Monday, January 14, 2008

Wasanii wamepotea, waliobaki ni kasuku

na innocent munyuku

SIKU zinazidi kukatika hii maana yake ni kwamba mwaka nao unayoyoma. Mambo nayo yanasogea huku ndoto za mwaka mpya kwamba masuala mengi yatakuwa poa zikiendelea kunasa kwenye bongo.

Lakini ukweli ni kwamba hakuna jipya katika maisha zaidi ya kuendelea kusuguana na makali ya bajeti. Mlo wa mmoja kwa siku haiwezi tena kuwa habari mpya.

Kupanda hata daladala iliyofurika hadi kutapita limekuwa jambo la anasa. Wabongo walio wengi sasa hasa waishio katika miji ya kuhitaji mabasi kwenda katika majukumu wamepungua miili.

Wanapungua miili kwani kila uchao wanasaga mguu kwenda katika majukumu yao. Hili ni jambo jema kwa afya ya mwili kwani vitambi vinapungua.

Nani atathubutu kupanda mabasi manne kila siku na nauli yenyewe iko juu? Kwa hiyo wakati mwingine unapunguza bajeti kwa kutembea kwa miguu ili nyumbani nako wauone mlango wa maliwato.

Huo ulikuwa utangulizi wa Mzee wa Busati Jumanne hii ambayo kwake ingali ikimpa hamu ya kuendelea kuwamo katika safina hii ya mwaka 2008.

Si lengo lake kujadili hali ya uchumi kwa Wadanganyika kwani kufanya hivyo kutazidi kumwongezea machungu ya maisha. Hana mbadala. Kujadili pasipo suluhisho ni dhambi.

Leo hii Mzee wa Busati ameona ni vema atete na wadau wa muziki nchini ambao bila shaka mambo mengine yamenasa katika vichwa vyao pasipo kujua kwamba wanapotoka.

Mwandika Busati ni msemakweli pia. Wala hajifichi na wala hawezi kukana kwamba anatumia yale maji yenye rangi ya mende kutoka Ilala.

Huwa anakaa kwenye mikusanyiko ya aina hiyo mara kwamba mara kwa kile kinachoitwa mkao wa majadiliano na wakati mwingine kupoteza mawazo.

Awapo huko mara nyingi huona wanamuziki wakipamba ukumbi kwa maikrofoni zao. Wanaimba kwa mbwembwe kuwapa burudani wateja katika baa husika.

Hakika wanatia faraja kwa nyimbo wanazoibuka nazo kwa siku. Wateja watahamasika na wengine pombe zikifika pahala pake huacha viti vyao na kwenda kuserebuka. Hiyo ni faraja ya moyo.

Lakini kinachomshangaza Mwandika Busati ni kwamba hao wanaoalikwa kutumbuiza wamekuwa kama ndege aitwaye kasuku.

Kama hujui sifa ya kasuku basi ni kwamba huyu ndege ana tabia ya kuiga kusema kama binadamu na mara nyingi hufugwa katika nyumba.

Atajitahidi kuiga kila kisemwacho. Hii ndiyo sifa kuu ya kasuku, ndege mwenye rangi nyingi ambaye ni kipenzi cha binadamu katika makazi yake.

Anachosema Mzee wa Busati kuhusu hizo bendi za muziki zinazotumbuiza katika flani flani ni kwamba wamezidi kuiga nyimbo za wasanii wengine.

Lakini wanatamba wakijiita wao ni wasanii mahiri. Watajiita wanamuziki waliobobea. Huku ni kupotosha ukweli wa mambo. Pengine lugha iko gongana na hivyo kutojua maana halisi ya msanii.

Ajuavyo Mzee wa Busati ni kwamba msanii ni kwamba ni mtu mwenye ustadi wa kuchora, kuchonga au kutia nakshi. Husemwa pia kuwa msanii ni mwenye ufundi wa kutunga na kutoa mawazo yake kama vile kwa ushairi, hadithi au tamthiliya.
Haijasemwa kwamba msanii ni mtu mwenye uwezo wa kuiga iga kama kasuku. Huo si usanii bali ubabaishaji.

Kama kweli mmeamua kuimba si mtunge nyimbo zenu? Ya nini kuendelea kuimba nyimbo za kale? Za kwenu zitasikizwa lini?

Mmebaki na nyimbo za Juma Kilaza na David Kabaka kila siku. Af mkitoka hapo mmeutwika kwa pombe za bure mnatembea kwa matao mkisema kwamba nyie ni wasanii.

Kama kweli mmeamua kushika vipaza sauti kwa jina la muziki basi leteni tungo zenu zisikike ili siku moja nanyi mtambe kwamba mlipata kufyatua albamu iliyovuma.

Si dhambi kuiga nyimbo za kale lakini isiwe kuwahadaa mashabiki kwa onyesho zima. Imbeni nyimbo zenu ili hata mkijisifu muwe na pa kuegemea.

Hivi leo hii Mwandika Busati anawezaje kujiita mwimbaji mahiri eti kwa vile tu kapaza sauti kanisani wakati wa kuimba tenzi za rohoni. Haikubaliki!

Nyimbo za kina Mbaraka Mwishehe zingali zinapendwa hadi kesho. Wengi wanapenda kuzikiza lakini ukweli wa mambo ni kwamba kubaki kuziiga pasipo kutunga mpya ni kupoteza wakati.

Mwandika Busati amefikia kikomo kwa wiki hii. Ataendelea na mengine juma lijalo kwa kasi ile ile pasipo kuogopa tindikali wala mtutu wa bunduki. Panapo ukweli tutaambizana.

Wasalaam,

No comments: