Monday, June 9, 2008

Imbeni ya Daudi na Goliath

Na Innocent Munyuku

LEO ni matumbo joto. Wadanganyika wamekuwa wenye uchu wa kutaka kufahamu utamu au shubiri ya bajeti kwa mwaka huu wa fedha.

Walalahoi ambao kimsingi ndio wenye kwenye nnji hii walishamaliza utabiri wao kwa hitimisho kwamba mwaka huu hakuna unafuu. Wataendelea kusaga meno kwa makali ya maisha.

Mzee wa Busati anachokiona ni kwamba kama utabiri wa walalahoi utakuwa wa kweli basi kazi kubwa ipo. Tujiandae kuwa na ongezeko la vibaka mitaani ambao kwao hiyo ndiyo njia pekee ya kujikwamua kimaisha.

Huo ulikuwa utangulizi kwa Mwandika Busati ambaye leo hii anajutia wema wake kwa watu wa Kibosho. Naam lazima ajute kwani kile kijamaa kinachojiita Mzee wa Kutibua kaonyeshwa mji na sasa anaanza kutusi wajanja wake.

Kwa hakika anachefua kama ilivyo Taifa Stars ambayo sasa ni kama inatembea gizani pasipo na dira inayoeleweka. Enewei huyu atapatiwa dawa muda si mrefu na hakika kilimilimi chake kinafikia ukingo.

Kilichomleta Mzee wa Busati hapa leo ni kilio chake kwa Taifa Stars ambayo juzi imenyukwa bao 1-0 na Cape Verde katika mchezo wa pili wa kuwania nafasi ya kucheza Kombe la Dunia mwaka 2010.

Si utani kwa sasa Wabongo wengi wametumbukia nyongo. Ukipita vijiweni hadithi ni juu ya ubutu wa safu ya ushambuliaji. Wanalalama hadi koo zao kukauka. Wanayo haki ya kulalama kwani wanadhani kuna pahala kocha ameteleza.

Wengine wanasema mpira wa kibongo ulisharogwa tangu enzi zileeeeee. Kwa hiyo ni kama mwendelezo wa nuksi dimbani. Kila wanapojaribu kufurukuta holaa.

Cape Verde wanachekelea kwa ushindi wao mlaini. Manake ilikuwa kama zali la mentali. Mwishoni mwa wiki si ajabu Taifa Stars ikafanywa mbuzi wa shughuli kwenye Uwanja wa Taifa Darisalama.

Mwandika Busati anasema hayo kwa sababu anaamini mechi kati ya Stars na Cameroon ni ngumu kwa upande wa watoto wa Maximo. Tuombe Mungu wakali wanaofanana na Eto’o wasiingie dimbani.

TMK Halisi wao wamekuja na Tatu Bila lakini kwa hili tifu la Cameroon na Stars si ajabu zikawa saba bila. Tusubiri tuone.

Mambo mengine yanachanganya kichwa kwa sababu haiwezekani kila mwaka bongo ndio iwe kichwa cha kujifunzia kunyolea. Hivi ni kweli soka hii imerogwa?

Kwa mechi ya keshokutwa la maana linaloweza kufanywa ni kuamini katika hadithi ya kwenye Biblia kuhusu Daudi na Goliath. Kwamba tusubiri miujiza la kuiangusha Cameroon kwa kombeo kama alivyofanya Daudi kwa Goliath.

Vinginevyo hali itakuwa ya kuchukiza kwa sababu Cameroon hawataki utani dimbani. Nani asiyejua uhodari wao? Kama kuna mwenye shaka na soka ya watu hao basi ana lake jambo.

Mzee wa Busati si mara moja au mbili ameshaweka wazi misimamo yake kwamba kwa soka hii ya kwetu ni heri tuangalie njia mbadala kuliko staili ya kanyaga twende.

Hivi kuna raha gani ya kuingia mashindanoni kila msimu na kutoka kapa? Kwanini taifa likubali kuwa msukule wa soka? Lazima kuwe na mwamko mpya sasa!

Mwandika Busati ameona aanze na hilo kwa sababu limekuwa likimkera kila siku. Wadau waje na programu endelevu ili siku moja Tanzania ing’are katika soka duniani.

Wakati mwingine Mzee wa Busati huwa anawaza na kuwazua kwamba Wabongo waliumbwa kwa ajili ya kuumbuka kwenye michezo? Hivi ndivyo ilivyo?

Bila shaka sivyo ila ukweli ni kwamba watangulizi katika mamlaka ya soka kuna pahala walikosea. Walikosea kwa kuendekeza soga na malumbano na vinara wa Serikali.

Walikosea kwa kuhubiri falsafa ya soka fitna badala ya kuweka wazi programu za maana katika maendeleo ya soka. Muda mwingi ulitumika kusuguana na kulumbana.

Mwandika Busati anakaribia kufikia ukingoni kwa juma hili. Husemwa kwamba jambo jema maishani ni kuandaa mambo kabla ya umauti. Kama ni wosia yafaa uandikwe mapema ili kila kitu kiwe sawia.

Basi Mzee wa Busati ameanza kuandika wosia kwa wadau wake. Mkiona amezimika ghafla mjue kwamba kila kilicho chenu kitaendelea kuwa mikononi mwenu. Ukweli ni kwamba angetamani apate wasaa wa kufufuka siku ya tatu lakini hilo haliwezekani.

Vinginevyo, kaeni na amani ya Mola. Pendaneni na kwa umoja wenu hakuna atakayethubutu kuwaangusha.

Wasalaam,

Sunday, May 25, 2008

Ni dansi au onyesho la vichupi?

Na Innocent Munyuku

BILA shaka mambo yanakwenda sawia. Mwandika Busati kama ilivyo kawaida yake yu safuni kujichanganya na wadau wake katika mijadala ya kila wiki.

Kwa juma hili hakuna shaka kwamba kila kitu kinakwenda vema manake kwenye viti virefu umati umejaa. Lugha zinagongana kwa tambo za kila aina.

Ukipita kwingineko pia watu wanaringa, wakipita kila mahala kwa matao. Utawaambia nini wakati mifuko imejaa shilingi? Muda wa mavuno umewadia na kwa walio wengi kila kitu kinawezakana kwa sababu fedha inaongea.

Mzee wa Busati kama kawaida yake kila siku kwake ni sikukuu. Si kama anazo nyingi bali amejiwekea mfumo usiohitaji makuu. Yeye na vitegemezi vyake hata wakila dagaa na dona yatosha. Vipapatio vya kuku ni majaliwa.

Siku chache zilizopita Darisalama ililipuka kwa burudani ya muziki wa dansi. Mbwembwe kila pahala, mashabiki wa Akudo Impact na FM Academia wakatambiana kila walivyoweza.

Miamba hiyo ya muziki wa dansi ikapiga maonyesho kwa siku moja. Mashabiki wakapagawa kama inavyokuwa kwa Simba na Yanga. Hata leo hii bado simulizi ya maonyesho hayo zinarindima.

Pamoja na mashabiki kupata uhondo huo, Mzee wa Busati ana lake jambo kuhusiana na maonyesho hayo. Jambo lenyewe ni nidhamu ya mavazi jukwaani.

Kilichotokea kwenye majukwaa wakati wacheza shoo wakifanya vitu vyao ni aibu ya mwaka. Mwandika Busati anazungumzia vichupi vya kina dada waliokuwa wananengua.

Hivi kweli huu ndio mfumo mliojiwekea? Wa kupanda jukwaani mkiwa nusu uchi? Akudo na FM Academia wanaweza kutoa jibu kwa swali hili.

Kibaya zaidi ni kwamba katika maonyesho hayo walikuwapo watendaji wa Serikali ambao walijumuika na mashabiki wengine kushabikia muziki uliokuwa ukiporomoshwa. Hakuna siri kwamba hata hao vichupi waliviona.

Je, wamechukua hatua gani juu ya hilo? Hivi muziki huo wa Kikongo hauchezeki hali kuonyeshana mipaka ya Ikulu?
Mzee wa Busati yu radhi aitwe mshamba, wa kuja na majina mengine lukuki lakini hili la kuonyeshana nyeti jukwaani hakika atalikemea. Raha i wapi basi kuonyeshana ya faragha?

Ipo siku wataingia na kuvamia jukwaa wakiwa uchi wa mnyama. Hilo litatokea kwa vile husemwa kuwa dalili ya mvua ni mawingu. Hawataona ugumu kufanya hivyo kwa sababu watakuwa wameshakuwa sugu na uovu wao.

Shingo zao zimeshaanza kuwa ngumu na ndio maana hawaoni soni kusasambua mbele ya hadhara na wanapopigiwa kofi akili zao hucharuka na kuwaka tamaa ya kuzidisha misasambuo.

Zi wapi mamlaka za kusimamia maadili katika sanaa? Hao nao wamekaa kimya. Wamejifungia kwenye vyumba wakijadili namna ya kula fedha za semina.

Hawana mawazo ya kukemea watu wanaokosa maadili jukwaani. Hivi muziki wa aina hiyo sharti wanawake wacheze kwa kuonyesha nyeti zao? Hii maana yake nini?

Au tuseme kwamba dunia ndivyo ilivyo? Kila mmoja yu huru kufanya atakalo ili mradi linaungwa mkono na hadhira. Mwandika Busati haelewi yanayoendelea zaidi ya kumuumiza kichwa.

Basi kama mmeamua kukaa kimya pasipo kukemea, Mzee wa Busati hatafumba mdomo atayasema kwani historia ndiyo yenye kutoa hukumu. Vijukuu vitaelezwa kwamba kibabu chenu hakikupenda mambo fulani.

Huu ndio mwisho wa hoja yake kwa juma hili. Kama ilivyo kawaida yake, Mzee wa Busati anaenda mafichoni kula raha. Ndio manake maisha haya ni mafupi linalowezekana leo lisingoje kesho.

Acha akajitafutie makazi ya faragha kwa kufanya tathmini wakati huu tunapokaribia nusu mwaka. Je, ahadi na mipango ya mwaka 2008 inakwenda sawia au inakwenda upogo?

Vinginevyo kila la heri. Baraka zikufikie hapo ulipo na tuonane juma lijalo tukiwa na siha njema.

Wasalaam,

Sunday, May 18, 2008

Chonde msimu huu msiyaige ya kifaurongo


Na Innocent Munyuku

ASIKWAMBIE mtu raha ya mjini sharti uwe na ngwenje kibindoni. Utakula unachotaka badala ya kula unachopata. Hayo ndo maisha ya mjini.

Lakini wakati mwingine raha hizo hugeuka karaha pale unapoona kuwa wenye kufanya matanuzi wengi wao wamezipata fedhwa kwa njia zisizo halali.

Hao ndio waliojaza miji miaka hii. Wanatumia fedha haramu kufanya matanuzi na kibaya zaidi ni kwamba wanatumia ngwenje hizo hizo zinazonuka kujitakasa.

Kujitakasa kwao kunakuja kwa njia ile wanayoiita eti misaada kwa yatima na wasiojiweza. Hivi kweli sadaka zenu zinakubalika kwa Muumba?

Kilio hiki cha Mzee wa Busati kimekuja baada ya kufanya kajitafiti kiduchu na kubaini kuwa katika maonyesho mengi ya burudani yanayopangwa na kukamilika, mpangilio mzima umejaa dhuluma.

Pengine mfano mdogo tu ni pale unapoona wajanja wa mashindano ya urembo nchini wanapomaliza kukusanya viingilio na kisha kujifanya kusaidia yatima.

Ukweli wa mambo ni kwamba ukiangalia mchakato mzima wa mashindano hayo hadi fainali kwa walio wengi wamepitia dhuluma. Watawalaghai wadhamini na washiriki pia. Hivi kweli huu ni uungwana?

Anachosema Mzee wa Busati ni kwamba dhamira ya misaada ya aina hiyo iendane na uhalisia wa wanaopewa misadaa katika jamii.

Mwandika Busati angali akielea hapo hapo katika ulimbwende kwa hoja kwamba misaada hiyo inayotolewa ni kweli kwamba inawasaidia walengwa? Pipi ni biskuti?

Hivi ni kweli kwamba yatima wanahitaji sana peremende na biskuti? Hiyo iwe ziada ila la msingi liwe kuwajali katika elimu ili maisha yao yawanyokee huko mbele ya safari.

Si waandaaji wa urembo tu wenye hulka ya kutenda hayo bali asasi nyingine za kijamii ambazo wakati mwingine hutumia yatima kujitangaza. Huku ni kupotoka.

Mzee wa Busati ameamua ayaseme haya mapema kwani kwa uzoefu wake watu wa aina hiyo kila mwaka wamekuwa wakiiga maisha ya kifaurongo.

Kifaurongo au pahala pengine hujulikana kama kiforongo ni mdudu ambaye kwa kawaida hupatikana katika kokwa ya embe na hujikinga kwa kujifanya amekufa pindi aguswapo.

Hivyo ndivyo walivyo hao wanaosemwa na Mwandika Busati. Wakiguswa kwa kuelezwa ukweli hukaa kimya na kujifanya hawasikii ama wamelala fofofo.

Hujifanya hamnazo kwa kutojali wanayoambiwa kuhusu mwendo wao katika jamii. Leo hii utakemea juu ya rushwa ya ngono, kesho wanayarudia na hivyo kwenda mbele miaka kibao ijayo.

Kwanini waendelee kuziba masikio? Au hawa si wenzetu katika jamii? Mitima yao i migumu kiasi gani? Mkiguswa leteni mshituko na si kujifanya mmekufa.

Mwandika Busati ataendelea kuyasema anayoyaona kuwa ni mabaya na hataacha kuyasifu yaliyo mema. Anafanya hivyo ili kutoihadaa dhamira yake.

Dhamira anayoisema ni ile ya kutumia vipaji mbalimbali kuwasaidia mambo ya msingi wasiojiweza na si kuwapa yanayoyeyuka kwa siku moja.

Hima uwe mshikamano, wasanii na wabunifu wa aina mbalimbali wajenge msimamo wa kuwasaidia kwa dhati yatima walio vituoni na wale wanaolala majalalani. Kama ni peremende basi viongwezwe na vingine vya kuwajengea maisha.

Mwandika Busati wakati anaelekea ukingoni atoe pongezi zake kwa Taifa Stars kwa kuinyamazisha Uganda Cranes. Basi na wakaze buti, wasiogope fangasi ili wakanuse ardhi ya Ivory Coast katika fainali za Kombe la Mataifa Afrika.

Mzee wa Busati atashangaa kama kutakuwa na porojo tena msimu huu. Amkeni na kasi iwe ya mbele kwa mbele.

Huu ndio ukomo wa Mzee wa Busati kwa juma hili. Wiki ya maumivu kwa walio wengi na mifano iko wazi tu. Idadi ya wanaoning’iniza miguu kwenye viti virefu imeshuka. Wametoweka kama ndui.

Mzee wa Kutibua na jopo lake pale Tabata Relini wameingia mitini. Simu zao zimezimwa kwa kuhofia madeni. Ila huziwasha usiku wa manane kwa ajili ya kusoma meseji. Poleni ila ipo siku mtajuta na kusaga meno.

Kama kwenye ule mlima mrefu kuliko yote barani Afrika hakuendeki basi ni heri mwende pachoto mkakusanye mabibo mtengenezee uraka ili mjidunge kwani hamkani fedhwa ya lager hamnayo!

Wasalaam,

Sunday, May 11, 2008

Bado tuendelee kuisubiri kastabini?

Na Innocent Munyuku

KUMEKUCHA! Ni Jumanne nyingine ambayo Mwandika Busati anatua kwenye anga zake za kujidai kwa ajili ya kuleta porojo zake.

Wiki imeanza vema ingawa siku kadhaa zilizopita mambo yamekwenda upogo. Ngwenje zimeanza kuyeyuka kwani kuna mengi ya kutekelezwa yamefuata mkondo. Suruali zimekuwa tupu.

Waliokuwa na ubavu wa chips na kuku wa kompyuta sasa wanalamba ugali na maharagwe ya Mbeya kwa sababu hata mkaa wa Msata haupatikaniki! Bei juu kwa kila kitu.

Hali inatisha wajameni na kama twafundwa juu ya kusoma alama za nyakati hii ni wazi kwamba Bunge la Bajeti nalo msimu huu litajaa maumivu. Kama vipi mlalahoi kapige debe upate mlo!

Mzee wa Busati wiki hii hoja yake kuu ni juu ya haya mashindano ya Kombe la Taifa yanayoendelea kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Maelfu wanakenua meno lakini kuna jambo haliko wazi.

Mzee wa Busati kasoma magazeti, kasikiza maoni ya wanaojiita kuwa ni wadau wa soka ingawa wanaonekana kujikita kwenye taarabu na muziki wa dansi. Eniwei wasihukumiwe kwa hayo kwani bongo husemwa kwamba hakuna spesholaizesheni.

Kila mmoja na lwake na ndio maana leo unaweza ukamwona Momburi akinywa Kilimanjaro badala ya Safari lager aliyoizoea anachojali ni ulabu wa kulipua ubongo wake ili kesho yake ahangaike kusaka ilipo supu ya mapupu.

Ni kwamba bongo hapa kila jambo linakwenda hata kama halikupangwa liwe hivyo. Na kwa mantiki hiyo usishange waziri fulani nyeti akienda kuwa mgeni rasmi kwenye Kipaimara.

Ataacha shughuli nyeti za kitaifa na kukimbilia huko. Huyo bila shaka anakuwa amesahau kuwa kuna yatima wanaosubiri japo mkono wake waushike nao wafarijike.

Waziri kama huyo amesahau kula na watoto wa mitaani ambao daima mlo wao uko jalalani. Hayo yote yamesahaulika na wakuu wetu wa kaya. Wamebaki kukumbatia urafiki na kwenda kuhudhuria ubarikio wa washikaji zao na kuwavuta wanahabari kama vile ni suala la kitaifa.

Hata hivyo, porojo za Mzee wa Busati hazilengi kuwashukia hao juma hili. Anawaweka kiporo wazidi kuharibu ili siku ikifika apate mengi ya kutema kwenye ndimi zake. Acha wawekwe kiporo.

Wiki hii anachosema Mwandika Busati ni kuhusu hayo mashindano ya Kombe la Taifa. Kwamba hivi lengo haswa ni nini?

Shirikisho la Soka Tanzania-TFF halina budi kuweka wazi maana halisi ya mashindano hayo kwani sasa washika kalamu na wadau wengine wa soka wamekuwa wakisagana kuhusu kiini cha michuano hiyo.

Ukikutana na nasoro utakwambia kuwa ni ya kusaka vipaji lakini wakati huo huo Mwakatobe atasema kuwa ni ya kusaka fedha za kuisaidia timu ya mkoa. Ukweli ni upi?

Mdau mwingine wa soka majuzi katanua msuli wa koo akasema eti mashindano hayo si ya kuibua vipaji na kwamba kama kuna michuano maalumu ya kufanya hivyo. Akaitaja kuwa ni Copa Coca Cola.

Lakini pamoja na mchanganyiko huo wa habari bado Mzee wa Busati anaamini kwamba mashindano hayo hayakupaswa kuwashirikisha wanasoka ambao tayari wamevuma Ligi Kuu Tanzania Bara.

Michuano hiyo ingabakishwa kwa ajili ya ndugu zetu wa Pachoto ama Kigoma ambao hawana mwanya wa kushiriki mashindano ya kimataifa kama hayo.

Hivi kweli kulikuwa na umuhimu kwa timu ya Mkoa wa Ilala kuwajaza nyota wa Simba na Yanga? Hii maana yake nini? Kwani ndani ya Ilala hakuna wanasoka chipukizi wa kuuwakilisha mkoa huo?

Anachokiona Mzee wa Busati ni kwamba michuano hiyo imebakwa na kuna haja ya TFF kujipanga na kuweka kanuni.

Kama Mwandika Busati angelikuwa na mwanya wa kupendekeza angelisema kwamba mashindano hayo waachiwe wanasoka wasiovuma ili miaka ijayo wanasoka waliofichika waongeze bidii watambulike katika ushiriki wao.

Kwa wajuvi wa Kiswahili, kastabihi husemwa kwamba ni chombo cha chuma au plastiki kinachowekwa kwenye ncha ya kidole cha shahada wakati wa kuingiza sindano katika kitambaa wakati wa kushona ili sindano isichome. Pahala pengine, kastabini huitwa subana ama tondoo.

Na ndio maana Mzee wa Busati anasema kwamba bado wadau wa soka wanapaswa kuwa na subira. Wasubiri ujio wa kastabini na waache wenye ubavu wa kupanga yasopangika waendelee na mambo yao.

Vinginevyo papara italeta yasiyoelezeka. Hadithi ya kupanda kwa soka itakuwa yenye ukakasi wa kimbunga na kilio cha kusaga meno.

Wasalaam,

Sunday, May 4, 2008

Hata walimbwende wanaulea ufisadi

Na Innocent Munyuku

USIOMBE kuzimika ghafla kwenye steji. Ni kama vile kifo cha penzi kinavyokuwa. Ni shubiri kwa kwenda mbele. Msosi hauliki mwanawane.

Mzee wa Busati kaleta kero, alitokomea gizani na mbaya zaidi ni kwamba hakuwa na uungwana wa kutoa neno la kwaheri. Yalomkuta ni siri yake ila ukweli ni kwamba kishapewa notisi yenye maelekezo machungu.

Watoa notisi ambao ni wadau wake wamemweleza wazi kwamba kama akirudia kutenda aliyoyatenda yaani kuzimika pasipo taarifa basi asubiri kumwagiwa upupu. Hakika ni adhabu kubwa.

Kwa hakika Mzee wa Busati anastahili adhabu kwani huo kwa kweli ni uhuni kama afanyavyo Mzee wa Kutibua ambaye yeye anaweza kuamua kulala popote hata kama kaunta kilevi kikimkolea. Ipo siku atajuta!

Tuachane na hayo, bila shaka wadau wameelewa somo kwani kuzimika kwa Mwandika Busati hakukuwa katika utani bali alikuwa akiwajibika katika masuala mengine ya kitaifa kule Idodomya kwenye jengo linalopitisha sheria. Mhh samahani wanasema ni jengo la watunga sheria.

Huko Mzee wa Busati kawa shuhuda wa mambo mengi, mema na mabaya. Ila alilofurahia Mwandika Busati ni kuona kuwa kumbe kuna majimbo ya uchaguzi ambayo ni kama hayana wabunge.

Kwamba yaliyo mengi yana wawakilishi bubu, hawasemi hawa, ndimi zao zimenasa wasipate kutoa sauti hata ya kuuliza suala mojawapo la jimboni kwake.

Mbaya zaidi ni kwamba kati ya wabunge hao ‘mabubu’ wanatoka sehemu ambako umasikini umekithiri. Cha ajabu ni kuwa wabunge waliotoka kwenye neema ndio wanaopaza sauti kudai tija kwa wapigakura wao. Hakika wonders will never cease.

Anyway hebu sasa turejee kwenye porojo zetu za kispoti na burudani. Hayo ya siasa hayafai manake unaweza ukijikuta unabadilishwa jina muda si mrefu. Wenye majimbo wasije wakatukimbiza mjini.

Pamoja na Mwandika Busati kuwa kimya kwa zaidi ya majuma mawili, ukweli wa mambo ni kwamba amekuwa karibu na kila jambo linalopita mjini.

Mojawapo ni haya maandalizi ya kusaka vimwana katika hatua za vitongoji na hatimaye kuingia kwa shindano la taifa la kigoli wa Tanzania.

Mawakala wa vitongoji wameshaanza kuingia mtaani kusaka fedha na mambo mengine ya kukamilisha mashindano. Mabingwa wa kuandika propozo za kuomba udhamini huu ni wakati wao wa kujidai.

Mabingwa wa kuongeza cha juu nao ni wakati wao wa kujaza matumbo kwani raha ya udhamini kwao nafasi zao ni kujaza fedha mfukoni ili mambo yawaendee sawia.

Hata hivyo, kwa mtazamo wa Mwandika Busati ni kwamba kuna ulazima wa kuweka mikakati ya makusudi katika maandalizi hayo hasa kutokana na historia ya mashindano hayo nchini.

Kila mwaka kero huwa ni zile zile; kashfa za ngono, upendeleo usio wa lazima katika kuwapata washindi na wakati mwingine utapeli kwa baadhi ya mawakala.

Ndimi za baadhi ya mawakala hujaa neema wanapotangaza mbele ya vyombo vya habari juu ya kuwapo kwa zawadi nono.

Watasema habari njema wakijitakasa kwamba msimu huu mambo ni shwari na zawadi ni za kutakata. Hata hivyo, kwa bahati mbaya huwa ndivyo sivyo.

Huu si mpango mzuri kutokana na ukweli kwamba kama ulaghai huu hautapigiwa kelele, ipo siku yatakuja mabaya zaidi na hivyo kuondoa maana nzima ya kuwa na michuano ya aina hiyo.

Lakini pendekezo la Mwandika Busati ni kwamba wakati mawakala wa urembo wenye damu ya kidhalimu wakipigiwa kelele, ni vema washiriki wakawa mstari wa mbele kusema kwamba kuna uvundo ndani yake.

Wakinyamaza na kuacha yapite maana yake ni kwamba mizizi itazidi kupata nguvu na hivyo kukomaza ufisadi katika sanaa hiyo.

Kina dada washiriki wawe mstari wa mbele kukataa udhalilishwaji kama utajitokeza kambini. Hali kadhalika wakinusa rushwa ya ngono wainue ndimi zao na kusema na wala wasikae kimya.

Na kwa kufanya hivyo, idadi ya wahuni katika urembo watapungua kama si kutokomea kabisa.

Mwandika Busati anafikia ukomo. Anajituliza akiangalia neema zinavyomshukia kama mvua za masika zinazoendelea.

Wanaosema kuwa huu ni mwaka wa shetani wafikirie mara mbili mbili. Wanaweza pia kujitakasa kwa maji ya bahari ili kuondoa nuksi.

Wasalaam,

Sunday, March 30, 2008

Wanjamanga si dawa ya chongo

Na Innocent Munyuku

KATIKA uso wa dunia, mwanadamu kapewa akili inayomwezesha kupangilia mambo mbalimbali maishani mwake.

Hata hivyo, husemwa kwamba akili ni nywele kila mtu na zake. Hii maana yake ni kwamba si rahisi mkafanana mawazo na ndio maana katika jamii huzuka mijadala ya mabishano.

Lakini kwa kutumia akili hiyo hiyo binadamu amekuwa fundi au mahiri wa kugeuza mambo fulani. Mtu mwenye ukurutu kwa mfano atajitahidi kuficha maradhi hayo kwa kuvaa gubigubi.

Hali kadhalika kwa mwenye mapunye kichwani haishangazi akionekana na kofia au kilemba. Hizo zote ni mbinu za kuficha maradhi hayo mbele yaw engine.

Lakini kuna mengine hayafichiki kama vile chongo. Mwanawane hata kama utapaka wanjamanga, chongo halifichiki kama lilivyo pembe la ng’ombe.

Mzee wa Busati kaibuka Jumanne hii ya ‘wajinga’ akiwa na hoja juu ya ukuzaji wa soka ndani ya Tanzania ambayo kimsingi ni kama vile wadau wanatwanga maji kwenye kinu.

Mengi yamekuwa yakisemwa kwa mbwembwe juu ya ukuzaji wa soka ndani ya bongo lakini ukweli wa mambo ni kwamba mbwembwe hizo ni danganya toto.

Kinachofanywa na viongozi katika mamlaka za soka ni sawa na kuficha chongo kwa kupaka wanjamanga. Porojo zimejaa kila mahala na ndimi zao zimejaa ushawishi wa giza.

Angalia msimu wa usajili unapowadia. Balaa mtindo mmoja. Viongozi wa klabu ndio wenye kimbelembele cha kuchagua wachezaji wanaodhani wataifaa timu yao.

Wanafanya hivyo bila kuwapa nafasi makocha katika suala la usajili. Matokeo yake ni kwamba si ajabu ukakuta timu haina beki mahiri kwa sababu pengine viongozi waliamua kuwajaza washambuliaji pekee.

Leo hii viongozi wa klabu wamekuwa kama miungu watu. Wengi wao hawana hata sifa za kuitwa viongozi wa soka. Hawafai waitwe hivyo kwa vile hawana taaluma ya mpira wa miguu. Wanachojua ni kupiga soka na kueneza ufitini.

Kwani hamjapata kusikia kuwa kiongozi fulani kaidhinisha adhabu kwa mchezaji pasipo sababu za msingi? Yanatokea kila leo na yangali yakiendelea.

Mwandika Busati anachosema ni kwamba kauli nyingi za zinazohubiri makuzi ya soka hazina maana kwa sasa kama mamlaka zinazohusika hazitaangalia kiini cha udumavu wa medani hiyo.

Haina maana kusema kwamba Wabongo wajipange kucheza fainali za Kombe la Dunia huku viongozi wababaishaji wasioweza hata kuchanganua mambo wakiendelea kukalia viti hivyo.

Anachonena Mzee wa Busati ni kwamba linapokuja suala la kukuza soka watoa hoja waangalie watokako, walipo na mwelekeo mbele yao.

Siku chache zilizopita, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Joel Bendera katoa mapendekezo yake katika mbio za kuboresha soka nchini.

Bendera amesisitiza umuhimu wa kuwashirikisha waamuzi na madaktari katika mafunzo ya soka. Kwamba wadau hao wapewe mafunzo ya mara kwa mara.

Huo ni mtazamo chanya unaungwa mkono na Mwandika Busati lakini bado ipo haja ya kuangalia magugu yaliyojaa ndani ya klabu mbalimbali za soka na vyama vyake.

Hatuwezi kuwa na mng’aro katika soka huku walioshika nafasi za uongozi wakiwa wapiga soga wasiokuwa na dira ya maendeleo.

Matokeo yake ni kwamba klabu nyingi zimebaki kuwa makaburi ya wachezaji kwa sababu viongozi wake wamekosa mwelekeo wenye neema. Hao kazi yao ni porojo na mahubiri ya ‘soka fitna’.

Kubebana na kuficha maradhi kwa kuvaa gubigubi hakutasaidia kwani ipo siku mambo yataharibika zaidi ya leo.

Leo hii bado kuna viongozi wa klabu za soka wanaoendelea kuamini ushirikina katika mchezo huo. Hawapeleki timu dimbani pasipo kuwalaza wachezaji makaburini au kuwanyoa nywele za kwapa.

Je, kwa sampuli hii ya uongozi mwadhani mtapaa kwenye ndege ya mafanikio ya soka? La hasha! Mtabaki kama mlivyo.

Mzee wa Busati hana budi kukunja jamvi. Ajiendee porini kwake kwa mapumziko akiamini kwamba somo limeeleweka.

Kwa walionaswa katika Siku ya Wajinga leo hii poleni kwa kujazwa ujinga. Vinginevyo muwe makini msimu ujao.

Wasalaam,

Saturday, March 22, 2008

Hamkani baadhi mnaitumikia ngono

Na Innocent Munyuku

KUMEKUCHA! Mzee wa Busati katumbukia kwenye buti tayari kwa mwendo wa kila Jumanne. Kwake mambo yako sawia ingawa anaelewa kwamba wapo waliopata majereha kiduchu kwenye pochi zao wakati wa ufufuo wa Bwana Yesu.

Hata hivyo, uhai ungalipo pumzi ya Mola inashuka. Hata kama mlo ni wa shida hayo ni majaribu na mapito ambayo mwenye kutoka damu sharti akumbane nayo.

Kina Momburi bila shaka sasa wanatweta hawajui watafikaje Tabata Relini. Si mchezo papake Mwanyamala hadi Tabata kwa mguu! Yataka moyo mwanawane.

Bila shaka sasa wanatembeza bakuli wakitoa sera tamu tamu ili wapate kufika tarehe njema za mwajiri. Lakini analoomba Mzee wa Busati ni kwamba msije zua misiba ambayo haipo ili mpate ngwenje za matanuzi. Mkitenda hayo mtakosa thawabu.

Juma lililopita Mwandika Busati alinena juu ya ukakasi wa sanaa hasa ya maigizo na mchezo wa ngono katika eneo hilo.

Akaweka wazi kwamba baadhi ya vikundi hivyo vya maigizo hasa vinavyoonyesha kazi zao kwenye runinga vimekuwa na mchezo mchafu wa kuwalazimisha ngono kina dada (waigizaji) ili wapate nafasi ya kuonekana kwenye vioo vya televisheni.

Na moja ya aya katika makala hayo ya juma lililopita ilisomeka hivi: “Mambo kama hayo kwa hakika yanasikitisha na kutia kichefuchefu. Kwamba kama viongozi wa vikundi fulani vya sanaa wanafikia hatua ya kudai rushwa ya ngono hii ni aibu.”

Kuanzia mwanzo wa waraka huo wa hadi mwisho hakuna pahala Mwandika Busati ametaja kikundi fulani au jina la kiongozi anayeendekeza ukware.

Lakini cha ajabu akaibuka mtu mmoja aliyejiita kiongozi wa kikundi cha sanaa za maigizo na kumtuhumu na kisha kumhukumu Mwandika Busati kwamba hakufanya kile yeye alichokiita ‘research’.

Akahitimisha hivyo kwamba katika sanaa ya maigizo mambo hayo hayapo. Mzee wa Busati naye akapata wasaa wa kuuliza iweje aitwe mdanganyifu?

Hiyo njemba ikadai eti kwa vile sikuwapa nafasi viongozi kupata maoni yao!(?). Akasisitiza hilo kwamba sikuwahoji viongozi wa makundi kisa Mzee wa Busati hakufika kwake!

Yeye ni nani hadi alazimishe kufikiwa? Pengine angesema kwamba yeye ndiye kinara wa viongozi wa vikundi vya sanaa nchini basi hoja yake ingekuwa inaelekea kwenye ukweli.

Kwani ni lazima kila kile alichokiita ‘research’ afikiwe kila mmoja? Twaangalia uwingi wa matukio na kama yeye hafanyi hivyo basi Muumba amrehemu.

Lakini ukweli wa mambo ni ule ule kwamba HAMKANI ndani ya sanaa kuna baadhi ya matukio ya kulazimisha unyumba ili binti fulani apate nafasi

Hata katika baadhi ya filamu za Kibongo nako ni kama shambiro kwa maana ya sehemu ambayo hufanyika mambo ya hovyo hasa yahusuyo ukahaba au uhuni ufananao na huo.

Mwandika Busati alitarajia kwamba jamaa aliyejiita kiongozi wa kundi la sanaa la maigizo angeleta hoja ya ushirikiano ya kukemea hali hiyo na si kushutumu na kisha kuhukumu kwamba Mwandika Busati hajui alichokinena.

Leteni hoja mezani tusemezane na si kujitakasa kwa maji ya bahari.

Haya si mashambulizi la hasha! Kinachosemwa na Mwandika Busati ni kwamba yafaa wakati mwingine kujadili ndani ya nafsi kabla ya kupayuka kwamba fulani katema urongo.

Au mpaka siku zipigwe kura za siri ndipo mpate kusadiki yasemwayo na Mzee wa Busati? Mwandika Busati aseme uwongo ili iweje?

Mlitaka asiseme ili iweje? Nanyi kuweni wadadisi na hakika mtayabaini haya kwamba yapo baadhi ya makundi ambayo hongo ya ngono imetawala.

Ndio maana juma lililopita ikawekwa wazi kwamba hawa si wasanii kwa sababu wameingia humo kiufisadi. Wamevaa joho lenye udhalimu ndani yake.

Habari ndiyo hiyo kwamba haya yasemwayo yapo na yanaendelea kufanyika. Kukaza koo na kusema kwamba fulani kasema uwongo bila shaka ni kutotenda haki.

Mzee wa Busati amefikia ukomo kwa juma hili akitaraji maoni kutoka kwa wadau.

Lakini jambo moja lililo wazi ni kwamba yu radhi hata ikibidi kupigwa mawe akitetea hoja yake. Hakuna urongo hapa. Wasanii wengi wa kike ni mashuhuda na haya.

La maana ni kuangalia namna ya kuangamiza kirusi hicho. Kufumba macho kwa joho la utakaso ni kuiangamiza sanaa.

Kila jema liwashukie wadau wa safu hii. Kwa waliojeruhiwa na Pasaka kubalini hali halisi mtajipanga mwaka ujao.

Wasalaam,

Sunday, March 16, 2008

Mwaigeuza sanaa kuwa shambiro?

Na Innocent Munyuku

KWA wajuzi wa Kiswahili, shambiro hutajwa kuwa ni sehemu ambayo hufanyika mambo ya hovyo hasa yahusuyo ukahaba au uhuni ufananao na huo.

Aghalabu shambiro huwa ni nyumba au pengine yaweza kuitwa danguro maalumu kwa kufanya umalaya.

Hilo ndilo shambiro. Wakware watajazana humo wakishindana kwa uovu wa kila aina. Hiyo ndiyo meli yao.

Mzee wa Busati juzi kasoma kwenye gazeti moja kwamba baadhi ya wasanii wa kike nchini wamekuwa wakilazimika kutoa uroda ili waonekane katika luninga.

Kwamba ili msanii wa kike apate kuonekana katika igizo fulani kupitia televisheni basi lazima avuliwe chupi.

Sharti atoe unyumba kwanza na kisha apate nafasi ya kung’ara katika igizo na mashabiki wapate kumwona akifanya vitu vyake kwenye luninga.

Mwandika Busati alipata kusikia habari ifananayo na hiyo kwamba hata katika mashindano ya kuwasaka visura rushwa ya ngono imetanda.

Mambo kama hayo kwa hakika yanasikitisha na kutia kichefuchefu. Kwamba kama viongozi wa vikundi fulani vya sanaa wanafikia hatua ya kudai rushwa ya ngono hii ni aibu.

Usanii kwa lugha nyepesi ni karama. Muumba ambaye ni Mola huwajalia baadhi yetu vipaji vya kila aina ukiwamo usanii.

Japo sanaa yahitaji pia elimu ya darasani, ukweli wa mambo ni kwamba mtu huzaliwa na sanaa.

Anachosema Mzee wa Busati ni kwamba kama leo hii watu wanatamba katika sanaa eti kwa sababu tu walitoa hongo ya ngono hawa hawawezi kuitwa wasanii.

Hawa si wasanii hata kidogo. Si wasanii kwa sababu wameingia humo kiufisadi. Wamevaa joho lenye udhalimu ndani yake. Wamelazimisha kuitwa wasanii.

Pengine yafaa waitwe makahaba au malaya ambao kwa jina la sanaa wanafanikiwa kuihadaa jamii.

Mzee wa Busati sasa amefumbua macho na anachokiona ni historia chafu ya viongozi wa vikundi vya sanaa na wasanii wao.

Kama kiongozi anathubutu kutaka mapenzi kwa msanii wa kike ili apewe kipaumbele ni lini basi kaya zetu zitawaona wasanii wa kweli?

Dunia ya aina hii haiwezi kukubalika iendelee kutamba chini ya jua. Hawa hapa si pahala pao. Yafaa waangamizwe ili watoweke.

Haifai kuwa na wasanii ambao historia zao ni mbaya. Haifai kuwa na waigizaji wanaowika kwa sababu walitoa miili yao kama asusa kwa viongozi wao wa sanaa.

Hawa ndio wanaotarajiwa kuwa vinara wa kupinga maovu kwa kutumia vipaji vyao. Hawa ndio dira ya jamii. Kama wanakiuka maadili basi si vema kuwaita wasanii bali wahuni!

Katika hili Mzee wa Busati anawaomba wadau kuungana ili kupiga vita maovu kama hayo. Mambo ya aina hii si ya kuyafumbia macho kwani mwisho wake ni mbaya.

Hawa wanatarajiwa kuwa wahamasishaji wa mambo mbalimbali kama vile vita dhidi ya Ukimwi au ufisadi.

Leo hii msanii atawezaje kupanda jukwaani kuhamasisha vita dhidi ya Ukimwi huku akiwa mkware? Bila shaka atakuwa anacheza muziki asioujua.

Basi na wenye masikio wasikie maneno haya ambayo Mwandika Busati ananena kwa uwazi na ukweli. Wanawali fungeni vibwebwe kupinga mtindo wa kutoa miili yenu kwa ajili ya kuonekana katika televisheni.

Enendeni kila njia mseme kwamba sasa inatosha na si wakati wa kuendelea kunyanyasika kwa jina la sanaa.

Kama baadhi yenu mnadhani haiwezekani kupinga udhalilishwaji huo basi badilisheni fani. Jihalalisheni moja kwa moja kuwa makahaba kwani madanguro yangalipo.

Mzee wa Busati amefikia ukomo kwa juma hili ambalo waumini wa Kristo wanasubiri ufufuo wake.

Kila jema katika Pasaka ila angalieni msije angusha magari kama ilivyo desturi ya Mzee wa Kutibua anayetamba kifedhuli maeneo ya Makumbusho. Msifuate nyayo zake kwani huko ni kujiangamiza.

Wasalaam,

Wednesday, February 20, 2008

Siku ya Valentine inapogeuzwa halimtumwa

Na Innocent Munyuku

SIMULIZI za ujio wa Rais wa Marekani George W. Bush zinaendelea. Mtawala huyo anayesemwa kuwa kinara wa dunia alitua nchini Jumamosi iliyopita kwa ziara ya siku nne ambayo inakoma leo.

Mzee wa Busati naye hakutaka kupitwa na jambo. Kwa nafasi yake alilazimika kujua walau machache yaliyomleta mtawala huyo.

Wengine wakaguswa na mbwembwe za ulinzi wa rais huyo. Hakuona wana wa Darisalama walivyokuwa wakiinua macho yao angani kushuhudia helikopta maalumu ya kinara huyo? Ina kitu na kwa wajuao umombo huiita Marine One!

Mwandika Busati hata hivyo kabla ya ujio wa Bush alikuwa na jambo jingine alilokuwa akisubiri kusemezana na wadau wake. Hilo si jingine bali ni pilika za Februari 14 ambayo huaminika kuwa ni Siku ya Wapendanao kote duniani.

Siku hiyo ni maalumu kwa watu kuonyeshana upendo wa dhati. Marafiki kwa marafiki, mke kwa mume au baba kwa mwana. Kwa ujumla ni siku ya kuonyesha kwamba unamjali mwingine.

Lakini mambo kwa wengi nchini hayakuwa kama ilivyonenwa hapo juu. Mtandao wa Mzee wa Busati umenasa mengi ya aibu siku hiyo.

Wengi wakaigeuza siku hiyo kuwa ni ya kula halimtumwa kwa kiwango cha hali ya juu.

Halimtumwa ni aina ya kiazi kitamu kilicho na rangi ya manjano ndani na kwa kawaida hupendwa sana na walaji kutokana na utamu wake huo.

Hivyo ndivyo walivyoigeuza Februari 14. Wakaifanya siku ya kula halimtumwa. Waking’ara na mavazi yao mekundu na mauaridi mkononi wakaamua kuifanya siku hiyo kuwa ni ya kufanya mapenzi.

Hawakujali kama wako salama au la. Walichoona wao kinafaa ni kula uroda kwa jina la Valentine! Hali hii kwa hakika imemtisha Mwandika Busati kwani kuigeuza siku kama hii kuwa ya kufanya mapenzi ni kuliangamiza taifa.

Nani kawalaani hawa kiasi hiki? Ni nani hasa alihusika na kupiga zumari la kuhamasisha ngono kwa watu hawa?

Lakini haya ndiyo madhara ya kukumbatia kila jambo kutoka ughaibuni. Tukiyaona ya Ulaya au Marekani basi huwa yenye kufyonzwa pasipo kujiuliza kama yanaeleweka.

Kinachomsikitisha Mzee wa Busati ni kwamba miaka inazidi kusonga mbele na hakuna dalili kwamba Wabongo wanaielewa maana halisi ya Februari 14.

Kwa walio wengi hiyo ni siku ya kujificha mahala kwa ajili ya ngono. Tena husikika pahala pengine kuwa wapo walionuna kwa vile wapenzi wao siku hiyo hawakutimizia haja zao za kimwili. Salaale...!

Hii boti ya Februari 14 isipoangaliwa itakimaliza kizazi cha Watanzania ambacho tayari kimefunikwa na maradhi mengine pamoja na umasikini.

Mzee wa Busati akisema ataonekana mwendawazimu lakini heri aseme ili waso mabahau wayachuje na kuyaweka sawia.

Kwamba kwanini basi wasijitokeze wadau na kutoa elimu kwa umma wa Watanzania kuhusu maana halisi ya Februari 14?

Waombe ngwenje kwa wafadhili waandae vijisemina waseme kwa uwazi kwamba siku hiyo si maalumu kwa ajili ya zinaa. Wasiigeuze Februari 14 kuwa kiazi aina ya halimtumwa.

Vinginevyo, miaka michache ijayo Tanganyika hii itajaa makaburi yalotokana na ulimbukeni kwa Februari 14.

Mzee wa Busati anajua fika kwamba kwa msimamo wake huu atakuwa amejijengea uadui na wamiliki wa nyumba za kulala wageni lakini ni heri aseme ili msije mkalaumu kwamba hamkuambiwa.
Mwandika Busati amefika tamati kwa juma hili. Tuombeane uhai ili tukutane tena wiki ijayo tupeane vionjo vingine.
Wasalaam,

Monday, January 14, 2008

Wasanii wamepotea, waliobaki ni kasuku

na innocent munyuku

SIKU zinazidi kukatika hii maana yake ni kwamba mwaka nao unayoyoma. Mambo nayo yanasogea huku ndoto za mwaka mpya kwamba masuala mengi yatakuwa poa zikiendelea kunasa kwenye bongo.

Lakini ukweli ni kwamba hakuna jipya katika maisha zaidi ya kuendelea kusuguana na makali ya bajeti. Mlo wa mmoja kwa siku haiwezi tena kuwa habari mpya.

Kupanda hata daladala iliyofurika hadi kutapita limekuwa jambo la anasa. Wabongo walio wengi sasa hasa waishio katika miji ya kuhitaji mabasi kwenda katika majukumu wamepungua miili.

Wanapungua miili kwani kila uchao wanasaga mguu kwenda katika majukumu yao. Hili ni jambo jema kwa afya ya mwili kwani vitambi vinapungua.

Nani atathubutu kupanda mabasi manne kila siku na nauli yenyewe iko juu? Kwa hiyo wakati mwingine unapunguza bajeti kwa kutembea kwa miguu ili nyumbani nako wauone mlango wa maliwato.

Huo ulikuwa utangulizi wa Mzee wa Busati Jumanne hii ambayo kwake ingali ikimpa hamu ya kuendelea kuwamo katika safina hii ya mwaka 2008.

Si lengo lake kujadili hali ya uchumi kwa Wadanganyika kwani kufanya hivyo kutazidi kumwongezea machungu ya maisha. Hana mbadala. Kujadili pasipo suluhisho ni dhambi.

Leo hii Mzee wa Busati ameona ni vema atete na wadau wa muziki nchini ambao bila shaka mambo mengine yamenasa katika vichwa vyao pasipo kujua kwamba wanapotoka.

Mwandika Busati ni msemakweli pia. Wala hajifichi na wala hawezi kukana kwamba anatumia yale maji yenye rangi ya mende kutoka Ilala.

Huwa anakaa kwenye mikusanyiko ya aina hiyo mara kwamba mara kwa kile kinachoitwa mkao wa majadiliano na wakati mwingine kupoteza mawazo.

Awapo huko mara nyingi huona wanamuziki wakipamba ukumbi kwa maikrofoni zao. Wanaimba kwa mbwembwe kuwapa burudani wateja katika baa husika.

Hakika wanatia faraja kwa nyimbo wanazoibuka nazo kwa siku. Wateja watahamasika na wengine pombe zikifika pahala pake huacha viti vyao na kwenda kuserebuka. Hiyo ni faraja ya moyo.

Lakini kinachomshangaza Mwandika Busati ni kwamba hao wanaoalikwa kutumbuiza wamekuwa kama ndege aitwaye kasuku.

Kama hujui sifa ya kasuku basi ni kwamba huyu ndege ana tabia ya kuiga kusema kama binadamu na mara nyingi hufugwa katika nyumba.

Atajitahidi kuiga kila kisemwacho. Hii ndiyo sifa kuu ya kasuku, ndege mwenye rangi nyingi ambaye ni kipenzi cha binadamu katika makazi yake.

Anachosema Mzee wa Busati kuhusu hizo bendi za muziki zinazotumbuiza katika flani flani ni kwamba wamezidi kuiga nyimbo za wasanii wengine.

Lakini wanatamba wakijiita wao ni wasanii mahiri. Watajiita wanamuziki waliobobea. Huku ni kupotosha ukweli wa mambo. Pengine lugha iko gongana na hivyo kutojua maana halisi ya msanii.

Ajuavyo Mzee wa Busati ni kwamba msanii ni kwamba ni mtu mwenye ustadi wa kuchora, kuchonga au kutia nakshi. Husemwa pia kuwa msanii ni mwenye ufundi wa kutunga na kutoa mawazo yake kama vile kwa ushairi, hadithi au tamthiliya.
Haijasemwa kwamba msanii ni mtu mwenye uwezo wa kuiga iga kama kasuku. Huo si usanii bali ubabaishaji.

Kama kweli mmeamua kuimba si mtunge nyimbo zenu? Ya nini kuendelea kuimba nyimbo za kale? Za kwenu zitasikizwa lini?

Mmebaki na nyimbo za Juma Kilaza na David Kabaka kila siku. Af mkitoka hapo mmeutwika kwa pombe za bure mnatembea kwa matao mkisema kwamba nyie ni wasanii.

Kama kweli mmeamua kushika vipaza sauti kwa jina la muziki basi leteni tungo zenu zisikike ili siku moja nanyi mtambe kwamba mlipata kufyatua albamu iliyovuma.

Si dhambi kuiga nyimbo za kale lakini isiwe kuwahadaa mashabiki kwa onyesho zima. Imbeni nyimbo zenu ili hata mkijisifu muwe na pa kuegemea.

Hivi leo hii Mwandika Busati anawezaje kujiita mwimbaji mahiri eti kwa vile tu kapaza sauti kanisani wakati wa kuimba tenzi za rohoni. Haikubaliki!

Nyimbo za kina Mbaraka Mwishehe zingali zinapendwa hadi kesho. Wengi wanapenda kuzikiza lakini ukweli wa mambo ni kwamba kubaki kuziiga pasipo kutunga mpya ni kupoteza wakati.

Mwandika Busati amefikia kikomo kwa wiki hii. Ataendelea na mengine juma lijalo kwa kasi ile ile pasipo kuogopa tindikali wala mtutu wa bunduki. Panapo ukweli tutaambizana.

Wasalaam,

Sunday, January 6, 2008

Kenya ilikuwa vipande mwaka mmoja kabla ya uchaguzi

MWAKA mmoja kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu nchini Kenya, wanasiasa waliotaka kuwania urais tayari walikuwa wanapigana vikumbo na kuwasha moto mkali wa kisiasa nchini humo. Rais wa sasa, Mwai Kibaki, anayedaiwa kuwa 'amebaka' demokrasia na kulazimisha kubakia Ikulu baada ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Desemba 27 mwaka 2007, alikuwa akilalamikiwa sana wakati huo kwa kushindwa kudhibiti nafasi yake ya urais, na alikuwa anapewa nafasi ndogo ya kushinda.
KILA Mkenya alikuwa anaushangaa utitiri wa watu waliokuwa `wamejitokeza mapema sana kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu ambao ulifanyika Desemba 27 mwaka huu.
Rais Mstaafu wa Kenya, Daniel arap Moi, alikuwa miongoni mwao. "Wanasiasa wanahusika kwa kuigawa nchi ya Kenya vipande vipande kwa kuhubiri ukabila. Wanazungukazunguka huku na kule wakijidai kuwa hiyo ndiyo demokrasia, kumbe wao wanawinda maslahi yao ambayo hayataisaidia nchi.
"Katika chama cha KANU, Mwenyekiti wake Uhuru Kenyatta anapata upinzani kutoka kwa Katibu Mkuu wa chama hicho, William Ruto, ambaye naye pia anataka kugombea urais.
"Chama kilichoiasi KANU, Liberal Demoratic Party (LDP) ambacho kinaongozwa na Raila Odinga kina wawaniaji urais wengi, akiwamo Raila mwenyewe, Kalonzyo Musyoka, Najib Balala na Musalia Mudavadi.
"Rais Mwai Kibaki atagombea kupitia chama cha Narc - Kenya baada ya Umoja uliounda Narc na kuiondoa KANU madarakani kusambaratika.
"Mwenyekiti wa Ford Kenya, Musikari Kombo, ingawa bado yumo ndani ya umoja wa Narc, ambao ndio unatawala nchi, naye ameamua kuwania urais," alisema Moi kwa masikitiko makubwa mwaka mmoja uliopita, na kuongeza:
"Hali hii haitaisaidia Kenya, na hasa ikizingatiwa kwamba wote hawa kila mmoja ana ajenda binafsi iliyojikita katika ukabila ili kufikia malengo yake binafsi. Hali hii itaivunja nchi na kuiacha vipande vipande."
Haya yalikuwa matamshi ya kwanza ya Mzee Moi kuhusu hali ya siasa ya Kenya na mwelekeo wake tangu chama chake cha KANU kilipoondolewa madarakani na Umoja wa Narc uliomweka madarakani Rais Kibaki mwaka 2002.
Moi alikuwa akikwepa sana kutoa mtamshi yoyote kuhusu Serikali ya Kibaki kwa madai kuwa 'Kibaki alikuwa anahitaji muda kuweka misingi mizuri ya utawala.'
Moi hakuwa peke yake katika kuonyesha wasiwasi wa utiriri wa wawaniaji urais. Mwandishi Mashuhuri nchini Kenya, Mutuma Mathiu, katika kuonyesha wasiwasi wake kuhusu hali ya kisiasa alisema:
"Jinsi mambo yanavyokwenda nchini Kenya, kila kiumbe kinachovuta hewa, na hasa wanasiasa, kitaingia katika kinyang'anyiro cha kuwania urais ifikapo Desemba mwaka huu.
"Musikari Kombo, Najib Balala, Raila Odinga, William Ruto na mkururo wa wanasiasa wengine tayari wamekwisha kutamka kuingia kwenye kinyang'anyiro cha kuwania urais.
"Haitashangaza kuwa ifikapo Desemba mwaka 2007, hata wale ambao tayari wamekufa watafufuka kwa kuogopa kuachwa nyuma kwenye kinyang'anyiro hiki.
"Sasa itakapofika hasa wakati wenyewe ndipo kitakuwa kivumbi. Pengine itakuwa zamu ya mbuzi, ng'ombe, mbwa na paka ambao nao wataonyesha nia ya kuchukua nafasi aliyoikalia Rais Kibaki," alisema Mathiu kwa kejeli, na kuongeza:
"Kwa maoni yangu, uwaniaji huu wa urais mwaka mmoja kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu ni dalili za wazi kuwa viongozi wetu ni wabinafsi na wapenda madaraka. Hawawajali wananchi na maendeleo ya Kenya kwa ujumla wake, bali ni waroho, wanaojiangalia wao wenyewe tu. Siasa za Kenya sasa ni pori la vurugu na mkanganyiko wa uongo wa kisiasa."
Ni kweli Kenya ilikuwa tayari imemeguka vipande vipande, vyote vikijikita katika misingi ya ubinafsi na ukabila. Waluo wa Nyanza walikuwa hawasikii chochote, walikuwa wanataka kumsikia Raila Odinga tu, basi. Waluhya magharibi mwa Kenya walikuwa wanamwangalia mtu wao Musalia Mudavadi, japo kulikuwa na Mluhya mwingine, Musikari Kombo, wa chama cha Ford Kenya. Wakikuyu, kabila kubwa kabisa anakotoka Rais Kibaki, hao ndio kabisa damu yao inanuka Ukikuyu tu, na hii inajionyesha wazi wazi; na kabila hili linaamini kuwa ndilo lenye haki ya kuitawala Kenya kisiasa na kiuchumi.
Waluo na Waluhya ni majirani, na hawajawahi kuungana kwa nia ya kupeleka urais magharibi mwa Kenya. Kwa zaidi ya miaka 44 iliyopita, Waluo na Waluhya wamekuwa na sauti kubwa katika kuamua nani awe mpangaji wa Ikulu - ama kwa uamuzi wa moja kwa mja au wa chini chini.
Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2002, Waluo na Waluhya waliupigia umoja wa Narc kura na kumwezesha Kibaki kunyakua madaraka. Baada ya kuingia madarakani, Kibaki alimteua Mluhya, Kijana Wamalwa (sasa ni marehemu), kuwa Makamu wa Rais, na kumwacha pembeni Raila Odinga. Hii ilikuwa kinyume cha makubaliano ya awali kati yake (Kibaki) na Raila kwamba nafasi hiyo ingekuwa ya Raila hasa baada ya kumsaidia sana Kibaki kuukwaa urais.
Baada ya kifo cha Wamalwa, Kibaki alimteua Mluhya tena, Moody Awori, kushika nafasi ya Makamu wa Rais, hatua ambayo iliendelea kumuudhi sana Raila.
Kuna uvumi kuwa Mudavadi na Raila walijaribu kutafuta fomula ya kuunganisha makabila haya mawili (Waluo na Waluhya) ili kujihakikishia kura nyingi katika Uchaguzi Mkuu uliomalizika wiki iliyopita.
Hatua hii ilikuwa na nia ya kufifisha nguvu za kabila kubwa la Wakikuyu linalokaa katikati mwa Kenya, na watu wa Bonde la Ufa (Rift Valley) ambako Mzee Moi alikuwa anadaiwa kuwa na ushawishi mkubwa.
Raila, Mudavadi na Musyoka anayetoka katika kabila la Wakamba, wakiungwa mkono na watu wa pwani mwa Kenya ambako anatoka Balala walimshinda Rais Kibaki Novemba 21, 2005 kwa kutumia mwavuli wa Orange Democratic Movement (ODM) wakati wa kura za maoni ambako Rais Kibaki alitaka kubadili Katiba. Huu ulikuwa mchuano kati ya Chungwa na Ndizi ambao ulimwacha Rais Kibaki njia panda kisiasa.
Kwa upande mwingine, Rais Mstaafu Moi alikuwa anapenda safari hii Uhuru Kenyatta ashinde urais baada ya juhudi zake kupitia kilichoitwa Mradi wa Uhuru (Uhuru Project) kushindwa vibaya mwaka 2002, na kuufanya Umoja wa Narc kunyakua madaraka, hali iliyosababisha chama chake cha KANU kuwa chama cha upinzani kwa mara ya kwanza tangu Kenya ipate Uhuru Desemba mwaka 1963.
Lakini kwa hali ya kisiasa ilivyokuwa, hii isingewezekana. Maji yalikuwa marefu sana kwa Mzee Moi. Ni kweli wakati huo alikuwa na ushawishi mkubwa kisiasa nyumbani kwake katika Bonde la Ufa ambao sasa unafifia kwa kasi. Hivyo asingeweza kumuuza Uhuru Kenyatta kwa Waluhya, Waluo, Wakamba (anakotoka Musyoka) na sehemu za pwani mwa Kenya.
Uhuru ni Mkikuyu, na makabila mengine nchini Kenya hayawaamini kabisa Wakikuyu kwa sababu ya kuhodhi siasa na biashara za nchi hiyo kupitia migongo ya makabila mengine. Watu wa pwani wanakwenda mbali zaidi kwa kusema kuwa "heri kula na Mluo kuliko kula au kuwa karibu na Mkikuyu".
Tetesi zilizokuwa zinavuma wakati huo mingoni mwa makabila yanayoishi katika majimbo ya uchaguzi pwani mwa Kenya zilikuwa zinasema kuwa miongoni mwa watu waliojitokeza kugombea urais, Musyoka ndiye wangependa awe Rais, na Raila awe Waziri Mkuu baada ya Katiba kubadilishwa.
Watu wa pwani hawakuwa peke yao kwa hili. Walikuwapo baadhi ya Wakenya sehemu nyingine za nchi ambao walipenda kuona hali inakuwa hivyo baada ya Uchaguzi Mkuu ili kumfanya Raila asiendelee kutingisha nchi kisiasa.
Katika makubaliano na Kibaki kabla Raila hajajiunga na Umoja wa Narc, kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2002, Raila alipaswa awe Waziri Mkuu kama ilivyodokezwa hapo juu.
Baada ya Rais Kibaki kuingia Ikulu, alimpiga teke Raila baada ya washauri wa karibu sana wa Kibaki, hasa kutoka katika kabila lake, kufanikiwa kumshawishi kufanya hivyo. Inasemekana kuwa ni watu hawa hawa waliomshawishi na kumshinikiza agombee tena urais safari hii kwa madai kuwa 'nchi haiwezi kuchukuliwa na Mluo.'
Tangu Rais Kibaki amweke pembeni, Raila ameupa taabu sana uongozi wake hadi majuzi Uchaguzi Mkuu ulipofanyika. Amekuwa mwiba mkali kwake, na ni mtu anayeogopwa sana na Kibaki mwenyewe na wengi wa mawaziri wake.
Kwa bahati mbaya sana kitu kimoja ni dhahiri nchini Kenya, nacho ni kwamba siasa zimejikita kwenye ukabila kwa kiwango cha kutisha. Wanasiasa wengi wanahubiri demokrasia na nia ya kuwakwamua wanyonge wa Kenya kutokana na lindi la umasikini, lakini moyoni wamesheheni ukabila na ajenda binafsi za kuwanufaisha wao na watu wa karibu yao.
Mbali na ukabila, jambo ambalo Wakenya wengi linawakera ni jinsi Rais Kibaki alivyoshindwa kudhibiti nafasi yake ya urais kabla ya Uchaguzi Mkuu wa juzi, kushindwa kuwadhibiti mawaziri na maofisa wake waandamizi kiasi kwamba wanafanya mambo jinsi wanavyoona, ukiwamo ufisadi; na mke wake, Lucy Kibaki, kuingilia masuala ya Serikali wakati yeye si sehemu ya Baraza la Mawaziri.
Wakenya wengi hawawaamini wanasiasa wakati huu ambako ufisadi unaongezeka, na Serikali kuonyesha kushindwa kufanya chochote cha maana kuzuia baa hili.
Wananchi wengi jijini Nairobi na mjini Kisumu mwaka mmoja uliopita walikuwa wanasema wazi kuwa Rais Kibaki akiamua kusimama kugombea tena urais atajiaibisha mwenyewe, na hasa baada ya 'kuvurunda' sana tangu achaguliwe kuwa Rais, na kwamba ishara za nyakati hazipo upande wake, yaani tayari zimekwisha kumpa kisogo.
Walisema kuwa hii itakuwa mbaya zaidi kama atasimama kupambana na Raila Odinga ambaye ana nguvu na ushawishi mkubwa kisiasa. Walisema kuwa ikiwa itatokea hivyo, mambo mawili yangetokea; ama Kibaki angelazimika kukubali kushindwa na kuondoka Ikulu au kutumia vyombo vya dola kuiba kura ili aonekane ameshinda, kitu ambacho kingeitikisa nchi.
Na kweli imetokea hivyo. Nchi si tu imetikisika, bali pia imewaka moto. Ni kama moto wa nyika wakati wa kiangazi. Masikini Kenya!

Twende wapi tukausikilize muziki wa Tanzania?

na innocent munyuku

JUMA moja limeshapita tangu mwaka mpya wa 2008 uanze. Salamu zingali zikimiminika kila mmoja kwa dua yake anaomba mema kwake na jirani yake. Ni dua mtindo mmoja.

Meseji zimejaa kwenye simu za viganjani. Maneno matamu yanapendezesha nafsi ingawa ukweli wa mambo ni kwamba si kila liombwalo huja kama atakavyo mwombaji.

Dunia ndivyo ilivyo. Nyakati kama hizi hata aliyekuwa akikusengenya atapumzika kwa muda kwani anayo furaha ya kuuona mwaka mpya.

Mzee wa Busati naye yu kundini akiwaza na kuwazua. Ameshatafakari mengi ya mwaka uliopita. Mwaka ulikuwa umejaa zege mgongoni. Mizigo ilikuwa mizito.

Utafanyaje katika hilo? Utakimbia familia? La hasha! Ni mapambano kwa kwenda mbele hata ikibidi kuwa mpambe wa mwenye ngwenje ni jambo jema.

Mbona kina Momburi ndivyo wanavyoishi? Wakiwa na haja ya bia za bure wanajua pa kukimbilia. Watapiga mguu hadi Mwana Mkude. Huko watakula matumbo na vichwa vya kuku wakishashibisha minyoo tumboni watashushia na safari lager mbili zilizoongezewa viroba vya konyagi.

Hapo mwanawane muziki unakuwa mkubwa kichwani. Watachanganya Kimombo na Kichaga juu. Basi utamu huo hauna maelezo ni kama vile wako peponi.

Enewei tuachane na hilo kwani alilojia Mzee wa Busati wiki hii ni hili la sanaa na utamaduni wa M-bongo. Ni ngumu kidogo kusema kwa uwazi kabisa kwamba ni wapi hasa utakumbana na sanaa ya Tanzania hasa katika muziki.

Pengine Mwandika Busati ataonekana mtata katika hili lakini ukweli ni kwamba leo hii ukisikia matamasha ya muziki basi usikae ukadhani kuwa huko utakuta mdumange au mganda.

Wala usisumbuke ukatoka mbio kuwahi tamasha hilo kwa ndoto ya kukuta Ingoma au Sindimba. Huko utakuta magoma kutoka ng’ambo. Vijana wakipishana kwa vikumbo kughani mashairi ya kina Tupac au Britney Spears.

Wataimba kama waimbavyo Waingereza na Wamarekani. Hakuna anayethubutu kufuata nyayo za Fela Kuti na Afrobeat zake. Wamesahau kabisa kuwaenzi wasanii wa bara la Afrika.

Hakuna tena ile shauku ya kuusambaza muziki wa Afrika. Kilichobaki sasa ni kujivunia mengine yanayovuma nchi za Kimagharibi. Watavaa kama Wamarekani na hata sema yao katika ndimi zao ni lafudhi za huko huko.

Huwezi tena kumtofautisha Ambwene na Cooper. Si rahisi tena kumtambua Achimwene na Smith. Ni ngumu pia kumtofautisha Shemakame na Erickson. Wote wanafanana kwa tabia, mavazi na mengineyo.

Ukiwaambia kuwa huko waendako siko wanakuja juu na kukuona u mjinga, mwingi wa tongotongo na usiyejua lolote katika dunia hii. Watakueleza kwa tambo pasipo hofu kwamba wao wanakwenda na wakati na huu ndio wakati.

Lakini je, hivi kweli huko ni kwenda na wakati au ni kukosa mkakati? Usingizi gani huu usiokuwa na tamati? Akili zimedumaa hata akawapiku nyati?

Hata simba mwituni wanazo kanuni hali kadhalika kunguni na nyuni. Iweje mwana wa adamu akose msimamo akashindwa kutambua kuwa kuendelea kukumbatia ya Magharibi ni hila kwa sanaa ya Afrika?

Mzee wa Busati kama hakosei huu ni mwaka wa nane tangu atambe na safu hii katika magazeti mbalimbali ya Kibongo na katika siku zote hizo amekuwa akipayuka juu ya uovu wa wasanii wengi nchini kuidharau sanaa ya Tanzania.

Walio wengi wanadhani kukaa na kujifunza kupiga ngoma ni ushamba na hapaswi kuitwa msanii. Wanadhani kuimba nyimbo za asili yao ni kujidhalilisha. Hawa wamezingirwa na utumwa wa akili.

Wamefugwa kwenye zizi la ujinga wa kujitakia. Hawaoni tena kama nyimbo za asili zina nguvu ya kuutambulisha utamaduni wa Mtanzania. Wamebaki kuchungulia runinga na kuiga wayaonayo kwenye vioo hivyo.

Bila shaka watasema huko ndiko liliko soko kubwa la muziki lakini je, kuna maana gani ya kuimba nyimbo zenye maisha kama karatasi ya chooni? Zitavuma leo, kesho kwisha habari.

Huo ni mtazamo tu wa Mwandika Busati. Mwenye kuwaza vinginevyo yu huru kuleta yake yapate kujadiliwa bila ncha ya upanga.

Ndoto ya Mzee wa Busati ni kwamba ifike siku M-bongo afike Ottawa kwa ziara ya kutambulisha nyimbo za Tanzania. Ifike siku Mtanganyika azuru New York au London akitangaza mema ya kwetu kupitia santuri zake.

Pamoja na ukweli kwamba wapo waliowahi kufanya hilo, bado kuna ufinyu wa wasanii kujitutumua na kufikia hatua hiyo. Walio wengi wanaimba ili wapate kula leo.

Kutokana na hilo ndiyo maana wamebaki kuiga badala ya kubuni. Amkeni msilale kama pono. Badilikeni ili wadau wapate pahala pa kuusikiliza muziki wa Tanzania.

Huu ni ukomo wa Mzee wa Busati wiki hii. Anatulia na kujipinda kwa ajili ya mambo mengine ya kujenga nchi. Lakini hajaacha kuomba mema kwa ajili ya Wakenya wanaopukutika sasa huku mzee mzima Kibaki akipunga upepo kwenye kasri lake jijini Nairobi ingawa wengine wanaliita jiji hilo kuwa ni New Robbery.

Wasalaam,

Wednesday, January 2, 2008

Manabii wa soka mpeni pumzi Maximo

na innocent munyuku

HERI ya Krismasi na fanaka ya mwaka mpya wa 2008. Mzee wa Busati anaimba Haleluya akila vipapatio vya kuku kwa pumzi yenye rutuba ambayo Mola amemjalia.

Yamekuja mengi mabaya na mazuri lakini kwa sasa neema imefika mlangoni. Kaya yake inadunda kwa mema. Hakuna matata.

Wiki hii Mwandika Busati kama ilivyo ada anakuja na porojo zake lakini zilizojaa udadisi na changamoto kwenye bongo za Wadanganyika.

Wiki hii Mwandika Busati ameamua kuwa tofauti na fikra za Wabongo walio wengi hasa kwa wapenda soka nchini.

Linalosemwa na Mzee wa Busati ni hali ya timu ya taifa ya Tanzania Bara ambayo wiki msimu huu kwa mara nyingine imeshindwa kubeba Kombe la Chalenji.

Kocha Mkuu wa timu hiyo Marcio Maximo kwa sasa bila shaka hawezi kutembea mitaa ya Kariakoo kama ilivyokuwa miezi sita nyuma.

Hawezi kutembea kwa matao kwa sababu watu wamefura. Wanachosema ni kwamba Maximo hawezi tena kuwa kocha wa timu hiyo. Kisa? Timu yao imefanya vibaya kwenye michuano hiyo.

Walitamani kombe libaki nyumbani na bila shaka hiyo ingekuwa zawadi mwafaka kwa Noeli na Mwaka Mpya. Lakini ndoto hiyo imekuwa chungu.

Kinachosemwa kwenye vijiwe sasa ni kwamba Maximo kashindwa kazi na kilichobaki afungashe aende zake Brazil.

Lakini Mzee wa Busati angependa hoja ya kumbeza Maximo sasa iwekwe kando kwa sababu ukweli wa mambo ni kwamba bado Tanzania haijasukwa vema katika soka.

Wakati fulani Mwandika Busati alipata kusema kuwa wanaopiga kelele kwamba Maximo hafai bila shaka ni wendawazimu kutokana na historia ya soka nchini.

Maximo kutoka Brazil ambako wanavuma katika soka haina maana kwamba angeweza kuibadilisha soka ya bongo kwa siku moja. Angali anahitaji muda.

Leo hii mwapiga kelele kwamba hafai, waliokuwapo kabla ya Maximo walitenda nini jema katika soka ya Tanzania? Si waliishia kupiga soga na kulumbana kila kukicha?

Mwasema ati Maximo hashauriki. Nani aliwahi kumshauri naye akagoma kufuata kilichosemwa?

Mwanena pia kwamba ati mlijua Maximo hana lolote. Huu ni unabii ambao kimsingi hauna tija katika maslahi ya soka nchini. Aliwakuta wachezaji wameshakauka hata akijaribu kuwakunja wanameguka. Huo ndio ukweli wa mambo.

Mwacheni apange timu awezavyo. Kumrushia madongo ya lawama ni kutomtendea haki kwani wengi wenu bila shaka mwaelewa matatizo ya huko nyuma.

Mzee wa Busati kwa kawaida hafichi kuweka wazi misimamo yake. Hata kama anaona kufanya hivyo kunaweza kumtenga na masahiba zake hilo kwake halimpi shida.

Maximo si wa kulaumiwa. Jiulizeni tuliteleza wapi na Maximo anajaribu kufanya nini.

Kama Mwandika Busati haendi mbali na ukweli ni kwamba anachofanya Maximo kwa sasa ni kutengeneza pepo ya soka kwa miaka ijayo.

Mnaodhani leo hii mtabeba Kombe la Dunia ni kupoteza wakati kwani hilo kimsingi haliwezakani. Acheni porojo mwacheni Maximo na programu yake.

Vinginevyo Mzee wa Busati anawapa uhondo wa shairi ambalo katumiwa na sahiba yake anayekwenda kwa jina la Mwafrika Merinyo. Kila la heri!

Sikukuu ziwe na raha
Zisijewepo karaha
Sote tuombe furaha
Na ucheshi na mizaha
Tule tunywe kwa staha
Ituwakie ya jaha!

Tumuombe na Karima
Tujalie yalo mema
Mwaka uishe salama
Heri isije tuhama
Tuondolee zahama
Riziki zisije zama!

Tufanyiane mazuri
Ya baraka na ya heri
Tujiepushie shari
Na fahari na kiburi
Tuzisafishe saduri
Mabaya tusihiyari!

Upendo kita mizizi
Heshima ikaze uzi
Vita tupige uozi
Tusije lia machozi
Ukweli nao uwazi
Ziwe ndo zetu hirizi!

Sinza kwetu karibuni
Mwaka huu na mwakani
Mavazi furahieni
Myavae maungoni
Kwa maarufu washoni
Msisahau jamani!!!!!!!!!!!

Wasalaam,

Mwalilia paradiso pasipo mauti?

na innocent munyuku

HERI ya mwaka mpya! Mzee wa Busati anawasabahi kwa furaha ya kuuona mwaka huu wa 2008. Yalopita si ndwele tugange yajayo.

Yawezakana mwaka uliomalizika jana ulijaa maumivu kwa wadau lakini hilo lisiwavunje moyo. Kazeni buti ili mambo yanyooke msimu huu.

Wiki hii pamoja na kuwa na furaha ya kuuona mwaka mpya, Mzee wa Busati anakenua meno baada ya kubaini kuwa katika kaya kumejaa mabahau na malimbukeni.

Hao hawataki kuguswa. Wakiguswa basi hufura kama moto wa volcano. Watapaza sauti zao kwa hasira na maneno machafu yawatoke kama vile hawakunyonya maziwa ya mama zao.

Juma lililopita Mzee wa Busati alitua kwenye safu yake akielezea umuhimu wa kumwacha huru Kocha Mkuu wa Taifa Stars Marcio Maximo.

Alichonena Mwandika Busati ni kwamba Maximo ambaye pia ni kocha wa Kilimanjaro Stars asiadhibiwe au kutupiwe lawama kupita kiasi.

Leo hii Maximo kwa wengine anaonekana adui mkubwa wa soka Tanzania. hawataki kumsikia wala kumwona usoni. Wanasema anaua soka Bongo.

Kimsingi alichokuwa anasema Mzee wa Busati ni kwamba kumtupia lawama kocha huyo ni jambo jema kama watupa lawama watakuwa na hoja mbadala.

Kwa bahati mbaya, hao wanaojiita wadau wa soka wakarusha makombora mazito kwa Mzee wa Busati. Wakatukana walivyoweza. Hapa akageuzwa Simon wa Kirene aliyemsaidia Yesu kubeba msalaba.

Wakasema hawana haja ya kuwa na Maximo eti kwa sababu analipwa mamilioni na hakuna analolifanya. Ameshindwa kazi! Hiyo ikawa kauli yao ya uhitimisho.

Wakaongeza kuwa kuna makocha wazawa ambao wakilipwa kama Maximo basi mambo yatakwenda sawia dimbani.

Lakini ukweli wa mambo ni bado kuna mengi ya kufanywa zaidi ya kulipwa vizuri katika kibarua cha ukocha. Lililo kuu ni maandalizi.

Juzi Mzee wa Busati kasikia mpango wa kujenga taasisi ya kukuza vipaji kwa vijana wenye umri usiozidi miaka 17.

Hayo ndiyo mambo ambayo yalipaswa kufanywa kabla hata Maximo hajaja. Yangeanza miaka tele nyuma leo hii tusingekuwa tunalaumu makocha gizani pasipo mbadala.

Leo kungekuwa na furaha kila kona kwani wachezaji waliopikwa wangekuwa tele na vipaji vyao viking’ara kimataifa.

Kelele hizi kwamba Maximo hafai wakati mwingine ni ufinyu wa fikra. Hao wanaopayuka leo hii hawana tofauti na wale wanaotamani kufika paradiso huku wakikataa kuonja mauti.

Miaka tele soka ya bongo ilitegemea tunguli na misimamo mibovu ya viongozi wa klabu na mamlaka zingine za soka.

Bila watu kulala makaburini timu isingeingizwa uwanjani. Bila mbuzi kuchinjwa na damu kupakwa wachezaji hakuna kutinga dimbani. Haya mambo si siri yamefanyika sana.

Hebu tusemezane kwa hoja. Hao makocha wazawa waliokuwapo kabla ya Maximo wamefanya jipya gani zaidi ya kukumbatia malumbano?

Mambo ya ulozi yamekuwa yakionekana kwa uwazi kabisa na ndio maana hivi karibuni Mkurugenzi wa Maendeleo ya Soka wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), Ashford Mamelodi alizitaka klabu kuachana na ndumba.

Mamelodi alitoa kauli hiyo wakati akifunga semina elekezi kwa timu za Ligi Kuu Tanzania Bara mjini Bagamoyo.

La maana linalopaswa kufanywa ni kuhakikisha kuwa kila anayejiita mdau na mkereketwa wa soka atambue majukumu ya kuendeleza soka kwa uongozi na ufundi.

Turejee kwa Maximo. Kocha huyo raia wa Brazil ametua nchini katika muda ambao Tanzania ilikuwa katika mlolongo wa migogoro katika klabu za soka.

Kwa bahati mbaya sana migogoro hiyo ingali ikiendelea kuzitafuna klabu. Klabu ambazo Maximo anastahili kubeba wachezaji kwa ajili ya timu ya taifa.

Hebu basi tuangalie mizizi ya soka yetu kabla ya kumtupia mawe Maximo. Bila shaka msimamo wake wafaa uheshimiwe, asipigiwe miluzi mingi. Huo ndio mtazamo wa Mzee wa Busati.

Vinginevyo Mwandika Busati anaomba mema yatue mwaka huu kwa wadau wake. Endeleeni kupanga yenye tija na kila mmoja awajibike kwa nafasi yake.

Wasalaam,