Friday, January 19, 2007

Si lazima wote waimbe

Si lazima wote waimbe
YAPO mambo ambayo kila yanapotokea katika hii dunia, basi huwa gumzo kwa mitazamo tofauti. Aghalabu mambo hayo yanaweza kuwa mema au mabaya.Watendaji wa mambo hayo wakati mwingine hulenga kupata umaarufu katika jamii. Na ndio maana katika baadhi ya nyimbo za muziki hapa kwetu zimekuwa zikitaja majina ya watu kuanzia mwanzo hadi mwisho.Kuna tetesi kwamba hao wanaotajwa hulipia kiasi fulani cha ngwenje ili wapate kurushwa hewani kupitia maikrofoni. Utasikia wakipayuka ‘Papaa Mkechee wapi Papaa Lusajo’ au ‘Papaa Kidume wapi Mukulu Ndago’.Inawezekana ni staili ya miaka mingi katika sanaa ya muziki lakini je, hao wanaotajwa wana kitu gani kipya kwa jamii? Ana mchango upi ambao msikilizaji wa tungo husika atakunwa kusikiliza?Kwa mtazamo wa Mzee wa Busati huu ni sawa na ulofa. Muziki gani huu wa kutajana majina kuanzia ubeti wa kwanza hadi wa mwisho? Maana yake nini hasa?Pengine kwa mtazamo wa Mwandika Busati staili hii ni bardani. Hakuna uzito wowote ndani yake na ni sawa na debe tupu ambalo halikosi kupiga kelele.Kama noma na iwe noma! Huu ni ubabaishaji katika sanaa. Imbeni kitu kinachoeleweka si kutajana majina tu. Imbeni mema kwa nchi kama vile vita dhidi ya maradhi mbalimbali na umaskini.Enendeni mkaseme maovu ya serikali mbalimbali za Afrika na hata huko Ulaya na kwingineko. Kemeeni wabakaji na walawiti kwani hayo yote ni kinyume na taratibu katika kaya nyingi.Wakemeeni na kuwaasa wafanyakazi wavivu wanaotumia vibaya nafasi zao kwa kujilimbikizia mali huku wengine wakila mlo mmoja kwa siku.Mwadhani kwa staili hii ya kutajana majina mtaweza kuuza tungo zenu kwa pesa nyingi ndani na nje ya nchi? Mtaishia kukaa kwenye viti virefu na kukamata chupa za bia. Mkienda mbali sana mtanunua mikweche ya magari kutoka Mashariki ya Mbali.Hakuna shaka kwamba ukosefu wa ubunifu ndicho chanzo cha muziki wa Tanzania kukosa kutamba nchi za mbali.Lakini pia muda huo mnaotumia kutaja majina ya watu wasio na jipya katika jamii, ingefaa basi mketi kupanga mikakati ya kuboresha muziki wetu na namna ya kuwabana wasambazaji wa kazi zenu ambao wakati mwingine wamekuwa kero kwa baadhi ya wanamuziki wanaofanya vizuri sokoni.Mzee wa Busati ataendelea kuyaweka haya bila hofu kwani tangu siku ya kwanza alipoanza kuyoyoma katika safu yake hii ambayo walau sasa itagota miaka sita aliahidi kuwa mkweli pasipo ukandamizaji.Ndio maana kero kama hizi zinapigiwa zumari ziende kuzimu. Walio wengi wanakerwa na mtindo wenu wa wanamuziki kutaja taja majina katika tungo.Mwenye Busati anayasema haya kwani ana hofu kwamba ipo siku baadhi ya hawa wanamuziki wataanza kuimba habari za wake zao na nyumba ndogo.Wataanza kutaja majina ya watu wao wa ukoo kwa sababu ndimi zao zimekuwa na shauku ya kutaja watu katika nyimbo. Wakishamaliza kutaja hayo watatueleza pia na umri wa familia zao.Mzee wa Busati angepita kuona siku moja akitua New York aulizwe habari za wanamuziki wa hapa kwetu ambao tayari kwa wakati huo watakuwa wameteka soko la muziki huko.Hiyo ndiyo ndoto endelevu ya Mzee wa Busati kwamba ije siku akiwa Congo Brazzaville aulizwe juu ya akina Dudu Baya au Banza Stone na Ally Choki.Kwamba ifike mahala wanamuziki wetu wajulikane kama ilivyo kwa nyota wa DRC ambao wanatamba barani Ulaya wakiingiza mamilioni ya faranga kwenye mifuko yao.Wamefikia mahala ambako hata kama hawatapiga ukumbini mwaka mzima, wanaendelea kunawiri kwa sababu mauzo ya albamu zao sokoni ni mazuri. Hawana haja ya kuumiza kichwa na viingilio vya buku tatu kwa kila kichwa kama ilivyo hapa kwetu.Uwezo wa kufikia walipo na hata kuwapiku upo ikiwa wanamuziki watakubali kutumia vichwa vyao ipasavyo. Wakibuni na kujipangia mikakati ya ushindi katika majukwaa ya muziki.Mikakati ni muhimu badala ya kupikiana majungu kila siku na kupishana kwa sangoma kusaka mbinu chafu za kuangushana.Huo ndio mtazamo wa Mzee wa Busati. Kwamba wakati wa mageuzi katika muziki ni huu na hakuna haja ya kusubiri miujiza kutoka sehemu nyingine. Ni suala la ubunifu katika tungo na mambo mengine yanayoambatana na muziki.Mwenye Busati anafikia ukomo kwa juma hili akisubiri kwa hamu kuangalia vituko kwenye viunga mbalimbali vya Darisalama na Mji Kasoro Bahari ambako wikiendi huwa njema ajabu.Hakuna kuulizana kila mmoja hujitanua kwa nafasi yake apendavyo na huwezi kujua kama wengine wanavinjari na pesa za mikopo au mafao ya wastaafu wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki.Kuuliza hakuna kwani kila mwenye chake hujipinda awezavyo ila maji yenye rangi ya mende yakishatoweka kichwani ndipo majuto hujaa tele.Lakini kwa kumalizia tu ni kwamba Mzee wa Busati anaomba wapenzi na mashabiki wa Yanga wasiisuse timu hiyo licha ya kutolewa mapema katika Ligi ya Mabingwa Afrika. Endeleeni kushikamana ili kuleta mafanikio katika Ligi Kuu.
Wasalaam,
munyuku@gmail.com
0754 471 920

No comments: