Thursday, January 18, 2007

Maembe anapoikazia buti Bagamoyo

na innocent munyuku

WAMEVUMA kina Marijan Rajab, Mbaraka Mwinshehe, Juma Kilaza na wengine wengi ambao kazi zao za muziki zingali zikitamba katika ulimwengu wa muziki.

Lakini cha ajabu ni kwamba pamoja na mchango wao kuwa mkubwa katika jamii, vijana wanaochipukia katika muziki walio wengi hawataki kujifunza mema kutoka kwa wakongwe hao.

Wamekimbilia kile kinachoitwa muziki wa kizazi kipya muziki ambao kwa asilimia kubwa umebeba ladha ya Kimagharibi na kuacha asili ya Waafrika. Kuanzia nguo zao jukwaani, misemo na majigambo wamechukua kutoka ughaibuni.

Mbaya zaidi ni kwamba hata katika ubunifu wako nyuma kwani walio wengi hawawezi kuimba pasipo kufuatisha santuri zao. Mamia hawajui kupiga ala za muziki ingawa wanajiita wanamuziki.

Hata hivyo, katika miaka ya hivi karibuni wapo vijana walioamua kufuata reli ya muziki wa asili kwa kuweka lafudhi za Kiafrika na kazi zao zimekuwa zikitamba katika sehemu mbalimbali duniani.

Mmoja wao ni Vitali Maembe na kundi lake la The Spirits. Maembe baada ya kuibuka na kuvuma na kibao cha Sumu ya Teja, hivi sasa ameamua kufyatua albamu yake ya kwanza akiipa jina la BAGAMOYO.

BAGAMOYO ina vibao 10 na kwa kuonyesha kuwa albamu hiyo iliyoipuliwa Oktoba mwaka jana kuwa ni moto wa kuotea mbali, katika miezi miwili ya kwanza ilishauza CD 1,000 ndani na nje ya nchi.

Lakini mbali na mafanikio hayo ya muda mfupi, wimbo wake wa Sumu ya Teja umefanikiwa kukaa katika chati za juu ukishika namba sita katika msimamo wa Soundclick World Music Charts.

Nchini Uingereza albamu hiyo imekuwa ikipendwa kutokana na staili ya uimbaji kutoka kwa Maembe. Mmoja wa wachambuzi wa muziki na masuala ya jamii, Fred Macha anayeishi Uingereza amepata kumwelezea Maembe kuwa mmoja wa wanamuziki wa Afrika wanaotakiwa kulindwa vipaji vyao.

Kwamba kwa vile Maembe amefanikiwa kulinda mila na utamaduni wa Kiafrika hana budi kupewa heshima kama msimamizi sahihi wa mila zinazomhusu mtu Mweusi.

Tayari mwanamuziki huyo ameshakamilisha kuzitengenezea video baadhi ya nyimbo katika albamu ya BAGAMOYO. Vibao vilivyowekwa katika video ni Afrika Shilingi Tano, Sumu ya Teja, Toka na Asalaam Aleykhum. Zinazosubiri kuingizwa katika video ni Mbwa wa Kiombwe, Naropoka, Kipande cha Papa, Kinoo na Hamia Ndege.

Lakini kinachowavuta wengi katika albamu hiyo ya Maembe ni kibao cha Hamia Ndege ukizungumzia namna ufisadi unavyoitafuna jamii katika nyanya mbalimbali.

Kwamba rushwa imekuwa kichocheo cha watu kubakia katika lindi umasikini kwani haki au fursa zao za msingi hawazipati kwa vile mianya ya rushwa imetawala.

‘Hamia ndege mpunga wa baba waliwa…ati walimdanganya dada, ati toa penzi ufaulu mtihani. Ati walimdanganya kaka, ati toa chochote upate ajira yako’ haya ni baadhi ya maneno katika wimbo wa Hamia Ndege.

Ukweli ni kwamba kipaji alicho nacho Maembe ni faraja kwa Watanzania kutokana na mashairi anayoyatoa kupitia kipaza sauti. Anazungumzia rushwa, amezungumzia ukoloni mambo leo.

Lakini zaidi ya yote, Maembe ni kipenzi cha watoto na katika hilo kila afanyapo ziara sehemu mbalimbali, nafasi ya kwanza huwapa watoto ambao kwa msimamo wake ndio msingi wa faraja katika jamii yoyote.

Hata hivyo, katika shughuli za muziki kuna kikwazo kwa wasanii mbalimbali wa muziki. Vigingi vinatoka kwa wasambazaji wa kazi zao na urasimu uliojaa katika vituo mbalimbali vya redio na televisheni.

Meneja wa wa Maembe, Gota Warioba anaweka wazi kuwa nchini Tanzania kuna urasimu wa ajabu na wizi wa wazi kutoka kwa wasambazaji wa muziki ambao asilimia 99 si waaminifu.

“Inashangaza kuona kuwa kazi za wanamuziki zinaibwa na hawa wasambazaji. Kwa hiyo sisi tulichoamua ni kusambaza wenyewe na katika hilo tumefanikiwa.

“Nani alipata kuuza nakala 1,000 kwa miezi miwili kwa usimamizi binafsi?” anahoji Gota na kuongeza kuwa wataendelea na msimamo huo hadi mambo yanyooke.

“Tunataka mapinduzi ya kweli katika muziki, wasanii wapate haki yao na si kuwarubuni na kuwaachia umasikini kila leo.”

Lakini mbali na lawama kwa wasambazaji kuna hoja nyingine kuwa baadhi ya watangazaji katika redio na wasimamizi wa vipindi katika televisheni ni wala rushwa.

“Tumeshasambaza CD za Maembe katika redio mbalimbali lakini ni wachache wanapiga nyimbo zake. Hali kadhalika video hazionyeshwi katika televisheni,” anasema Gota.

Gota anasema kuwa ili mambo hayo yafike ukomo wanahitaji mapinduzi ya kweli katika muziki ili mambo yaende vizuri kwa maslahi ya wasanii na taifa kwa ujumla.

Kwamba ifike mahala wasanii wasiendelee kuwa ombaomba na badala yake wawe msaada mkubwa kwa jamii yao. Wawezeshwe ili wapate nafasi ya kuwa na ubunifu wa hali juu.

Ni nani atashika kipaza sauti angali na njaa tumboni? Mwanamuziki gani ataleta mashairi ya hekima wakati mwili umejaa matatizo kwa sababu tu kadhulumiwa na wasambazaji wa kazi zake? Huu ni wakati wa kuyapinga haya.

Leo hii Gota na Maembe wake wanalia, juzi kalia Stara Thomas, mwaka juzi kalia Ras Inno. Wasanii wengine waungane katika kilio hiki ili hawa mafisadi wanaendelea kula kwa mgongo wa wasanii waishie kunako shimo la giza wasipate kuona mbele katika dhuluma yao.

munyuku@gmail.com
+255 754 471 920

No comments: