na innocent munyuku
JUMA moja limeshapita tangu mwaka mpya wa 2008 uanze. Salamu zingali zikimiminika kila mmoja kwa dua yake anaomba mema kwake na jirani yake. Ni dua mtindo mmoja.
Meseji zimejaa kwenye simu za viganjani. Maneno matamu yanapendezesha nafsi ingawa ukweli wa mambo ni kwamba si kila liombwalo huja kama atakavyo mwombaji.
Dunia ndivyo ilivyo. Nyakati kama hizi hata aliyekuwa akikusengenya atapumzika kwa muda kwani anayo furaha ya kuuona mwaka mpya.
Mzee wa Busati naye yu kundini akiwaza na kuwazua. Ameshatafakari mengi ya mwaka uliopita. Mwaka ulikuwa umejaa zege mgongoni. Mizigo ilikuwa mizito.
Utafanyaje katika hilo? Utakimbia familia? La hasha! Ni mapambano kwa kwenda mbele hata ikibidi kuwa mpambe wa mwenye ngwenje ni jambo jema.
Mbona kina Momburi ndivyo wanavyoishi? Wakiwa na haja ya bia za bure wanajua pa kukimbilia. Watapiga mguu hadi Mwana Mkude. Huko watakula matumbo na vichwa vya kuku wakishashibisha minyoo tumboni watashushia na safari lager mbili zilizoongezewa viroba vya konyagi.
Hapo mwanawane muziki unakuwa mkubwa kichwani. Watachanganya Kimombo na Kichaga juu. Basi utamu huo hauna maelezo ni kama vile wako peponi.
Enewei tuachane na hilo kwani alilojia Mzee wa Busati wiki hii ni hili la sanaa na utamaduni wa M-bongo. Ni ngumu kidogo kusema kwa uwazi kabisa kwamba ni wapi hasa utakumbana na sanaa ya Tanzania hasa katika muziki.
Pengine Mwandika Busati ataonekana mtata katika hili lakini ukweli ni kwamba leo hii ukisikia matamasha ya muziki basi usikae ukadhani kuwa huko utakuta mdumange au mganda.
Wala usisumbuke ukatoka mbio kuwahi tamasha hilo kwa ndoto ya kukuta Ingoma au Sindimba. Huko utakuta magoma kutoka ng’ambo. Vijana wakipishana kwa vikumbo kughani mashairi ya kina Tupac au Britney Spears.
Wataimba kama waimbavyo Waingereza na Wamarekani. Hakuna anayethubutu kufuata nyayo za Fela Kuti na Afrobeat zake. Wamesahau kabisa kuwaenzi wasanii wa bara la Afrika.
Hakuna tena ile shauku ya kuusambaza muziki wa Afrika. Kilichobaki sasa ni kujivunia mengine yanayovuma nchi za Kimagharibi. Watavaa kama Wamarekani na hata sema yao katika ndimi zao ni lafudhi za huko huko.
Huwezi tena kumtofautisha Ambwene na Cooper. Si rahisi tena kumtambua Achimwene na Smith. Ni ngumu pia kumtofautisha Shemakame na Erickson. Wote wanafanana kwa tabia, mavazi na mengineyo.
Ukiwaambia kuwa huko waendako siko wanakuja juu na kukuona u mjinga, mwingi wa tongotongo na usiyejua lolote katika dunia hii. Watakueleza kwa tambo pasipo hofu kwamba wao wanakwenda na wakati na huu ndio wakati.
Lakini je, hivi kweli huko ni kwenda na wakati au ni kukosa mkakati? Usingizi gani huu usiokuwa na tamati? Akili zimedumaa hata akawapiku nyati?
Hata simba mwituni wanazo kanuni hali kadhalika kunguni na nyuni. Iweje mwana wa adamu akose msimamo akashindwa kutambua kuwa kuendelea kukumbatia ya Magharibi ni hila kwa sanaa ya Afrika?
Mzee wa Busati kama hakosei huu ni mwaka wa nane tangu atambe na safu hii katika magazeti mbalimbali ya Kibongo na katika siku zote hizo amekuwa akipayuka juu ya uovu wa wasanii wengi nchini kuidharau sanaa ya Tanzania.
Walio wengi wanadhani kukaa na kujifunza kupiga ngoma ni ushamba na hapaswi kuitwa msanii. Wanadhani kuimba nyimbo za asili yao ni kujidhalilisha. Hawa wamezingirwa na utumwa wa akili.
Wamefugwa kwenye zizi la ujinga wa kujitakia. Hawaoni tena kama nyimbo za asili zina nguvu ya kuutambulisha utamaduni wa Mtanzania. Wamebaki kuchungulia runinga na kuiga wayaonayo kwenye vioo hivyo.
Bila shaka watasema huko ndiko liliko soko kubwa la muziki lakini je, kuna maana gani ya kuimba nyimbo zenye maisha kama karatasi ya chooni? Zitavuma leo, kesho kwisha habari.
Huo ni mtazamo tu wa Mwandika Busati. Mwenye kuwaza vinginevyo yu huru kuleta yake yapate kujadiliwa bila ncha ya upanga.
Ndoto ya Mzee wa Busati ni kwamba ifike siku M-bongo afike Ottawa kwa ziara ya kutambulisha nyimbo za Tanzania. Ifike siku Mtanganyika azuru New York au London akitangaza mema ya kwetu kupitia santuri zake.
Pamoja na ukweli kwamba wapo waliowahi kufanya hilo, bado kuna ufinyu wa wasanii kujitutumua na kufikia hatua hiyo. Walio wengi wanaimba ili wapate kula leo.
Kutokana na hilo ndiyo maana wamebaki kuiga badala ya kubuni. Amkeni msilale kama pono. Badilikeni ili wadau wapate pahala pa kuusikiliza muziki wa Tanzania.
Huu ni ukomo wa Mzee wa Busati wiki hii. Anatulia na kujipinda kwa ajili ya mambo mengine ya kujenga nchi. Lakini hajaacha kuomba mema kwa ajili ya Wakenya wanaopukutika sasa huku mzee mzima Kibaki akipunga upepo kwenye kasri lake jijini Nairobi ingawa wengine wanaliita jiji hilo kuwa ni New Robbery.
Wasalaam,
Sunday, January 6, 2008
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment