonyesha nia ya dhati kujumuika nasi na sisiti kusema kuwa hii ni njia mojawapo kuelekea katika mafanikio ya Zemkala,” alisema Gota.

Pamoja na hayo, Gota aliongeza kuwa anaweka mkakati wa kulifanya kundi lake hilo liwe na maonyesho ya ndani ya nchi badala ya kuwaburudisha watu wa nje pekee.

“Tanzania hakuna utamaduni wa kupenda kuangalia ngoma za asili, wamezoea dansi au disko lakini sisi tunadhani upo umuhimu wa kuwa na show (onyesho) walau mara moja kila wiki hapa kwetu ili watu waone uzuri wake…wasikimbilie kwingine.”

Zemkala hujikita katika mazoezi kila Jumatatu, Jumatano na Ijumaa kuanzia asubuhi hadi mchana katika Ukumbi wa Utamaduni wa Russia uliopo Sea View jijini Dar es Salaam.

munyuku@gmail.com
+255 471 920

No comments: