Sunday, May 18, 2008
Chonde msimu huu msiyaige ya kifaurongo
Na Innocent Munyuku
ASIKWAMBIE mtu raha ya mjini sharti uwe na ngwenje kibindoni. Utakula unachotaka badala ya kula unachopata. Hayo ndo maisha ya mjini.
Lakini wakati mwingine raha hizo hugeuka karaha pale unapoona kuwa wenye kufanya matanuzi wengi wao wamezipata fedhwa kwa njia zisizo halali.
Hao ndio waliojaza miji miaka hii. Wanatumia fedha haramu kufanya matanuzi na kibaya zaidi ni kwamba wanatumia ngwenje hizo hizo zinazonuka kujitakasa.
Kujitakasa kwao kunakuja kwa njia ile wanayoiita eti misaada kwa yatima na wasiojiweza. Hivi kweli sadaka zenu zinakubalika kwa Muumba?
Kilio hiki cha Mzee wa Busati kimekuja baada ya kufanya kajitafiti kiduchu na kubaini kuwa katika maonyesho mengi ya burudani yanayopangwa na kukamilika, mpangilio mzima umejaa dhuluma.
Pengine mfano mdogo tu ni pale unapoona wajanja wa mashindano ya urembo nchini wanapomaliza kukusanya viingilio na kisha kujifanya kusaidia yatima.
Ukweli wa mambo ni kwamba ukiangalia mchakato mzima wa mashindano hayo hadi fainali kwa walio wengi wamepitia dhuluma. Watawalaghai wadhamini na washiriki pia. Hivi kweli huu ni uungwana?
Anachosema Mzee wa Busati ni kwamba dhamira ya misaada ya aina hiyo iendane na uhalisia wa wanaopewa misadaa katika jamii.
Mwandika Busati angali akielea hapo hapo katika ulimbwende kwa hoja kwamba misaada hiyo inayotolewa ni kweli kwamba inawasaidia walengwa? Pipi ni biskuti?
Hivi ni kweli kwamba yatima wanahitaji sana peremende na biskuti? Hiyo iwe ziada ila la msingi liwe kuwajali katika elimu ili maisha yao yawanyokee huko mbele ya safari.
Si waandaaji wa urembo tu wenye hulka ya kutenda hayo bali asasi nyingine za kijamii ambazo wakati mwingine hutumia yatima kujitangaza. Huku ni kupotoka.
Mzee wa Busati ameamua ayaseme haya mapema kwani kwa uzoefu wake watu wa aina hiyo kila mwaka wamekuwa wakiiga maisha ya kifaurongo.
Kifaurongo au pahala pengine hujulikana kama kiforongo ni mdudu ambaye kwa kawaida hupatikana katika kokwa ya embe na hujikinga kwa kujifanya amekufa pindi aguswapo.
Hivyo ndivyo walivyo hao wanaosemwa na Mwandika Busati. Wakiguswa kwa kuelezwa ukweli hukaa kimya na kujifanya hawasikii ama wamelala fofofo.
Hujifanya hamnazo kwa kutojali wanayoambiwa kuhusu mwendo wao katika jamii. Leo hii utakemea juu ya rushwa ya ngono, kesho wanayarudia na hivyo kwenda mbele miaka kibao ijayo.
Kwanini waendelee kuziba masikio? Au hawa si wenzetu katika jamii? Mitima yao i migumu kiasi gani? Mkiguswa leteni mshituko na si kujifanya mmekufa.
Mwandika Busati ataendelea kuyasema anayoyaona kuwa ni mabaya na hataacha kuyasifu yaliyo mema. Anafanya hivyo ili kutoihadaa dhamira yake.
Dhamira anayoisema ni ile ya kutumia vipaji mbalimbali kuwasaidia mambo ya msingi wasiojiweza na si kuwapa yanayoyeyuka kwa siku moja.
Hima uwe mshikamano, wasanii na wabunifu wa aina mbalimbali wajenge msimamo wa kuwasaidia kwa dhati yatima walio vituoni na wale wanaolala majalalani. Kama ni peremende basi viongwezwe na vingine vya kuwajengea maisha.
Mwandika Busati wakati anaelekea ukingoni atoe pongezi zake kwa Taifa Stars kwa kuinyamazisha Uganda Cranes. Basi na wakaze buti, wasiogope fangasi ili wakanuse ardhi ya Ivory Coast katika fainali za Kombe la Mataifa Afrika.
Mzee wa Busati atashangaa kama kutakuwa na porojo tena msimu huu. Amkeni na kasi iwe ya mbele kwa mbele.
Huu ndio ukomo wa Mzee wa Busati kwa juma hili. Wiki ya maumivu kwa walio wengi na mifano iko wazi tu. Idadi ya wanaoning’iniza miguu kwenye viti virefu imeshuka. Wametoweka kama ndui.
Mzee wa Kutibua na jopo lake pale Tabata Relini wameingia mitini. Simu zao zimezimwa kwa kuhofia madeni. Ila huziwasha usiku wa manane kwa ajili ya kusoma meseji. Poleni ila ipo siku mtajuta na kusaga meno.
Kama kwenye ule mlima mrefu kuliko yote barani Afrika hakuendeki basi ni heri mwende pachoto mkakusanye mabibo mtengenezee uraka ili mjidunge kwani hamkani fedhwa ya lager hamnayo!
Wasalaam,
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment