Thursday, January 18, 2007

Raila kapiga zumari Kenya, tulicheze Tanzania

na innocent munyuku

WANASEMA uzee ni dalili ya hekima lakini pamoja na ukweli huo uzee hauhalalishi kuziba vipaji au mianya ya wengine kuonyesha uwezo wao katika masuala mbalimbali yahusuyo jamii. Basi tuseme pia katika hili uzee waweza kutumika kama mwongozo au mifano sahihi kwa ustawi wa jamii.

Katika hilo ndio maana hadi hii leo kwa baadhi ya kaya huwatumia wazee katika kufanya suluhisho kwenye eneo husika hasa kama kutatokea kutokuelewana baina yao. Pengine kutokana na hilo inawezekana wengine wakadiriki kusema kuwa ukubwa ni jalala.

Lakini katika nyanja za siasa hasa barani Afrika hali ni tofauti. Wazee wameonyesha njia mbaya kwa kung’ang’ania madaraka na huu kwa mtazamo wa kawaida kabisa ni ishara na mwongozo usiofaa kwa vijana wanaochipukia katika siasa na hata waliosimama kabisa.

Nimeamua kuandika haya kwa kusimamia hoja ya Mbunge wa Jimbo la Lang’ata nchini Kenya, Raila Odinga aliyependekeza hivi karibuni kuwa ni vema wanasiasa wa nchini mwake ambao wamekuwa madarakani kwa muda mrefu waachie ngazi na kupisha damu changa.

Odinga alisema kuwa anashangaa kuwaona wanasiasa wa jinsi hiyo ambao hadi hii leo wangali wakishika utawala tangu enzi ya marehemu baba yake Jaramongi Oginga Odinga.

Ingawa Odinga alikuwa akiyasema hayo kukipigia debe chama chake cha Orange for Democratic Movement-Kenya (ODM-K), maneno yake yalitosha kuwa changamoto kwa ajili ya kujenga vyama vyenye damu mpya na mawazo mapya katika siasa.

Nchini humo kwa mfano, Makamu wa Rais Moody Awori ana umri wa miaka 79, huku kukiwa na mawaziri wengine wenye umri mkubwa kama yeye akiwemo Njenga Karume (80), Simone Nyachae (75) na John Michuki (74).

Kimsingi hoja ya Raila si ya kuachwa ipite hivi hivi pasipo kuungwa mkono na katika hili ndio maana nasema kuwa mwanasiasa huyo machachari amelenga sehemu husika kutokana na ukweli kwamba sehemu mbalimbali barani Afrika lina tatizo kama hilo.

Tanzania kama ilivyo Kenya pia ina wanasiasa ambao leo hii wana rekodi ya kubakia katika ulingo huo huku wakiziba ya damu changa zisiweze kuonyesha upeo wao katika nyanya mbalimbali. Hao wamejaa tele na ni kama wamepigiliwa misumari.

Ndani ya Tanzania wapo wanasiasa ambao tangu wengine hatujazaliwa wapo katika ulingo huo wakiendesha maisha yao kwa mgongo wa siasa na hadi hii wangali madarakani kama vile hakuna Mtanzania kijana mwenye uwezo wa kuyatenda hayo ayatendayo huyo aliyeko madarakani.

Naungana na Raila kusema kuwa hii ni dalili mbaya kwa mustakabali wa taifa letu kwani ukweli ni kwamba wanasiasa wa aina hii hawana jipya katika mioyo yao. Hawana jipya la kutueleza, wamebaki na mbinu za kale ambazo kwa nyakati hizi hatuwezi kukubaliana nazo.

Kwamba hawana fikra pevu tena, vichwa vyao pamoja na kwamba wanaweza kuwa na hekima, hawana jema la kuwafundisha wengine. Ni heri kwao wakakubali mabadiliko kuliko kung’ang’ania siasa. Huu uwe wakati wa kuwafundisha wengine. Na kufundisha kuzuri ni kwa kumpisha mwanafunzi kitini na kumwelekeza namna ya kuliongoza jahazi.

Kama wanasiasa wa jinsi hii wameshindwa kuleta maendeleo au kuishauri Serikali husika kwa kipindi cha miaka 20 au 30 leo hii watakuwa na miujiza gani katika kulisukuma gurudumu mbele gurudumu la maendeleo na tija halisi kwa Watanzania?

Hawa wazee wa siasa wana jipya gani leo hii? Watasimama waseme kitu ambacho kwa wakati huu watu watakubali kuwa wanachokinena ndicho sahihi? Lakini hakuna shaka kwamba salamu wamezipata wakati ule wa kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka jana. Baadhi yao nasikia walizomewa na wakalazimika kushuka jukwaani wakiwa wamevaa sura za aibu.

Hivi kwani ni lazima wote wawe wanasiasa? Kwanini wengine wasibaki pembeni na kuangalia vichwa vingine vikiongoza jahazi? Bila shaka zumari la Raila lafaa lisikizwe kwa makini na lichezwe hapa kwenye ardhi yetu ya Tanzania. Tusipuuze kwani alichokisema nchini Kenya ndicho kilichopo hapa kwetu.

Sileti siasa za kibaguzi lakini kwa mtazamo, ufike wakati wazee wakubali mabadiliko si kwa kuwapiga watoto wao (wa damu) bali pia kuwapa nafasi wengine wajaribu kujiwekea rekodi zao. Ninachotarajia kwa muda huu ni hawa wazee wajenge vitalu bora kwa kuwapika vijana kisiasa badala ya kuwawekea vizingiti ambavyo kimsingi vinaliangamiza taifa.

Kwamba wakati huu uwe mwafaka kwa Watanzania kujifunza kutokana na changamoto ya kina Raila na kundi lake. Kwani hawa vijana wasipojifunza leo watapata wapi nafasi hiyo? Wasipojaribu leo watajaribu lini?

Tusione aibu kuwapisha vijana waonyeshe walichonacho kwenye vichwa vyao na kama watateleza huo utakuwa muda mwafaka kuwarekebisha na kuwaelekeza wapite wapi na watufikishe wapi. Kuwabana ni kuwanyima haki yao na huu si utaratibu mzuri wa kukuza maendeleo. Tuwape nafasi hii leo.

Niseme pia kuwa hatujachelewa kufikia kuwapa vijana nafasi. Ni suala la maandalizi ambayo yakianza sasa bila shaka katika Uchaguzi Mkuu ujao wazee watakubali kukaa pembeni na kuwapisha vijana waendelee kukimbiza kijiti cha maendeleo.

Hakika tusione aibu kabisa kuanza kulicheza zumari la Raila. Huo ndio uungwana, kubalini mabadiliko mapema ili heshima yenu isipotee.

munyuku@gmail.com

0754 471 920

No comments: