Sunday, January 6, 2008

Kenya ilikuwa vipande mwaka mmoja kabla ya uchaguzi

MWAKA mmoja kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu nchini Kenya, wanasiasa waliotaka kuwania urais tayari walikuwa wanapigana vikumbo na kuwasha moto mkali wa kisiasa nchini humo. Rais wa sasa, Mwai Kibaki, anayedaiwa kuwa 'amebaka' demokrasia na kulazimisha kubakia Ikulu baada ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Desemba 27 mwaka 2007, alikuwa akilalamikiwa sana wakati huo kwa kushindwa kudhibiti nafasi yake ya urais, na alikuwa anapewa nafasi ndogo ya kushinda.
KILA Mkenya alikuwa anaushangaa utitiri wa watu waliokuwa `wamejitokeza mapema sana kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu ambao ulifanyika Desemba 27 mwaka huu.
Rais Mstaafu wa Kenya, Daniel arap Moi, alikuwa miongoni mwao. "Wanasiasa wanahusika kwa kuigawa nchi ya Kenya vipande vipande kwa kuhubiri ukabila. Wanazungukazunguka huku na kule wakijidai kuwa hiyo ndiyo demokrasia, kumbe wao wanawinda maslahi yao ambayo hayataisaidia nchi.
"Katika chama cha KANU, Mwenyekiti wake Uhuru Kenyatta anapata upinzani kutoka kwa Katibu Mkuu wa chama hicho, William Ruto, ambaye naye pia anataka kugombea urais.
"Chama kilichoiasi KANU, Liberal Demoratic Party (LDP) ambacho kinaongozwa na Raila Odinga kina wawaniaji urais wengi, akiwamo Raila mwenyewe, Kalonzyo Musyoka, Najib Balala na Musalia Mudavadi.
"Rais Mwai Kibaki atagombea kupitia chama cha Narc - Kenya baada ya Umoja uliounda Narc na kuiondoa KANU madarakani kusambaratika.
"Mwenyekiti wa Ford Kenya, Musikari Kombo, ingawa bado yumo ndani ya umoja wa Narc, ambao ndio unatawala nchi, naye ameamua kuwania urais," alisema Moi kwa masikitiko makubwa mwaka mmoja uliopita, na kuongeza:
"Hali hii haitaisaidia Kenya, na hasa ikizingatiwa kwamba wote hawa kila mmoja ana ajenda binafsi iliyojikita katika ukabila ili kufikia malengo yake binafsi. Hali hii itaivunja nchi na kuiacha vipande vipande."
Haya yalikuwa matamshi ya kwanza ya Mzee Moi kuhusu hali ya siasa ya Kenya na mwelekeo wake tangu chama chake cha KANU kilipoondolewa madarakani na Umoja wa Narc uliomweka madarakani Rais Kibaki mwaka 2002.
Moi alikuwa akikwepa sana kutoa mtamshi yoyote kuhusu Serikali ya Kibaki kwa madai kuwa 'Kibaki alikuwa anahitaji muda kuweka misingi mizuri ya utawala.'
Moi hakuwa peke yake katika kuonyesha wasiwasi wa utiriri wa wawaniaji urais. Mwandishi Mashuhuri nchini Kenya, Mutuma Mathiu, katika kuonyesha wasiwasi wake kuhusu hali ya kisiasa alisema:
"Jinsi mambo yanavyokwenda nchini Kenya, kila kiumbe kinachovuta hewa, na hasa wanasiasa, kitaingia katika kinyang'anyiro cha kuwania urais ifikapo Desemba mwaka huu.
"Musikari Kombo, Najib Balala, Raila Odinga, William Ruto na mkururo wa wanasiasa wengine tayari wamekwisha kutamka kuingia kwenye kinyang'anyiro cha kuwania urais.
"Haitashangaza kuwa ifikapo Desemba mwaka 2007, hata wale ambao tayari wamekufa watafufuka kwa kuogopa kuachwa nyuma kwenye kinyang'anyiro hiki.
"Sasa itakapofika hasa wakati wenyewe ndipo kitakuwa kivumbi. Pengine itakuwa zamu ya mbuzi, ng'ombe, mbwa na paka ambao nao wataonyesha nia ya kuchukua nafasi aliyoikalia Rais Kibaki," alisema Mathiu kwa kejeli, na kuongeza:
"Kwa maoni yangu, uwaniaji huu wa urais mwaka mmoja kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu ni dalili za wazi kuwa viongozi wetu ni wabinafsi na wapenda madaraka. Hawawajali wananchi na maendeleo ya Kenya kwa ujumla wake, bali ni waroho, wanaojiangalia wao wenyewe tu. Siasa za Kenya sasa ni pori la vurugu na mkanganyiko wa uongo wa kisiasa."
Ni kweli Kenya ilikuwa tayari imemeguka vipande vipande, vyote vikijikita katika misingi ya ubinafsi na ukabila. Waluo wa Nyanza walikuwa hawasikii chochote, walikuwa wanataka kumsikia Raila Odinga tu, basi. Waluhya magharibi mwa Kenya walikuwa wanamwangalia mtu wao Musalia Mudavadi, japo kulikuwa na Mluhya mwingine, Musikari Kombo, wa chama cha Ford Kenya. Wakikuyu, kabila kubwa kabisa anakotoka Rais Kibaki, hao ndio kabisa damu yao inanuka Ukikuyu tu, na hii inajionyesha wazi wazi; na kabila hili linaamini kuwa ndilo lenye haki ya kuitawala Kenya kisiasa na kiuchumi.
Waluo na Waluhya ni majirani, na hawajawahi kuungana kwa nia ya kupeleka urais magharibi mwa Kenya. Kwa zaidi ya miaka 44 iliyopita, Waluo na Waluhya wamekuwa na sauti kubwa katika kuamua nani awe mpangaji wa Ikulu - ama kwa uamuzi wa moja kwa mja au wa chini chini.
Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2002, Waluo na Waluhya waliupigia umoja wa Narc kura na kumwezesha Kibaki kunyakua madaraka. Baada ya kuingia madarakani, Kibaki alimteua Mluhya, Kijana Wamalwa (sasa ni marehemu), kuwa Makamu wa Rais, na kumwacha pembeni Raila Odinga. Hii ilikuwa kinyume cha makubaliano ya awali kati yake (Kibaki) na Raila kwamba nafasi hiyo ingekuwa ya Raila hasa baada ya kumsaidia sana Kibaki kuukwaa urais.
Baada ya kifo cha Wamalwa, Kibaki alimteua Mluhya tena, Moody Awori, kushika nafasi ya Makamu wa Rais, hatua ambayo iliendelea kumuudhi sana Raila.
Kuna uvumi kuwa Mudavadi na Raila walijaribu kutafuta fomula ya kuunganisha makabila haya mawili (Waluo na Waluhya) ili kujihakikishia kura nyingi katika Uchaguzi Mkuu uliomalizika wiki iliyopita.
Hatua hii ilikuwa na nia ya kufifisha nguvu za kabila kubwa la Wakikuyu linalokaa katikati mwa Kenya, na watu wa Bonde la Ufa (Rift Valley) ambako Mzee Moi alikuwa anadaiwa kuwa na ushawishi mkubwa.
Raila, Mudavadi na Musyoka anayetoka katika kabila la Wakamba, wakiungwa mkono na watu wa pwani mwa Kenya ambako anatoka Balala walimshinda Rais Kibaki Novemba 21, 2005 kwa kutumia mwavuli wa Orange Democratic Movement (ODM) wakati wa kura za maoni ambako Rais Kibaki alitaka kubadili Katiba. Huu ulikuwa mchuano kati ya Chungwa na Ndizi ambao ulimwacha Rais Kibaki njia panda kisiasa.
Kwa upande mwingine, Rais Mstaafu Moi alikuwa anapenda safari hii Uhuru Kenyatta ashinde urais baada ya juhudi zake kupitia kilichoitwa Mradi wa Uhuru (Uhuru Project) kushindwa vibaya mwaka 2002, na kuufanya Umoja wa Narc kunyakua madaraka, hali iliyosababisha chama chake cha KANU kuwa chama cha upinzani kwa mara ya kwanza tangu Kenya ipate Uhuru Desemba mwaka 1963.
Lakini kwa hali ya kisiasa ilivyokuwa, hii isingewezekana. Maji yalikuwa marefu sana kwa Mzee Moi. Ni kweli wakati huo alikuwa na ushawishi mkubwa kisiasa nyumbani kwake katika Bonde la Ufa ambao sasa unafifia kwa kasi. Hivyo asingeweza kumuuza Uhuru Kenyatta kwa Waluhya, Waluo, Wakamba (anakotoka Musyoka) na sehemu za pwani mwa Kenya.
Uhuru ni Mkikuyu, na makabila mengine nchini Kenya hayawaamini kabisa Wakikuyu kwa sababu ya kuhodhi siasa na biashara za nchi hiyo kupitia migongo ya makabila mengine. Watu wa pwani wanakwenda mbali zaidi kwa kusema kuwa "heri kula na Mluo kuliko kula au kuwa karibu na Mkikuyu".
Tetesi zilizokuwa zinavuma wakati huo mingoni mwa makabila yanayoishi katika majimbo ya uchaguzi pwani mwa Kenya zilikuwa zinasema kuwa miongoni mwa watu waliojitokeza kugombea urais, Musyoka ndiye wangependa awe Rais, na Raila awe Waziri Mkuu baada ya Katiba kubadilishwa.
Watu wa pwani hawakuwa peke yao kwa hili. Walikuwapo baadhi ya Wakenya sehemu nyingine za nchi ambao walipenda kuona hali inakuwa hivyo baada ya Uchaguzi Mkuu ili kumfanya Raila asiendelee kutingisha nchi kisiasa.
Katika makubaliano na Kibaki kabla Raila hajajiunga na Umoja wa Narc, kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2002, Raila alipaswa awe Waziri Mkuu kama ilivyodokezwa hapo juu.
Baada ya Rais Kibaki kuingia Ikulu, alimpiga teke Raila baada ya washauri wa karibu sana wa Kibaki, hasa kutoka katika kabila lake, kufanikiwa kumshawishi kufanya hivyo. Inasemekana kuwa ni watu hawa hawa waliomshawishi na kumshinikiza agombee tena urais safari hii kwa madai kuwa 'nchi haiwezi kuchukuliwa na Mluo.'
Tangu Rais Kibaki amweke pembeni, Raila ameupa taabu sana uongozi wake hadi majuzi Uchaguzi Mkuu ulipofanyika. Amekuwa mwiba mkali kwake, na ni mtu anayeogopwa sana na Kibaki mwenyewe na wengi wa mawaziri wake.
Kwa bahati mbaya sana kitu kimoja ni dhahiri nchini Kenya, nacho ni kwamba siasa zimejikita kwenye ukabila kwa kiwango cha kutisha. Wanasiasa wengi wanahubiri demokrasia na nia ya kuwakwamua wanyonge wa Kenya kutokana na lindi la umasikini, lakini moyoni wamesheheni ukabila na ajenda binafsi za kuwanufaisha wao na watu wa karibu yao.
Mbali na ukabila, jambo ambalo Wakenya wengi linawakera ni jinsi Rais Kibaki alivyoshindwa kudhibiti nafasi yake ya urais kabla ya Uchaguzi Mkuu wa juzi, kushindwa kuwadhibiti mawaziri na maofisa wake waandamizi kiasi kwamba wanafanya mambo jinsi wanavyoona, ukiwamo ufisadi; na mke wake, Lucy Kibaki, kuingilia masuala ya Serikali wakati yeye si sehemu ya Baraza la Mawaziri.
Wakenya wengi hawawaamini wanasiasa wakati huu ambako ufisadi unaongezeka, na Serikali kuonyesha kushindwa kufanya chochote cha maana kuzuia baa hili.
Wananchi wengi jijini Nairobi na mjini Kisumu mwaka mmoja uliopita walikuwa wanasema wazi kuwa Rais Kibaki akiamua kusimama kugombea tena urais atajiaibisha mwenyewe, na hasa baada ya 'kuvurunda' sana tangu achaguliwe kuwa Rais, na kwamba ishara za nyakati hazipo upande wake, yaani tayari zimekwisha kumpa kisogo.
Walisema kuwa hii itakuwa mbaya zaidi kama atasimama kupambana na Raila Odinga ambaye ana nguvu na ushawishi mkubwa kisiasa. Walisema kuwa ikiwa itatokea hivyo, mambo mawili yangetokea; ama Kibaki angelazimika kukubali kushindwa na kuondoka Ikulu au kutumia vyombo vya dola kuiba kura ili aonekane ameshinda, kitu ambacho kingeitikisa nchi.
Na kweli imetokea hivyo. Nchi si tu imetikisika, bali pia imewaka moto. Ni kama moto wa nyika wakati wa kiangazi. Masikini Kenya!

No comments: