Na Innocent Munyuku
KWA wajuzi wa Kiswahili, shambiro hutajwa kuwa ni sehemu ambayo hufanyika mambo ya hovyo hasa yahusuyo ukahaba au uhuni ufananao na huo.
Aghalabu shambiro huwa ni nyumba au pengine yaweza kuitwa danguro maalumu kwa kufanya umalaya.
Hilo ndilo shambiro. Wakware watajazana humo wakishindana kwa uovu wa kila aina. Hiyo ndiyo meli yao.
Mzee wa Busati juzi kasoma kwenye gazeti moja kwamba baadhi ya wasanii wa kike nchini wamekuwa wakilazimika kutoa uroda ili waonekane katika luninga.
Kwamba ili msanii wa kike apate kuonekana katika igizo fulani kupitia televisheni basi lazima avuliwe chupi.
Sharti atoe unyumba kwanza na kisha apate nafasi ya kung’ara katika igizo na mashabiki wapate kumwona akifanya vitu vyake kwenye luninga.
Mwandika Busati alipata kusikia habari ifananayo na hiyo kwamba hata katika mashindano ya kuwasaka visura rushwa ya ngono imetanda.
Mambo kama hayo kwa hakika yanasikitisha na kutia kichefuchefu. Kwamba kama viongozi wa vikundi fulani vya sanaa wanafikia hatua ya kudai rushwa ya ngono hii ni aibu.
Usanii kwa lugha nyepesi ni karama. Muumba ambaye ni Mola huwajalia baadhi yetu vipaji vya kila aina ukiwamo usanii.
Japo sanaa yahitaji pia elimu ya darasani, ukweli wa mambo ni kwamba mtu huzaliwa na sanaa.
Anachosema Mzee wa Busati ni kwamba kama leo hii watu wanatamba katika sanaa eti kwa sababu tu walitoa hongo ya ngono hawa hawawezi kuitwa wasanii.
Hawa si wasanii hata kidogo. Si wasanii kwa sababu wameingia humo kiufisadi. Wamevaa joho lenye udhalimu ndani yake. Wamelazimisha kuitwa wasanii.
Pengine yafaa waitwe makahaba au malaya ambao kwa jina la sanaa wanafanikiwa kuihadaa jamii.
Mzee wa Busati sasa amefumbua macho na anachokiona ni historia chafu ya viongozi wa vikundi vya sanaa na wasanii wao.
Kama kiongozi anathubutu kutaka mapenzi kwa msanii wa kike ili apewe kipaumbele ni lini basi kaya zetu zitawaona wasanii wa kweli?
Dunia ya aina hii haiwezi kukubalika iendelee kutamba chini ya jua. Hawa hapa si pahala pao. Yafaa waangamizwe ili watoweke.
Haifai kuwa na wasanii ambao historia zao ni mbaya. Haifai kuwa na waigizaji wanaowika kwa sababu walitoa miili yao kama asusa kwa viongozi wao wa sanaa.
Hawa ndio wanaotarajiwa kuwa vinara wa kupinga maovu kwa kutumia vipaji vyao. Hawa ndio dira ya jamii. Kama wanakiuka maadili basi si vema kuwaita wasanii bali wahuni!
Katika hili Mzee wa Busati anawaomba wadau kuungana ili kupiga vita maovu kama hayo. Mambo ya aina hii si ya kuyafumbia macho kwani mwisho wake ni mbaya.
Hawa wanatarajiwa kuwa wahamasishaji wa mambo mbalimbali kama vile vita dhidi ya Ukimwi au ufisadi.
Leo hii msanii atawezaje kupanda jukwaani kuhamasisha vita dhidi ya Ukimwi huku akiwa mkware? Bila shaka atakuwa anacheza muziki asioujua.
Basi na wenye masikio wasikie maneno haya ambayo Mwandika Busati ananena kwa uwazi na ukweli. Wanawali fungeni vibwebwe kupinga mtindo wa kutoa miili yenu kwa ajili ya kuonekana katika televisheni.
Enendeni kila njia mseme kwamba sasa inatosha na si wakati wa kuendelea kunyanyasika kwa jina la sanaa.
Kama baadhi yenu mnadhani haiwezekani kupinga udhalilishwaji huo basi badilisheni fani. Jihalalisheni moja kwa moja kuwa makahaba kwani madanguro yangalipo.
Mzee wa Busati amefikia ukomo kwa juma hili ambalo waumini wa Kristo wanasubiri ufufuo wake.
Kila jema katika Pasaka ila angalieni msije angusha magari kama ilivyo desturi ya Mzee wa Kutibua anayetamba kifedhuli maeneo ya Makumbusho. Msifuate nyayo zake kwani huko ni kujiangamiza.
Wasalaam,
Sunday, March 16, 2008
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment