na innocent munyuku
ALIYEKUWA mgombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa Rais na wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi mwaka jana, Dk. Edmund Sengondo Mvungi amesema chama chake hakikuona sababu ya kuandamana kuwapongeza wabunge wa upinzani waliomaliza Bunge la Bajeti kwa kuwa hakuna ujasiri wowote waliouonyesha.
Dk. Mvungi alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita katika mahojiano maalum na Rai, kwenye Makao Makuu ya NCCR-Mageuzi Mtaa wa Kilosa, Ilala jijini Dar es Salaam.
“Tuwapongeze hawa kwa ushujaa upi? Tunawapongeza kwa lipi kubwa?,”alihoji Mvungi na kuongeza:
“Kwangu mimi wamekuwa kati ya watu waliopitisha bajeti ambayo ilikuwa ya hovyo kabisa…angalia suala la mikopo kwa elimu ya juu, kwa nini ukubali vipitishwe vigezo vya kukopeshwa kwa madaraja? Hawa watoto wengine watakwenda wapi?”.
Alhamisi iliyopita vyama vya Upinzani vilifanya maandamano jijini Dar es Salaam na baadaye kufanya mkutano wa hadhara kwenye viwanja vya Jangwani baada ya kuwapokea wabunge wa kambi hiyo waliotokea mjini Dodoma kuhudhuria Bunge la Bajeti.
Akizungumzia upinzani nchini, Dk. Mvungi amesema vyama vingi vya upinzani havisemi lugha moja katika mageuzi halisi kwa Watanzania.
Alisema tatizo la upande wa upinzani ni kwamba viongozi wengi wanakuwa na ndoto ya kwenda Ikulu moja kwa moja bila kuweka wazi nini kinawapeleka huko.
“Mnakaa mnajadiliana kwamba hivi tukikuachia nafasi utawafanyia nini wananchi, una malengo gani utasikia mmoja akisema ahh acha tu tutajua huko huko nikifika.
“Huu si utaratibu mzuri, lazima tuelezwe kwamba wananchi utawafanyia nini na wewe mwenyewe umejiandaa vipi kutekeleza unayoahidi,” alisema na kuongeza:
“Binafsi sikuzunguka Tanzania nzima wakati wa kampeni kwa lengo la kuwa katika historia ya nchi kwamba niliwahi kuwa rais. Hapana. Nilizunguka ili kuwapa raia fikra juu ya nini Watanzania tunatakiwa tuwe.
“Ndio maana nasema hivi kwanza tukae tuambizane, tuaminiane halafu twende mbele. Mageuzi si ya Mvungi tu bali ni yetu sote.”
Akizungumza mafanikio katika miezi takribani minane ya uongozi mpya wa awamu ya nne, Dk. Mvungi anasema hawezi kusema kuwa kuna mafanikio makubwa.
“Jambo jema ninaloweza kusema ni kwamba tumebaki na amani ile ile tuliyoizoea Watanzania. Lakini kwa kweli matumaini katika huduma ya jamii hakuna, hali ni mbaya.
“Tulipoamua kufanya uchaguzi tulitegemea mabadiliko ya maisha ya watu na hatuchagui serikali itupeleke nyuma, bali mbele kimaendeleo.
“Lakini hofu yangu pia ni kuwa huenda kuna waliokwenda kuwachagua watu ili nao waendelee kunufaika na ulaji.”
Pamoja na hayo Dk. Mvungi anasema katika uchaguzi uliopita Chama Cha Mapinduzi kilifanya mapinduzi makubwa ndani ya chama. Mapinduzi ambayo kama yanalenga dhamira njema yanaweza kuisaidia Tanzania.
“Ndiyo kulikuwa na mapinduzi makubwa ndani ya CCM, hawa waliofanya mapinduzi walikuwa makini sana. Hawa ndio wanaojiita ‘wanamtandao’.
“CCM imebadilika, watu wapya kabisa wenye matamanio mapya na ndio maana nasema mchakato wa CCM haukuwa wa kizembe na wala halikuwa jambo dogo lililofanywa na wanamtandao.
“Lakini mimi nasema hawa wanamtandao wana lengo ambalo bila shaka ni kula na bila shaka zile bilioni 21 zilizotengwa kwa ajili ya kusambazwa mikoani zitawanufaisha hawa watu.
“Wanamtandao ni wengi, Rais kishachagua baraza la mawiziri, wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya sasa wengine waliobaki watapewa nini? Bila shaka ni hizi pesa za kifuta machozi.”
Alisema katika mfumo huu wa chama dola, ni CCM ndicho kitakachoamua nani apewe pesa hizo. “Nafikiri wanajipanga hivyo.”
munyuku@gmail.com
+255 754 471 920
Thursday, January 18, 2007
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment