Friday, January 19, 2007

Eti pesa za Uhuru zililiwa na waliovaa suti!

Na Innocent Munyuku

YAWEZEKANA mkashangaa haya mapinduzi kwenye safu hii. Kwamba iweje kaja mtawala mwingine ghafla bin vuu? Jibu la swali kama hilo ni rahisi. Mwasisi wa ‘Mtaani Kwetu’ kaona jambo la heri kwenda kwao kuongeza nguvu kwani inasemekana ndumba zimegoma kutii amri.

Haya ni maneno ya ‘Mtaani Kwetu’ nami kama mmoja wa waliosikia sina budi kuwahabarisha wengine kwamba mzee mzima kakimbilia Umakondeni kuweka mambo sawa.

Lakini tukiachana na hilo, huku ‘Mtaani Kwetu’ kuna mambo yamekuwa yakisemwa na kwa hakika wanaonguruma na maneno hayo wanaonekana kukerwa kwa siku nyingi. Hawaogopi hawa watu. Ni kama vile wamevaa mabomu tayari kwa kujilipua.

Kinachosemwa ‘Mtaani Kwetu’ ni kwamba kitendo cha kuchangia sherehe za Uhuru wa Tanganyika mwaka jana kimewakera huku mtaani. Wanasema badala ya kukusanya hizo pesa kwa ajili ya tiba hospitalini wao wamezikusanya na kuzitumbua kwa saa chache.

Aliyeanza kunena kero hiyo ni jamaa mmoja ambaye kajitambulisha kuwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam sehemu ya Mlimani. Kasema yeye kanyimwa mkopo kwa ajili ya elimu lakini kumbe Serikali inayo uwezo wa kuwahamasisha wafanyabiashara na kuchangia sherehe badala ya elimu.

‘Mtaani Kwetu’ wamekerwa na jambo hili na kama wangemwona Waziri Mkuu na bosi wake ana kwa ana huku mtaani basi sijui wangemsalimia kwa lugha gani.

Sherehe zimepita na wao kinachowafanya walalame ni kwamba ugumu wa maisha unaendelea. Mwingine akasema eti hayo mabilioni ya shilingi yaliyochangishwa yeye hakuwahi hata kupata maji ya sh 200 pale kwenye Uwanja wa Taifa. Aliambulia ukali wa jua la utosi na kupakana jasho na shombo.

Hayo ndiyo mambo ya ‘Mtaani Kwetu’ ambako si ajabu ukakutana na mtu akaanza kulia tu. Kisa? Ugumu wa maisha! Lakini wapo wanaosema kwamba nafuu basi hizo pesa za Uhuru zingenunua dawa kwa ajili ya wagonjwa hospitalini.

Wangezipeleka hata Mwanamanyala, au Amana na sehemu nyingine zenye kuhitaji ubora wa afya. Hilo fungu lingeweza kununua vitanda na kuwapa nafuu kina mama wajawazito ambao kwa nyakati fulani huku ‘Mtaani Kwetu’ tulisikia habari kwamba kina mama hao hulala mzungu wa nne kwa sababu vitanda havitoshi.

Maneno ya huku ‘Mtaani Kwetu’ wakati mwingine unaweza ukashika kichwa kwa mshtuko manake watu wanatema cheche pasipo hofu. Rafiki zangu Mmachinga ndio kabisa usithubutu kuwasikiliza.

Hawa jamaa baada ya ule mpango wa bomoa bomoa na kuwahamisha kwenye makao mapya, hivi sasa wana hasira na Serikali yao. Wengine imefikia hatua hata ya kujutia kura zao wakati wa Uchaguzi Mkuu uliopita.

Wangali wakilalama kwamba hawakutendewa haki kuhamishwa. Njoo ‘Mtaani Kwetu’ uwasikilize wanavyosema. Wanasema wamepoteza nguvu zao nyingi na hivyo vibanda vilivyovunjwa hawa jamaa wanaokusanya kodi (TRA) walipitisha bakuli zao kutaka malipo.

Ghafla Serikali imewageuka. Wametemwa na huko walikopelekwa wanadai hakuna lolote la maana zaidi ya kuambulia vumbi. Ukija ‘Mtaani Kwetu’ utasikia mengi hadi ukome ubishi.

‘Mtaani Kwetu’ walio wengi ni kama vile wamevuta bangi ya Malawi. Manake husemwa kuwa hii ni kiboko kuzidi ya Musoma au Morocco. Hii ya Malawi ina ubora wa aina yake. Ukivuta ‘inakubangua’ kweli kweli haina utani.

Basi hawa wavutaji ndio waliojaa huku ‘Mtaani Kwetu’ lakini naomba niseme kwamba hizi ni hisia zangu kwani sijawahi kuwafuma wakiwa na hizo bangi ila kwa jinsi wanavyojiamini naona kama vile wana nguvu ya ziada kwenye bongo zao.

Ukija ‘Mtaani Kwetu’ wanaolia sana ni wale wenye matumbo yaso na uhakika wa kumeza kitu kwa kila siku iendayo kwa Mungu. Hawa wanakula wanachokipata na si wanachokitaka.

Ndio manaa huku ‘Mtaani Kwetu’ ni rahisi kuwakuta ‘wanasiasa’ mahiri kwa kupanga safu ya uongozi. Utawasikia wakisema ahh fulani ndiye alifaa kuwa Mkuu wa Kaya. Kisa? Maisha bora waliyoambiwa wakati wa Uchaguzi Mkuu hayaonekani.

Waliambiwa habari za kuongezeka kwa ajira, lakini leo hii huku ‘Mtaani Kwetu’ wanazidi kuteseka. Wamebaki kutafakari kero. Lakini nani alaumiwe? Ajira gani watapewa hawa watu wakati hawana elimu ya kutosha katika vichwa vyao? Wanasubiri rehema za Allah.

Kilichobaki ni kulilia pesa za Uhuru, lawama kwa Serikali kwa kuwakimbiza Mmachinga. Hizi ni nyimbo za kila siku kibwagizo kinaweza kuwa chochote kati hivi vifuatavyo; rushwa, huduma mbovu za jamii hasa katika sekta ya afya.

Mie kama mpiga mbiu sitaacha kuwaeleza wengine juu ya hiki kinachoendelea kusemwa huku ‘Mtaani Kwetu’ ni heri mkayajua manake isije siku mnakuja mnashangaa raia wamenuna na hawataki salamu zenu.

Msije mkashangaa kuona jamaa wamejifungia kwenye vibanda vyao vya ‘mbavu za mbwa’ hawatoki kuwalaki kwenye ziara zenu. Hawakufurahishwa na michango ya Uhuru manake wanasema fedha hizo zililiwa na wenye ubavu wa kuvaa suti na si walalahoi.

Naam, ni lazima tuwajulishe ya huku mtaani kwa sababu wakati mwingi mko katika kupanga mikakati ya kuijenga nchi. Mkitoka ofisini mwaelekea kwenye makazi yenu ambako watu wa huku ‘Mtaani Kwetu’ hawawezi kuja kuwasalimia kwenye makazi yenu.

Mvamizi wa safu hii amefikia ukomo. Kama mapinduzi haya yatapewa baraka basi atabakia ulingoni kwa muda mrefu ujayo. Na hapo itaundwa upya serikali ya mapinduzi ya Mtaani Kwetu. Aliyepinduliwa ataambulia kuwa mshauri mkuu.

Wasalaam,
munyuku@gmail.com
0754 471 920

No comments: