Wednesday, December 29, 2010

Ni uhuru upi tunaojivunia?

Na Innocent Munyuku

MAMA Teresa wa Calcutta aliwahi kusema: “Yesterday is gone. Tomorrow has not yet come. We have only today. Let’s begin.” Mtawa huyo wa Kanisa Katoliki alizaliwa Agosti 26, 1910 na kufariki dunia Septemba 5 mwaka 1997.

Kwa tafsiri isiyo rasmi, Mama Teresa alikuwa akisema kuwa “Jana imepita. Kesho haijawadia. Tunayo siku ya leo. Tuanze kuifanyia kazi.”

Nimeanza makala haya kwa nukuu hiyo kutokana na malalamiko ya baadhi ya viongozi wa Serikali ya Tanzania na watendaji wengine wakuu pindi wanapoulizwa nini hasa kiini cha umasikini wetu hata baada ya kupewa uhuru miaka 49 iliyopita.

Wengi wao watatoa sababu zinazofanana. Watawataja wakoloni ama biashara ya utumwa kwamba ni mambo yaliyochangia umasikini wetu. Hapa wanaizungumzia JANA badala ya kuifanyia kazi LEO waliyonayo mkononi. Pengine itoshe kusema kuwa kuendelea kulalamika wakati huu tunapotimiza miaka 49 ya Uhuru wa Tanganyika ni ukosefu wa akili timamu.

Ninachotaka kusema hapa ni kwamba binafsi ninapotafakari uhuru huu, siamini kama kweli tuko huru. Huu ni sawa na uhuru wa bendera! Tanzania haiko huru kiuchumi na ndiyo maana watu wake wamelala kwenye dimbwi la umasikini.

Tanzania pamoja na kuwa na rasilimali nyingi, wananchi wake wanaendelea kutaabika. Mlo mmoja kwa siku ni jambo la kawaida kwao. Kwa mamilioni ya watu ndani ya ardhi hii kwao huo ndio mtindo wanaostahili na wanaishi sasa wakiwa na mazoea hayo.

Wajanja wachache wamejinufaisha na utajiri wa taifa hili. Tuliowapa dhamana ya kutufikisha katika nchi ya ahadi wametugeuka na kutuacha nyikani. Mali zinachumwa na kuliwa na hao wachache. Nyuso zao zimejaa furaha na wala hawana mawazo ya kuwaibua wengine. Labda watafanya hivyo kwa mtoto wa mjomba.

Hoja yangu ni kwamba sioni mantiki ya kusherehekea siku hii pasipo kwanza kufuta au kuwaangamiza watu wachache wanaosababisha mamilioni ya Watanzania wakose neema kwenye ardhi yao. Hatutakuwa huru kama tumebanwa na minyororo ya ufukara kiasi hiki.

Hao waliosababisha tukaingizwa katika mikataba mibovu inayotugharimu fedha nyingi wasiachwe wapite hivi hivi. Waliobariki mikataba ya hovyo kwenye madini ama vitalu vya uwindaji nao wawajibishwe ili walau keki hiyo iwasaidie Watanzania wengine. Vinginevyo sioni sababu ya kutamba kwamba tuko huru wakati kiuchumi hatuko huru.

Mara kadhaa ninapopata nafasi ya kuketi vijiweni na Watanzania wenzangu hasa vijana nanasa mambo mengi ambayo natamani mtawala wa nchi pia angepata wasaa wa kuyasikia. Bila shaka anayapata lakini kwa vile sina uhakika ni heri nitumie nafasi hii kuyasema baadhi ya masuala yanayojadiliwa kila wakati huko mitaani.

Leo hii Watanzania wanatimiza miaka 49 tangu wapate uhuru kutoka mikononi mwa Waingereza mwaka 1961. Ni sherehe kubwa na yenye simulizi nyingi; mbaya na njema. Miaka 49 ya uhuru si lele mama. Hii maana yake ni kwamba kama ni maisha ya binadamu Tanzania tayari ni mtu mzima anayejitegemea kwa mambo mengi. Si mtu wa hovyo!

Lakini kwa bahati mbaya sana miaka hii ya uhuru ni dhahiri kwamba hakuna jema la kujivunia ukilinganisha na mataifa mengine yaliyopata uhuru baada ya Tanzania. Sisi tumebaki kujisifu kuwa tuna amani.

Amani si jambo baya hata kidogo katika jamii, lakini amani wakati tumbo ni tupu, halina chakula ni sawa na kutwanga maji kwenye kinu. Kinachosemwa mitaani ni kwamba Tanzania licha ya kuwa taifa huru, maisha ya Watanzania yameendelea kuwa magumu kila uchao.

Watu wanalalama kuhusu kupanda kwa bei za bidhaa hasa zile zinazohitajika katika maisha ya kila siku. Hicho ndicho wanacholalamikia. Lakini pia wanasema juu ya uwajibikaji mdogo wa watendaji wa Serikali. Wanazungumzia ubovu wa baadhi ya mawaziri, wakuu wa mikoa na wilaya.

Ingawa wengi wao hawana ubavu wa kupaza sauti, wanasema kwa kadiri wawezavyo kwamba hata watendaji katika ngazi ya vijiji ni waovu wasiopaswa kukalia viti hivyo. Hawaishii hapo, wanakerwa na ubovu wa huduma za afya. Kina mama na watoto, wazee na wahitaji wengine wa huduma hiyo wanakwazwa na utendaji wa wauguzi na madaktari.

Ninaamini kwamba hili halihitaji mjadala mrefu kwani hospitali na zahanati nyingi mambo si shwari kwa wagonjwa. Ni jambo la kawaida kwa wagonjwa kulala wanne kitanda kimoja. Hili si la ajabu. Si jambo geni pia kuwakuta wagonjwa wamerundikana chini wakilalia mkeka. Watanzania wamezoea. Si kama wameridhika bali mfumo umewaweka hapo.

Ukitaka muhuri wa Mtendaji wa Serikali za Mitaa nao siku hizi umekuwa mradi mkubwa kwa hao wenye dhamana ya kuushika. Karatasi haigongwi pasipo rupia mkononi. Wananchi wamezoea kulipa fedha hata kwa yale ambayo wanapaswa wahudumiwe bure. Yanaonekana kama vile yameshakuwa sugu na yasiyoweza kufutwa.

Si hi hayo tu, rushwa nayo ni keo kubwa kwa Watanzania. Wengine wamefikia hatua ya kusema kuwa kama kuitokomeza imeshindikana, basi tuihalalishe. Watu wanakwenda kwa mtindo wa kisasa na kutokana na hali hiyo si rahisi leo hii kuwanasa wala rushwa kama ilivyokuwa miaka 10 iliyopita.

Pamoja na ukweli kwamba wananchi wana mchango mkubwa katika kukabiliana na rushwa, wanacholalamikia wao ni kwamba walio juu ndio viongozi wa jambo hilo. Wanasema kama katibu mkuu wa wizara anadaka rushwa mwananchi wa kawaida afanyeje? Tule wote kwani huo ndio mpango uliopo.

Wengine wananong’ona kwamba kama mbunge fulani kaingia bungeni kwa njia ya hongo diwani naye ataachaje kutetea nafasi yake kwa rushwa? Haya si mambo ya siri yanasemwa lakini kwa bahati mbaya sana si rahisi kuyapatia ushahidi. Lakini ukweli wa mambo ni huo rushwa inanuka nchini.

Hii maana yake ni kwamba walio wengi hawapati huduma kwa kiwango kinachostahili. Kama ni ajira, matibabu na mengine hayapatikani mpaka utoe rushwa. Ukikanyaga polisi utaambiwa hawana karatasi ya kuandikia maelezo ya mlalamikaji. Lakini kabla ya hilo kama utakuwa unahitaji kuwapeleka mahala alipo mtuhumiwa utaelezwa kwamba hawana gari na kama lipo watasema halina mafuta. Kodi tunazolipa zinatumikaje?

Hizo zote ni njia za kukufanya uwe mstari wa mbele kufungua pochi na kuwapa ulichonacho ili mambo yaende. Hii ndiyo miaka 49 ya Uhuru wa Tanganyika tunayoishi. Kwa uwazi ni kwamba maisha ya rushwa hayana maana nyingine zaidi ya kuendelea kukandamizana na kwa njia hiyo kuliangamiza taifa.

Kama nilivyodokeza awali, kuna waliodiriki kusaini mikataba hafifu ya kimataifa ambayo leo hii taifa linaangamia kwa kukosa maarifa. Waliopewa dhamana wamekula cha kwao na hawana hofu ya maisha. Anayepata taabu ni mlalahoi ambaye hajui aanzie wapi ili afikie kilele cha maisha bora. Amekwazwa na mfumo ambao hautaki mabadiliko.

Hayo ndiyo yanayosemwa vijiweni lakini hakuna shaka kwamba ndiyo hali halisi kwa maisha ya kila siku. Je, katika miaka 49 ya uhuru Watanzania tunajivunia nini? Imani na utulivu wa kutoona mabomu yakilipuka mitaani? Pengine yapaswa kuwapo na tafakuri ya kina kwani kwa mtazamo wangu amani kamili maana yake ni kuwa na utulivu wa akili pia.

Kama matumbo hayana shibe sidhani kama mtu anaweza kutembea kwa matao akisema kuwa yu huru na amani ya kweli. Tusibweteke na miaka 49 ya uhuru tusake njia ya kujikwamua uwezo tunao. Wenye mamlaka ya kuwaongoza wananchi waache visingizio, tuache kuijadili JANA badala yake tuifanyie kazi LEO.

munyuku@gmail.com
0754 471 920

No comments: