Sunday, May 25, 2008

Ni dansi au onyesho la vichupi?

Na Innocent Munyuku

BILA shaka mambo yanakwenda sawia. Mwandika Busati kama ilivyo kawaida yake yu safuni kujichanganya na wadau wake katika mijadala ya kila wiki.

Kwa juma hili hakuna shaka kwamba kila kitu kinakwenda vema manake kwenye viti virefu umati umejaa. Lugha zinagongana kwa tambo za kila aina.

Ukipita kwingineko pia watu wanaringa, wakipita kila mahala kwa matao. Utawaambia nini wakati mifuko imejaa shilingi? Muda wa mavuno umewadia na kwa walio wengi kila kitu kinawezakana kwa sababu fedha inaongea.

Mzee wa Busati kama kawaida yake kila siku kwake ni sikukuu. Si kama anazo nyingi bali amejiwekea mfumo usiohitaji makuu. Yeye na vitegemezi vyake hata wakila dagaa na dona yatosha. Vipapatio vya kuku ni majaliwa.

Siku chache zilizopita Darisalama ililipuka kwa burudani ya muziki wa dansi. Mbwembwe kila pahala, mashabiki wa Akudo Impact na FM Academia wakatambiana kila walivyoweza.

Miamba hiyo ya muziki wa dansi ikapiga maonyesho kwa siku moja. Mashabiki wakapagawa kama inavyokuwa kwa Simba na Yanga. Hata leo hii bado simulizi ya maonyesho hayo zinarindima.

Pamoja na mashabiki kupata uhondo huo, Mzee wa Busati ana lake jambo kuhusiana na maonyesho hayo. Jambo lenyewe ni nidhamu ya mavazi jukwaani.

Kilichotokea kwenye majukwaa wakati wacheza shoo wakifanya vitu vyao ni aibu ya mwaka. Mwandika Busati anazungumzia vichupi vya kina dada waliokuwa wananengua.

Hivi kweli huu ndio mfumo mliojiwekea? Wa kupanda jukwaani mkiwa nusu uchi? Akudo na FM Academia wanaweza kutoa jibu kwa swali hili.

Kibaya zaidi ni kwamba katika maonyesho hayo walikuwapo watendaji wa Serikali ambao walijumuika na mashabiki wengine kushabikia muziki uliokuwa ukiporomoshwa. Hakuna siri kwamba hata hao vichupi waliviona.

Je, wamechukua hatua gani juu ya hilo? Hivi muziki huo wa Kikongo hauchezeki hali kuonyeshana mipaka ya Ikulu?
Mzee wa Busati yu radhi aitwe mshamba, wa kuja na majina mengine lukuki lakini hili la kuonyeshana nyeti jukwaani hakika atalikemea. Raha i wapi basi kuonyeshana ya faragha?

Ipo siku wataingia na kuvamia jukwaa wakiwa uchi wa mnyama. Hilo litatokea kwa vile husemwa kuwa dalili ya mvua ni mawingu. Hawataona ugumu kufanya hivyo kwa sababu watakuwa wameshakuwa sugu na uovu wao.

Shingo zao zimeshaanza kuwa ngumu na ndio maana hawaoni soni kusasambua mbele ya hadhara na wanapopigiwa kofi akili zao hucharuka na kuwaka tamaa ya kuzidisha misasambuo.

Zi wapi mamlaka za kusimamia maadili katika sanaa? Hao nao wamekaa kimya. Wamejifungia kwenye vyumba wakijadili namna ya kula fedha za semina.

Hawana mawazo ya kukemea watu wanaokosa maadili jukwaani. Hivi muziki wa aina hiyo sharti wanawake wacheze kwa kuonyesha nyeti zao? Hii maana yake nini?

Au tuseme kwamba dunia ndivyo ilivyo? Kila mmoja yu huru kufanya atakalo ili mradi linaungwa mkono na hadhira. Mwandika Busati haelewi yanayoendelea zaidi ya kumuumiza kichwa.

Basi kama mmeamua kukaa kimya pasipo kukemea, Mzee wa Busati hatafumba mdomo atayasema kwani historia ndiyo yenye kutoa hukumu. Vijukuu vitaelezwa kwamba kibabu chenu hakikupenda mambo fulani.

Huu ndio mwisho wa hoja yake kwa juma hili. Kama ilivyo kawaida yake, Mzee wa Busati anaenda mafichoni kula raha. Ndio manake maisha haya ni mafupi linalowezekana leo lisingoje kesho.

Acha akajitafutie makazi ya faragha kwa kufanya tathmini wakati huu tunapokaribia nusu mwaka. Je, ahadi na mipango ya mwaka 2008 inakwenda sawia au inakwenda upogo?

Vinginevyo kila la heri. Baraka zikufikie hapo ulipo na tuonane juma lijalo tukiwa na siha njema.

Wasalaam,

No comments: