Sunday, May 11, 2008

Bado tuendelee kuisubiri kastabini?

Na Innocent Munyuku

KUMEKUCHA! Ni Jumanne nyingine ambayo Mwandika Busati anatua kwenye anga zake za kujidai kwa ajili ya kuleta porojo zake.

Wiki imeanza vema ingawa siku kadhaa zilizopita mambo yamekwenda upogo. Ngwenje zimeanza kuyeyuka kwani kuna mengi ya kutekelezwa yamefuata mkondo. Suruali zimekuwa tupu.

Waliokuwa na ubavu wa chips na kuku wa kompyuta sasa wanalamba ugali na maharagwe ya Mbeya kwa sababu hata mkaa wa Msata haupatikaniki! Bei juu kwa kila kitu.

Hali inatisha wajameni na kama twafundwa juu ya kusoma alama za nyakati hii ni wazi kwamba Bunge la Bajeti nalo msimu huu litajaa maumivu. Kama vipi mlalahoi kapige debe upate mlo!

Mzee wa Busati wiki hii hoja yake kuu ni juu ya haya mashindano ya Kombe la Taifa yanayoendelea kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Maelfu wanakenua meno lakini kuna jambo haliko wazi.

Mzee wa Busati kasoma magazeti, kasikiza maoni ya wanaojiita kuwa ni wadau wa soka ingawa wanaonekana kujikita kwenye taarabu na muziki wa dansi. Eniwei wasihukumiwe kwa hayo kwani bongo husemwa kwamba hakuna spesholaizesheni.

Kila mmoja na lwake na ndio maana leo unaweza ukamwona Momburi akinywa Kilimanjaro badala ya Safari lager aliyoizoea anachojali ni ulabu wa kulipua ubongo wake ili kesho yake ahangaike kusaka ilipo supu ya mapupu.

Ni kwamba bongo hapa kila jambo linakwenda hata kama halikupangwa liwe hivyo. Na kwa mantiki hiyo usishange waziri fulani nyeti akienda kuwa mgeni rasmi kwenye Kipaimara.

Ataacha shughuli nyeti za kitaifa na kukimbilia huko. Huyo bila shaka anakuwa amesahau kuwa kuna yatima wanaosubiri japo mkono wake waushike nao wafarijike.

Waziri kama huyo amesahau kula na watoto wa mitaani ambao daima mlo wao uko jalalani. Hayo yote yamesahaulika na wakuu wetu wa kaya. Wamebaki kukumbatia urafiki na kwenda kuhudhuria ubarikio wa washikaji zao na kuwavuta wanahabari kama vile ni suala la kitaifa.

Hata hivyo, porojo za Mzee wa Busati hazilengi kuwashukia hao juma hili. Anawaweka kiporo wazidi kuharibu ili siku ikifika apate mengi ya kutema kwenye ndimi zake. Acha wawekwe kiporo.

Wiki hii anachosema Mwandika Busati ni kuhusu hayo mashindano ya Kombe la Taifa. Kwamba hivi lengo haswa ni nini?

Shirikisho la Soka Tanzania-TFF halina budi kuweka wazi maana halisi ya mashindano hayo kwani sasa washika kalamu na wadau wengine wa soka wamekuwa wakisagana kuhusu kiini cha michuano hiyo.

Ukikutana na nasoro utakwambia kuwa ni ya kusaka vipaji lakini wakati huo huo Mwakatobe atasema kuwa ni ya kusaka fedha za kuisaidia timu ya mkoa. Ukweli ni upi?

Mdau mwingine wa soka majuzi katanua msuli wa koo akasema eti mashindano hayo si ya kuibua vipaji na kwamba kama kuna michuano maalumu ya kufanya hivyo. Akaitaja kuwa ni Copa Coca Cola.

Lakini pamoja na mchanganyiko huo wa habari bado Mzee wa Busati anaamini kwamba mashindano hayo hayakupaswa kuwashirikisha wanasoka ambao tayari wamevuma Ligi Kuu Tanzania Bara.

Michuano hiyo ingabakishwa kwa ajili ya ndugu zetu wa Pachoto ama Kigoma ambao hawana mwanya wa kushiriki mashindano ya kimataifa kama hayo.

Hivi kweli kulikuwa na umuhimu kwa timu ya Mkoa wa Ilala kuwajaza nyota wa Simba na Yanga? Hii maana yake nini? Kwani ndani ya Ilala hakuna wanasoka chipukizi wa kuuwakilisha mkoa huo?

Anachokiona Mzee wa Busati ni kwamba michuano hiyo imebakwa na kuna haja ya TFF kujipanga na kuweka kanuni.

Kama Mwandika Busati angelikuwa na mwanya wa kupendekeza angelisema kwamba mashindano hayo waachiwe wanasoka wasiovuma ili miaka ijayo wanasoka waliofichika waongeze bidii watambulike katika ushiriki wao.

Kwa wajuvi wa Kiswahili, kastabihi husemwa kwamba ni chombo cha chuma au plastiki kinachowekwa kwenye ncha ya kidole cha shahada wakati wa kuingiza sindano katika kitambaa wakati wa kushona ili sindano isichome. Pahala pengine, kastabini huitwa subana ama tondoo.

Na ndio maana Mzee wa Busati anasema kwamba bado wadau wa soka wanapaswa kuwa na subira. Wasubiri ujio wa kastabini na waache wenye ubavu wa kupanga yasopangika waendelee na mambo yao.

Vinginevyo papara italeta yasiyoelezeka. Hadithi ya kupanda kwa soka itakuwa yenye ukakasi wa kimbunga na kilio cha kusaga meno.

Wasalaam,

No comments: