na mwandishi wetu
BAADA ya kufifia kwa bendi maarufu mkoani Morogoro kama Moro Jazz iliyotamba na marehemu Mbaraka Mwinshehe, mkoa huo ulibaki kama yatima katika masuala ya muziki.
Hii ilitokana na wadau kutotaka au kutokuwa na ari au uwezo wa kumiliki bendi za muziki wa dansi. Matokeo yake, burudani ya aina hiyo ikazidi kushamiri katika jiji la Dar es Salaam.
Lakini leo hii, Morogoro si yatima tena katika muziki wa dansi. Hilo linajihidhirisha baada ya kuibuka kwa bendi mpya ya Mikumi Sound iliyojikita mkoani humo kiasi cha mwaka mmoja uliopita.
Wiki iliyopita nimekuwa shuhuda wa makali ya bendi hiyo inayotumia mtindo wa Tekenya katika mapigo yake wakati ilipotumbuiza kwenye Ukumbi a VIP mjini Morogoro.
Umahiri wao jukwaani huwezi kuamiani kuwa bendi hii inaundwa na wanamuziki wenye usongo wa kujitangaza kimataifa.
Hao ni Sadiq Jakaya anayepiga gitaa la solo, Balely Mohamed anayevuma na gitaa la bass, Toto Site (kinanda), Abeid Said anayepiga drums huku Jose Kigenda ambaye ni rais wa bendi hiyo. Kuna washambuliaji wa jukwaa katika unenguaji hawa ni Monter Bige, Cool Mud, Dogoo Kaisi na Hamis Makata.
Kama ulikuwa ukiwaza kushabikia bendi za Kikongo, bila shaka nuna sababu tena ya kufanya hivyo kutokana na ukweli kwamba muziki wa Mikumi Sound ni kiboko yao. Hawatanii katika fani na wako makini. Wameshafyatua albamu mbili sasa nazo ni Cheo ni Dhamana yenye vibao sita na Mama Mkwe yenye nyimbo tano.
Rais wa bendi hiyo, Jose Kigenda katika mahojiamo maalumu anasema kuwa wanamuziki wake wamekuwa wabunifu kutokana na maelewano baina yao.
“Mikumi Sound si ya wababaishaji na tunawaomba mashabiki waelewe kuwa tumekuja kamili na tumeiva kimuziki,” anasema Kigenda na kuongeza:
“Tunajua mashabiki wanataka nini na hapa Morogoro tumegundua kuwa hawataki mambo ya kuwaiga Wakongo na ndio maana sisi tumeitikia wito kwa kuthamini utamaduni wa Mtanzania.
“Ndio maana kila siku nawaambia kuwa wanaodhani wamesimama kimuziki wakae chonjo, mwendo wetu ni wa taratibu lakini tuko makini sana,” anasema.
Mapema Juni mwaka huu, bendi hiyo iliandaa onyesho maalumu kuipongeza timu ya soka ya Moro United kwa kushika nafasi ya pili katika michuano ya Kombe la Kagame.
Katika onyesho hilo, bendi hiyo iliwapagawisha mashabiki wake kwa vibao kemkem kutoka kwenye albamu ya Mama Mkwe inayoundwa pia na nyimbo za Usiku wa
Deni, Dunia Duara, Mchumba Mwema na Afrika Tekenya
Twist.
Katika kuhakikisha kuwa inabeba mashabiki wengi zaidi, bendi hiyo imeshazuru mikoa mbalimbali nchini kujitangaza. Moja ya ziara iliyofana ni ile ya kuitangaza albamu yake Mama Mkwe.
Lakini hayo yote yasingewezekana kama sio ubavu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Mikumi Sound, Rena Vegula. Huyu kwa watu wengine wanaweza kumwita mwanamke wa shoka kutokana na kutokuwa na woga katika uendeshaji wa masuala ya maendeleo.
“Wazo la bendi lilianzia mjini Arusha mwaka 2003 na lengo hasa lilikuwa kuitangaza Mikumi kama mbuga nzuri Tanzania na ndio maana tukaamua kuipa jina hili,” anasema Rena mama wa watoto wanne; Abel, Erick, Peter na Aneth.
Wakati wazo hilo linaanza mwaka 2003, Rena alikuwa jijini Arusha akiendesha biashara zake. “Nina ukumbi wa starehe pale Arusha unaitwa Ricks Club sasa wakati ule bendi ya Olduvai ilikuwa ikipiga pale.
“Baadhi ya wanamuziki wetu wakawa wanaonyesha moyo wa kuendeleza muziki lakini vifaa hatukuwa navyo, ndipo tukaamua kununua vifaa vyetu.”
Alipoulizwa kama haoni kikwazo kuendesha bendi ya muziki wa dansi, Rena anasema kuwa haoni kikwazo kwa sababu dhamira yake ni kuona muziki wa Tanzania unakua na wanamuziki wake wanapata neema.
“Nikwambie kitu kwamba matarajio yetu ni makubwa sana hadi utashangaa,” anasema. “Mipango tuliyo nayo ni mizuri na tunasikilizana.”
Anasema kuwa hadi sasa, bendi hiyo inajiendesha na hakuna mzigo mkubwa sana kama hapo awali.
Kwa nini basi Mikumi Sound ikahamia Morogoro?
Rena anaeleza kuwa mwaka jana walipata nafasi ya kuiendesha hoteli ya Masuka Village iliyopo barabara ya Boma mjini Morogoro, kwa hiyo wakaamua kuihamishia bendi mjini hapo ili kuwa nayo karibu.
“Hapa tukaona nafasi nzuri ya kuikarabati bendi na hii ilitokana na kupokewa vizuri hapa Morogoro, mashabiki wanakubali na kuipenda kazi yetu.”
Lakini Rena ana msimamo ambao kwa hakika unajenga asili yetu kama Watanzania pale anaposema kuwa hatakubali kuwaajiri Wakongo kwenye bendi yake.
Anasema kimsingi kumwacha Mtanzania na kumwajiri Mkongo katika bendi ni dhambi kwani unamnyima mtu wako wa karibu mkate wa kila siku.
Anasema umefika wakati sasa kwa Watanzania kuthamini watu na vipaji vyao na kwamba hao wa nje hawana muujiza zaidi ya kwamba wanajituma katika kazi zao za muziki.
“Ndio maana ukiingia katika maonyesho yetu moja kwa moja unapata ladha ya muziki wetu na hatutaki kuiga,” anasema na kuongeza kuwa wanataka kuziba pengo la Mbaraka Mwinshehe.
“Tanzania kuna vipaji vingi mno katika muziki, ni suala la kuwaibua hawa wasanii na kila jambo linawezekana, hakuna sababu ya kuiga nyimbo za wanamuziki wa Kongo hii ni aibu kwa taifa.”
Ni mwanamke jasiri ambaye daima ulimi wake hulenga katika ari ya kuthubutu kutenda na kutekeleza masuala ya maendeleo na hilo amefanikiwa kutokana na malengo yake kukubalika pia kwa mumewe anayekwenda kwa jina la Henry Vegula.
“Mume ananielewa na hata watoto pia wanaelewa kwamba kazi ina manufaa kwetu sote,” anasema Rena.
Friday, January 19, 2007
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment