Thursday, January 18, 2007

Tuchangie harusi hadi lini?

na innocent munyuku

KIASI cha miaka miwili nyuma, rafiki yangu wa karibu alipata kuniambia namna alivyojijengea ukuta mgumu dhidi ya ndugu, jamaa na marafiki baada ya kuweka wazi msimamo wake juu ya kutochangia harusi.

Katika simulizi zake, jamaa huyo akanieleza kuwa ilifika mahala akashindwa kuchangia pesa kwa ajili ya harusi kwa vile aliangalia hesabu ya bajeti yake kwa mwezi, akakuta anatumia kiasi kikubwa cha pesa katika kuchangia harusi badala ya mambo mengine ambayo anaamini ni ya msingi zaidi.

Akatoa mfano kwamba kama kila mwezi watu sita wanaoa au kuolewa na kila mmoja atamchangia Sh 20,000 ina maana kila mwezi atenge Sh 120,000. Hivyo basi kwa mwaka mzima itamgharimu Sh 1,440,000. Hiyo ilikuwa miaka miwili iliyopita na kuna uwezekano mkubwa gharama kwa ajili ya shughuli hizo zimepanda.

Nimelazimika kuandika makala hii kutokana na kuguswa na hali halisi ya maisha ya Mtanzania wa kawaida na ukweli kwamba, kila siku michango ya harusi imeendelea kushamiri miongoni mwetu.

Kwamba kwa vile gharama ya maisha imepanda kwa kiwango kikubwa ni heri tukaangalia maeneo muhimu ya kuchangia ili kuleta tija kwa kila Mtanzania. Nasema hivyo kwa sababu dhamira yangu inanituma kuamini kuwa, michango mikubwa katika harusi haina neema kwa wahusika. Kama kuna wanaonufaika katika michango hiyo ni wachache na kwa muda mfupi.

Imebainika kuwa, michango mingi hasa ya pesa huishia kwa waliochangia na si kwa maharusi. Kwamba fedha zinazokusanywa hatimaye huishia kwenye matumbo ya waliochanga kwa kunywa na kula siku ya harusi na baadaye kile kinachoitwa kuvunja kamati.

Binafsi ningeunga mkono kuendelea kwa michango hiyo kama pesa zingewanufaisha moja kwa moja maharusi. Kwa mfano zimepatikana shilingi milioni nne basi wapewe maharusi kwa ajili ya kuendelea na maisha yao.

Ya nini basi tuchangishane mamilioni ya pesa halafu tuzitumbue pesa hizo kwa kunywa bia na kula pilau? Kuna maana gani basi kuwaona maharusi baada ya siku chache wanalia njaa kwa sababu pesa zimeshatumika kukamilisha sherehe ya wao kuungana katika ndoa? Ni heri tubadilike sasa kwani huko tuendako siko.

Nitatetea hoja yangu hii kwa msingi mkuu mmoja nao ni kuwa, naamini wanaojiandaa kufunga ndoa kwa mujibu wa sheria wamefikisha umri wa kufanya hivyo na wanapojiandaa katika muungano huo wa hiari wawili hao wameshaweka maandalizi ya maisha yao mapya.

Kwa maana hiyo, katika mazingira kama hayo ni jambo lililo wazi kuwa wanaooana lazima watakuwa kwenye nafasi ya kukabiliana na majukumu ya ndoa ikiwa ni pamoja na maisha ya kila siku. Wanachotakiwa ni kujiandaa kama afanyanyo mwanafunzi darasani kukabiliana na mitihani yake.

Si mara moja au mbili, kumekuwa na matukio ya kuchefua roho baada ya kumalizika kwa harusi. Utasikia bwana na bibi harusi wanakabiliwa na madeni yaliyotakana na ‘kuzidi kwa bajeti’ ya harusi yao. Wanabaki kukuna vichwa wasijue watalizipaje pesa hizo. Huu si uungwana!

Kwa hakika si uungwana na ndio maana napiga zumari hili lenye sauti ya kupinga kuchangishana pesa kwa ajili ya harusi na baadaye kuzitumia pesa hizo kwa ajili ya kushibisha matumbo na kuwaacha wanandoa ambao ni wahusika wakuu wa shughuli hiyo wakienda nyumbani mikono mitupu.

Kama kweli tuna mapenzi ya dhati na maharusi kwa nini basi pesa zinazochanganywa wasipewe ili wajue nini cha kufanya mara baada ya kutoka kwa kasisi au sheikh? Huu ni muda wa kubadilika, matarumbeta na kukodi kumbi za kifahari tuwaachie wengine ambao wana uwezo wa kutenda pasipo kutembeza bakuli.

Badala yake tuchangie katika masuala mengine ambayo naamini kuwa ni muhimu kuliko hili la kuchangishana ili watu wapate kushiba kwenye harusi. Tulipe mgongo suala la harusi na tuangalie maeneo mengine kama elimu au afya.

Kuna mifano hai kwamba, wapo watu walioshindwa kuendelea na masomo kwa sababu tu hawana pesa za kuwawezesha kusonga mbele. Hao wamejaa kwenye ardhi ya Tanzania. Wamefumbiwa macho kwa sababu dhamira za walio wengi ni kutoa pesa ambayo baada ya mwezi mmoja ataitumia kwa kunywa bia na kutafuna vipapatio vya kuku.

Jaribu leo kuitisha kikao kwamba unataka kujiendeleza shule na unahitaji kuchangiwa pesa kwa ajili ya kukidhi gharama za masomo. Hata marafiki zako wa karibu wanaweza kukupiga chenga. Naam watapiga chenga kwa sababu huo utamaduni ni mpya katika mioyo yao. Wamezoea kuchanga ili siku chache baadaye wazirejeshe pesa hizo kwa faida yao. Hawaangalii matokeo mema yanayolengwa kuja kwa miaka walau minne ijayo.

Naamini kabisa kuwa pesa zinazotumika katika kufanikisha harusi zingewasaidia wahitaji wengine kama wagonjwa waliolazwa hospitalini. Inawezekana wakajitokeza wengine wakadai kuwa hilo ni jukumu la Serikali. Huko ni kupotoka, kwani kama tuna ubavu wa kufanya harusi za kifahari kwa kuchangishana pesa kwanini tushindwe kuwasaidia watu wengine katika masuala muhimu?

Leo hii nikiamua kwenda kanisani kufunga ndoa na kisha kuingia kwenye banda langu la uani na mke wangu bado nitakuwa na amani kwamba jambo la msingi limeshafanyika nalo ni uhalali wa ndoa hiyo mbele ya kasisi na baraka kutoka kwa mashuhuda wanaotambulika kwa mujibu wa sheria. Sitakuwa na kinyongo bali furaha tele moyoni.

Watanzania tumekuwa wepesi wa kuiga mengi kutoka Ulaya na Marekani kwanini basi utaratibu wa ndoa za ‘kimya kimya’ nao tusiige kutoka kwao? Kwamba huko ughaibuni mtu anajikuna anapofikia na kufanikisha harusi yake na wala hana haja ya kulia shida kwa wengine. La maana ni cheti cha ndoa kwa mujibu wa sheria zilizopo.

No comments: