Friday, January 19, 2007

Kifimbo: Tusibeze tiba za asili

na innocent munyuku

HISTORIA inaonyesha kuwa binadamu kabla ya kuibuka kwa teknolojia za kisasa alitumia vitu vingi vya asili. Kuanzia chakula na dawa kwa magonjwa mbalimbali.

Kuibuka kwa mbinu mpya katika nyanja za kila aina kukasababisha utengenezwaji wa dawa viwandani na hivyo kurahishisha ufungaji na usambazaji pia.

Pamoja na uvumbuzi wa viwanda vya dawa, ukweli wa mambo ni kwamba tiba za asili zingali na umuhimu mkubwa kwa binadamu na mataifa mengi yanaendelea kuzitumia dawa hizo.

Tanzania ni moja ya nchi ambazo zimeendelea kutumia tiba za asili kwa magonjwa mbalimbali ikiwemo zile za kupunguza makali ya ugonjwa wa ukimwi, homa na ngiri.

Hata hivyo, kumekuwa na wimbi la watoa tiba za asili ambao wengi wao si waaminifu. Hili ni kundi ambalo limejiwekea mizizi ya kuwatapeli watu badala ya kutoa tiba halisi kwa wagonjwa.

Katika mahojiano na gazeti hili mapema wiki hii, mganga maarufu wa tiba za asili nchini Dk. Haruna Kifimbo anasema ujio wa kundi la ‘makanjanja’ katika tiba za asili ni kero kubwa kwa jamii.

“Mimi ninachoomba ni mamlaka za Serikali hapa nchini kuwadhibiti hawa wahalifu wa tiba za asili. Wanaharibu maana ya huduma hii.

“Si kila mtu anaweza kuwa mganga wa tiba za asili hilo lazima tukubaliane na kwa vile hawa wanaoharibu sekta hii tunaishi nao mitaani ni suala la kuwakamata na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria ili kuokoa maisha ya Watanzania,” anasema Dk. Kifimbo.

Dk. Kifimbo anaeleza kuwa kama waharibifu wa aina hiyo hawatadhibitiwa, Tanzania itajikuta iko kwenye janga litakalolidhoofisha taifa.

Akizungumzia uwezo wa tiba hizo katika jamii, Kifimbo anasema dawa hizo zimekuwa zikiokoa maisha watu kila siku. Anayataja maradhi ambayo wamekuwa wakikabiliana nayo kuwa ni pamoja na upungufu wa nguvu za nguvu za kiume.

“Ukweli ni kwamba katika miaka ya hivi karibuni, wanaume wengi wamekuwa wakipungukiwa nguvu za kiume na tiba zipo. Matatizo kama haya mara nyingi hutokana na vyakula tunavyokula hasa vilivyopoteza uasili wake, mtu mwenye kisukari, ngiri, presha au ugonjwa wa figo anaweza kukumbwa na tatizo hili,” anasema.

Dk. Kifimbo anasema wakati umefika kwa jamii kutambua umuhimu wa matumizi ya dawa za asili kwani uzoefu unaonyesha kuwa ni nzuri kwa matumizi ya binadamu na hukomesha kabisa magonjwa sugu.

Anatolea mfano magonjwa kama kuwashwa sehemu za siri, chunusi sugu na mabaka, maumivu ya mara kwa mara ya mgongo au kiuno, kukojoa kitandani, kukosa usingizi homa ya matumbo au magonjwa nyemelezi.

“Angalia Wachina wanavyoendelea kutumia dawa za asili, wanajua ubora wake ndio maana wamezing’ang’ania. Sasa sisi tunazibeza nadhani hii ni hatari kwetu kama hatutakuwa makini.

“Amerika ya Kusini nao wako mstari wa mbele katika kudumisha matumizi ya dawa hizi. Kwa hiyo ni jukumu letu kama wataalamu wa tiba kuhakikisha kuwa tunakuwa wabunifu kila siku na kuwadhibiti wanaoharibu sekta hii, hiki ni kilio changu.”

Mbali na kutoa huduma ya tiba, Dk. Kifimbo amekuwa akijitolea kuisaidia jamii katika mambo mbalimbali. “Naamini katika jamii bora na ndio maana ninachokipata nagawana na wengine,” anasema Kifimbo.

No comments: