Sunday, March 30, 2008

Wanjamanga si dawa ya chongo

Na Innocent Munyuku

KATIKA uso wa dunia, mwanadamu kapewa akili inayomwezesha kupangilia mambo mbalimbali maishani mwake.

Hata hivyo, husemwa kwamba akili ni nywele kila mtu na zake. Hii maana yake ni kwamba si rahisi mkafanana mawazo na ndio maana katika jamii huzuka mijadala ya mabishano.

Lakini kwa kutumia akili hiyo hiyo binadamu amekuwa fundi au mahiri wa kugeuza mambo fulani. Mtu mwenye ukurutu kwa mfano atajitahidi kuficha maradhi hayo kwa kuvaa gubigubi.

Hali kadhalika kwa mwenye mapunye kichwani haishangazi akionekana na kofia au kilemba. Hizo zote ni mbinu za kuficha maradhi hayo mbele yaw engine.

Lakini kuna mengine hayafichiki kama vile chongo. Mwanawane hata kama utapaka wanjamanga, chongo halifichiki kama lilivyo pembe la ng’ombe.

Mzee wa Busati kaibuka Jumanne hii ya ‘wajinga’ akiwa na hoja juu ya ukuzaji wa soka ndani ya Tanzania ambayo kimsingi ni kama vile wadau wanatwanga maji kwenye kinu.

Mengi yamekuwa yakisemwa kwa mbwembwe juu ya ukuzaji wa soka ndani ya bongo lakini ukweli wa mambo ni kwamba mbwembwe hizo ni danganya toto.

Kinachofanywa na viongozi katika mamlaka za soka ni sawa na kuficha chongo kwa kupaka wanjamanga. Porojo zimejaa kila mahala na ndimi zao zimejaa ushawishi wa giza.

Angalia msimu wa usajili unapowadia. Balaa mtindo mmoja. Viongozi wa klabu ndio wenye kimbelembele cha kuchagua wachezaji wanaodhani wataifaa timu yao.

Wanafanya hivyo bila kuwapa nafasi makocha katika suala la usajili. Matokeo yake ni kwamba si ajabu ukakuta timu haina beki mahiri kwa sababu pengine viongozi waliamua kuwajaza washambuliaji pekee.

Leo hii viongozi wa klabu wamekuwa kama miungu watu. Wengi wao hawana hata sifa za kuitwa viongozi wa soka. Hawafai waitwe hivyo kwa vile hawana taaluma ya mpira wa miguu. Wanachojua ni kupiga soka na kueneza ufitini.

Kwani hamjapata kusikia kuwa kiongozi fulani kaidhinisha adhabu kwa mchezaji pasipo sababu za msingi? Yanatokea kila leo na yangali yakiendelea.

Mwandika Busati anachosema ni kwamba kauli nyingi za zinazohubiri makuzi ya soka hazina maana kwa sasa kama mamlaka zinazohusika hazitaangalia kiini cha udumavu wa medani hiyo.

Haina maana kusema kwamba Wabongo wajipange kucheza fainali za Kombe la Dunia huku viongozi wababaishaji wasioweza hata kuchanganua mambo wakiendelea kukalia viti hivyo.

Anachonena Mzee wa Busati ni kwamba linapokuja suala la kukuza soka watoa hoja waangalie watokako, walipo na mwelekeo mbele yao.

Siku chache zilizopita, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Joel Bendera katoa mapendekezo yake katika mbio za kuboresha soka nchini.

Bendera amesisitiza umuhimu wa kuwashirikisha waamuzi na madaktari katika mafunzo ya soka. Kwamba wadau hao wapewe mafunzo ya mara kwa mara.

Huo ni mtazamo chanya unaungwa mkono na Mwandika Busati lakini bado ipo haja ya kuangalia magugu yaliyojaa ndani ya klabu mbalimbali za soka na vyama vyake.

Hatuwezi kuwa na mng’aro katika soka huku walioshika nafasi za uongozi wakiwa wapiga soga wasiokuwa na dira ya maendeleo.

Matokeo yake ni kwamba klabu nyingi zimebaki kuwa makaburi ya wachezaji kwa sababu viongozi wake wamekosa mwelekeo wenye neema. Hao kazi yao ni porojo na mahubiri ya ‘soka fitna’.

Kubebana na kuficha maradhi kwa kuvaa gubigubi hakutasaidia kwani ipo siku mambo yataharibika zaidi ya leo.

Leo hii bado kuna viongozi wa klabu za soka wanaoendelea kuamini ushirikina katika mchezo huo. Hawapeleki timu dimbani pasipo kuwalaza wachezaji makaburini au kuwanyoa nywele za kwapa.

Je, kwa sampuli hii ya uongozi mwadhani mtapaa kwenye ndege ya mafanikio ya soka? La hasha! Mtabaki kama mlivyo.

Mzee wa Busati hana budi kukunja jamvi. Ajiendee porini kwake kwa mapumziko akiamini kwamba somo limeeleweka.

Kwa walionaswa katika Siku ya Wajinga leo hii poleni kwa kujazwa ujinga. Vinginevyo muwe makini msimu ujao.

Wasalaam,

No comments: