Na Innocent Munyuku
KUMEKUCHA! Mzee wa Busati katumbukia kwenye buti tayari kwa mwendo wa kila Jumanne. Kwake mambo yako sawia ingawa anaelewa kwamba wapo waliopata majereha kiduchu kwenye pochi zao wakati wa ufufuo wa Bwana Yesu.
Hata hivyo, uhai ungalipo pumzi ya Mola inashuka. Hata kama mlo ni wa shida hayo ni majaribu na mapito ambayo mwenye kutoka damu sharti akumbane nayo.
Kina Momburi bila shaka sasa wanatweta hawajui watafikaje Tabata Relini. Si mchezo papake Mwanyamala hadi Tabata kwa mguu! Yataka moyo mwanawane.
Bila shaka sasa wanatembeza bakuli wakitoa sera tamu tamu ili wapate kufika tarehe njema za mwajiri. Lakini analoomba Mzee wa Busati ni kwamba msije zua misiba ambayo haipo ili mpate ngwenje za matanuzi. Mkitenda hayo mtakosa thawabu.
Juma lililopita Mwandika Busati alinena juu ya ukakasi wa sanaa hasa ya maigizo na mchezo wa ngono katika eneo hilo.
Akaweka wazi kwamba baadhi ya vikundi hivyo vya maigizo hasa vinavyoonyesha kazi zao kwenye runinga vimekuwa na mchezo mchafu wa kuwalazimisha ngono kina dada (waigizaji) ili wapate nafasi ya kuonekana kwenye vioo vya televisheni.
Na moja ya aya katika makala hayo ya juma lililopita ilisomeka hivi: “Mambo kama hayo kwa hakika yanasikitisha na kutia kichefuchefu. Kwamba kama viongozi wa vikundi fulani vya sanaa wanafikia hatua ya kudai rushwa ya ngono hii ni aibu.”
Kuanzia mwanzo wa waraka huo wa hadi mwisho hakuna pahala Mwandika Busati ametaja kikundi fulani au jina la kiongozi anayeendekeza ukware.
Lakini cha ajabu akaibuka mtu mmoja aliyejiita kiongozi wa kikundi cha sanaa za maigizo na kumtuhumu na kisha kumhukumu Mwandika Busati kwamba hakufanya kile yeye alichokiita ‘research’.
Akahitimisha hivyo kwamba katika sanaa ya maigizo mambo hayo hayapo. Mzee wa Busati naye akapata wasaa wa kuuliza iweje aitwe mdanganyifu?
Hiyo njemba ikadai eti kwa vile sikuwapa nafasi viongozi kupata maoni yao!(?). Akasisitiza hilo kwamba sikuwahoji viongozi wa makundi kisa Mzee wa Busati hakufika kwake!
Yeye ni nani hadi alazimishe kufikiwa? Pengine angesema kwamba yeye ndiye kinara wa viongozi wa vikundi vya sanaa nchini basi hoja yake ingekuwa inaelekea kwenye ukweli.
Kwani ni lazima kila kile alichokiita ‘research’ afikiwe kila mmoja? Twaangalia uwingi wa matukio na kama yeye hafanyi hivyo basi Muumba amrehemu.
Lakini ukweli wa mambo ni ule ule kwamba HAMKANI ndani ya sanaa kuna baadhi ya matukio ya kulazimisha unyumba ili binti fulani apate nafasi
Hata katika baadhi ya filamu za Kibongo nako ni kama shambiro kwa maana ya sehemu ambayo hufanyika mambo ya hovyo hasa yahusuyo ukahaba au uhuni ufananao na huo.
Mwandika Busati alitarajia kwamba jamaa aliyejiita kiongozi wa kundi la sanaa la maigizo angeleta hoja ya ushirikiano ya kukemea hali hiyo na si kushutumu na kisha kuhukumu kwamba Mwandika Busati hajui alichokinena.
Leteni hoja mezani tusemezane na si kujitakasa kwa maji ya bahari.
Haya si mashambulizi la hasha! Kinachosemwa na Mwandika Busati ni kwamba yafaa wakati mwingine kujadili ndani ya nafsi kabla ya kupayuka kwamba fulani katema urongo.
Au mpaka siku zipigwe kura za siri ndipo mpate kusadiki yasemwayo na Mzee wa Busati? Mwandika Busati aseme uwongo ili iweje?
Mlitaka asiseme ili iweje? Nanyi kuweni wadadisi na hakika mtayabaini haya kwamba yapo baadhi ya makundi ambayo hongo ya ngono imetawala.
Ndio maana juma lililopita ikawekwa wazi kwamba hawa si wasanii kwa sababu wameingia humo kiufisadi. Wamevaa joho lenye udhalimu ndani yake.
Habari ndiyo hiyo kwamba haya yasemwayo yapo na yanaendelea kufanyika. Kukaza koo na kusema kwamba fulani kasema uwongo bila shaka ni kutotenda haki.
Mzee wa Busati amefikia ukomo kwa juma hili akitaraji maoni kutoka kwa wadau.
Lakini jambo moja lililo wazi ni kwamba yu radhi hata ikibidi kupigwa mawe akitetea hoja yake. Hakuna urongo hapa. Wasanii wengi wa kike ni mashuhuda na haya.
La maana ni kuangalia namna ya kuangamiza kirusi hicho. Kufumba macho kwa joho la utakaso ni kuiangamiza sanaa.
Kila jema liwashukie wadau wa safu hii. Kwa waliojeruhiwa na Pasaka kubalini hali halisi mtajipanga mwaka ujao.
Wasalaam,
Saturday, March 22, 2008
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment