na innocent munyuku
MSANII wa muziki wa kizazi kipya nchini Tanzania Albert Motika maarufu kama Mr. Ebbo alipata kufyatua kibao ambacho wengi walikifurahia kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni porojo zilizojaa kwenye wimbo huo uliopachikwa jina la Mnisamehe.
Katika wimbo huo, Mr. Ebbo anaeleza baadhi ya mambo ambayo kwa akili ya kawaida hayatekelezeki na kama yatatekelezwa basi itakuwa balaa. Kama pale anaposema angefurahi kuona magazeti yote yameandikwa kwa lugha ya Kimasai au mnada wa ng’ombe wa Pugu usogezwe hadi Mtaa wa Samora jijini Dar es Salaam.
Lakini msanii huyo anaendelea kuimba kwamba hata gari moshi zisiwe na honi kwenye safari zake na anaomba apande gari lisilo na breki. Kila anachosema mwisho wake humalizia kwa kutaka asamehewe kwa kauli yake hiyo. Bila shaka ujumbe ulishafika.
Nami kabla sijajikita katika msingi wa makala yangu hii leo naomba nisamehewe kwa hoja yangu kwamba tuzo kwa marais wa nchi iliyoandaliwa na tajiri Mohamed Ibrahim, kwa mtazamo wangu hailengi kufichua ama kuutokomeza ufisadi katika Afrika.
Kwa zaidi ya wiki mbili sasa, vyombo mbalimbali vya habari vimekuwa vikiandika kwa kina taarifa hiyo ya tajiri huyo anayependa kuitwa Mo Ibrahim ambaye asili yake ni nchini Sudan ingawa mwaka 1975 alipewa uraia wa Uingereza.
Tajiri huyo bila shaka kwa nia njema kama alivyoona katika dhamira yake ametangaza kuanzishwa kwa tuzo maalumu ya marais wa Afrika na kwamba rais atakayebainika kuwa anafuata misingi ya utawala bora na kuwawezesha raia wake kuwa na maisha mazuri basi atajinyakulia kitita cha dola za Marekani milioni 5 (zaidi ya shilingi bilioni 5 za Tanzania).
Lakini mshindi wa tuzo hiyo atakuwa pia akilipwa dola za Marekani 200, 000 (zaidi ya shilingi milioni 200) kila mwaka hadi ukomo wa maisha yake.
Binafsi niliposikia habari hizo nilijiuliza mambo mengi na baadaye nikaona si jambo jema kwa watawala wetu kupimwa uwezo wao wa kazi za kuwaongoza wananchi kwa mashindano na ahadi ya mamilioni ya pesa. Hapakuwa na haja hiyo na wala sioni kama umuhimu wa aina hiyo upo katika jamii zetu.
Hata hivyo, wakati naendelea kuwaza jambo hilo nikaikumbuka moja ya hotuba ya mtawala wa zamani wa Afrika Kusini P.W. Botha. Huyu ndiye mwasisi wa siasa za kibaguzi za rangi nchini humo aliyerejea kuzimu hivi karibuni akiwa na umri wa miaka 90. Botha katika moja ya hotuba yake alipata kusema kuwa njia rahisi ya kuziteka akili za mtu mweusi basi mpe mwanamke wa Kizungu na hapo atakupa siri zote.
Lakini Botha hakuishia kusema hayo, katika hotuba yake hiyo na hata katika mazungumzo yake ya kawaida mara kwa mara alisema njia nyingine ya kuuteka ubongo wa mtu Mweusi, mpe zawadi ya pesa na hapo atawajibika hata kama litakuwa suala la kumnyima usingizi.
Katika hilo, Botha hakumaanisha kuwa hakuna mwanadamu asiyependa pesa la hasha! Alichosema ni kuwa ni mazoea kwamba kwa mtu Mweusi hata jambo ambalo ni wajibu wake alifanye katika misingi fulani atapenda apewe ‘kitu kidogo’ ili aendelee kuwajibika. Kwamba anapopigwa ‘mjeledi’ wa pesa mambo hayaendi kombo.
Siku ile nilipoyafumbua macho yangu na kusoma habari kwamba kuna tuzo kwa ajili ya viongozi watakaoonekana kufuata utawala bora, nilipata mshangao kwamba iweje leo hii kuibuke na kitu kama hicho kwa watawala wetu. Nikasema ndani ya mtima wangu kuwa kumbe Botha pamoja na ufedhuli wake alilonena lina ukweli kiasi chake.
Je, urais sasa ni kama mashindano ya Miss World ambako warembo hujiandaa kuanzia ngazi za chini lengo likiwa ni kuibuka kinara kwa wengine? Au urais wa Afrika umekuwa kama michuano ya Klabu Bingwa Afrika?
Kwa ufahamu wangu, viongozi wengi barani Afrika wameingia madarakani kwa kupigiwa kura za ndiyo na wananchi. Hawakuvamia Ikulu na kwa maana hiyo kulikuwa na maandalizi ya uchaguzi kwa kampeni za kuwania nafasi hiyo, kampeni ambazo bila shaka ziliambatana na ahadi juu ya nini watawafanyia raia wao pindi watakapopata ridhaa ya kutawala.
Leo hii, linaibuka la kuibuka kwamba marais wapimwe utendaji wao na kisha wapewe pesa kama zawadi. Huku ni kupotoka! Hawa wamekuwa watoto kwamba hawaendi kuoga hadi wapewe ahadi ya peremende? Wamekuwa watumwa kwamba hawawezi kufanya kazi hadi wachapwe na mijeledi kwenye migongo yao?
Huyu Mo Ibrahim ambaye pia ni mwanzilishi wa Kampuni ya Simu za mkononi ya Celtel kama kweli ana nia ya kuwasaidia watu wake ndani ya Afrika, angeanzia nchini mwake alikozaliwa huko Sudan ambako hali si shwari katika Darfur. Angeanzia huko kama Waingereza wanavyoamini kuwa charity starts at home.
Nionavyo mimi, zawadi ya pesa kwa marais haiwezi kuijenga Afrika hata siku moja. Huo ndio mtazamo wangu na hicho ndicho ninachokiamini. Fisadi ni fisadi tu na hawezi kubadilika eti kwa sababu kaona pesa mbele yake. Kiongozi mwenye nia ya dhati huzaliwa na moyo wa aina hiyo na hujipanga kuwatumikia watu wake kwa haki hata kama itamlazimu kulala sehemu isiyo ya kifahari.
Ninachokiona ni kuudhalilisha utu kwa kigezo cha pesa. Kwamba kinachoonekana hapa si changamoto kama baadhi ya watu wanavyojaribu kuamini bali ni udhalilishaji kwa wakuu wa Afrika.
Kama nilivyodokeza hapo juu kuwa kigezo cha pesa kisiwe hoja ya msingi kuwapima watawala wetu. Mtu mwadilifu aliyepewa dhamana ya utawala wa nchi anatarajiwa kuwa mwenye kuumia na umaskini wa watu, mwadilifu sharti asilale usingizi pale anapoona raia wake wanakufa kwa magonjwa au njaa.
Mwadilifu anapaswa kutokuwa mwenye makuu kwa kujinufaisha yeye wakati raia wake wakikosa elimu na huduma nyingine muhimu za jamii. Lakini katika hili, mwadifu pia ni yule ambaye atafanya na kutimiza majukumu yake pasipo kuwekewa mfuko wa mamilioni ya dola za Marekani mbele yake. Huyu ndiye anayetufaa.
Wenye kuandaa utaratibu huo wamepanga zawadi hizo kwa hao watakaoonekana kuwa watawala bora lakini je, na hao marais wazandiki na wadhalimu watapewa adhabu na nani? Bila shaka kuna mahala mpango huu utakwenda upogo.
Hivi kweli palikuwa na umuhimu wa kuanzisha tuzo hizi kwa wakati huu? Waandaaji hawakuona kuwa upo umuhimu wa kuwajengea mazingira mazuri raia wa kawaida kabisa ambao wamekuwa wakipata wakati mgumu kukabiliana na maisha ya kila siku?
Au tuseme kwamba yale yaliyopatwa kunenwa na Manabii kwamba mwenye nacho huongezewa yanaendelea kutimia? Rais wa nchi awaye yote anapostaafu hupewa mafao yanayomwezesha kuwa na maisha bora kwa kipindi kirefu lakini si mwananchi wa kawaida.
I wapi basi mipango ya kuwakomboa Waafrika kama mambo yenyewe ni haya? Zumari la kuwakataza hao wanaojifanya kuwa wanaidai Afrika madeni makubwa mbona halipigwi tena? Badala yake twaibuka na mambo ambayo kwa mtazamo binafsi hauna jema katika maendeleo ya Afrika zaidi ya kuwadhalilisha watawala wetu.
Sina hakika na akiba ya Mo Ibrahim katika akaunti zake za benki, lakini kama nilingelijua ningelimshauri jambo moja nalo ni kujenga shule za aina mbalimbali ndani ya bara hilo ili kufuta ujinga kwa mamilioni ya watu barani humo.
Lakini pia angeweza kujenga misingi ya kuwainua Waafrika moja kwa moja kwa kuanzisha kampuni ambazo zitatoa ajira kama alivyofanikiwa katika Celtel ambayo kwa sasa imeuzwa kwa wawekezaji wa Kuwait. Hili la kuwashindanisha wakuu wetu wa nchi kwa ahadi ya pesa kamwe sikubaliano nalo. Naomba kutofautiana!
munyuku@gmail.com
0754 471 920
Thursday, January 18, 2007
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment