Wednesday, December 29, 2010

Anguko la CCM haliko mbali

Na Innocent Munyuku

KESHO Ijumaa tunahitimisha mwaka 2010 na kuingia mwaka mpya wa 2011. Kwa watakaobahatika kuuona mwaka mwingine hawana budi kumshukuru Mungu.

Mwaka huu unaogota kesho ulikuwa na mambo mengi. Mipango ilikuwa mingi na bila shaka kuna mengi pia yametekelezwa huku mengine yakitelekezwa.

Binafsi nauangalia mwaka 2010 kwa jicho pana hasa katika ulingo wa siasa. Pilika zilikuwa nyingi kutokana na ukweli kwamba mwaka huu tumefanya uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani.

Uchaguzi wa mwaka huu tumeshuhudia maajabu makubwa. Wananchi sasa wameanza kubaini nini kinawafaa. Wako huru kuchagua wanachokitaka. Zile nyakati za hofu zimekwenda na maji na ndiyo maana Chama Cha Mapinduzi-CCM kimepata wakati mgumu safari hii.

Hakuna anayeweza kubisha hilo. Angalia matokeo katika majimbo ambayo awali yalionekana kuwa nguzo muhimu ya CCM, leo hii yameangukia Upinzani. Wananchi wametumia haki yao na kufanya uamuzi.

Kimbunga cha safari hii ni ishara tosha kwamba miaka ya CCM kucheza na akili za watu zimekwenda na maji. Enzi za kuwalaghai wapigakura kwa vipapatio vya kuku na fulana zinaelekea ukingoni.

Kichwa cha habari cha makala haya kinasema: ‘Anguko la CCM haliko mbali’. Naam, huo ndio mtazamo wangu. Kwamba kwa mwenendo wa chama hicho hivi sasa kama hakitakubali mabadiliko chanya basi huo ndio mwisho wao.

Nasema hivyo kutokana na ukweli kwamba baadhi ya watendaji wakuu wa chama hicho ni kama vile wamelewa madaraka. Baadhi yao hawaambiliki, hawataki kukosolewa. Wameamua kuishi kwa mazoea! Hilo ni kosa kubwa katika utawala.

Pengine hayo yanatokea kwa vile katika uso wa dunia, mwanadamu kapewa akili inayomwezesha kupangilia mambo mbalimbali maishani mwake.

Hata hivyo, husemwa kwamba akili ni nywele kila mtu na zake. Hii maana yake ni kwamba si rahisi mkafanana mawazo na ndiyo maana katika jamii huzuka mijadala ya mabishano.

Lakini kwa kutumia akili hiyo hiyo binadamu amekuwa fundi au mahiri wa kugeuza mambo fulani. Mtu mwenye ukurutu kwa mfano atajitahidi kuficha maradhi hayo kwa kuvaa gubigubi.

Hali kadhalika kwa mwenye mapunye kichwani haishangazi akionekana na kofia au kilemba. Hizo zote ni mbinu za kuficha maradhi hayo mbele ya wengine.

Lakini kuna mengine hayafichiki kama vile chongo. Si dhambi nikawakumbusha viongozi wa CCM kwamba wanjamanga si dawa ya chongo. Si rahisi kuficha kilema.

Nani hajui kuwa leo hii ndani ya CCM kuna mpasuko? Kila kukicha baadhi ya makada wa siku nyingi wamekuwa wakirushiana maneno ambayo kimsingi hayalengi kukiimarisha chama.

Kila mmoja ndani ya chama sasa anayo nafasi ya kupayuka na kutoa hisia zake. Hii ni dalili ya wazi kuwa humo ndani kuna fukuto. Tanuru linawaka na kwa mtindo huo, Wana-CCM sasa wanajikaanga kwa mafuta yao.

Vurugu kwenye kura za maoni ni ushahidi mwingine kwamba CCM sasa inaporomoka. Wengi wetu tumeshuhudia maajabu katika mchakato mzima. Baadhi ya majimbo yameangukia kwa wapinzani kutokana na CCM kucheza karata zisizo.

Mgombea wao anashinda kura za maoni, lakini mwishowe anawekewa zengwe zenye pembe. Hila za aina hiyo zimeiponza CCM kwa kiasi kikubwa.

Kwa mtazamo wangu, CCM inahitaji mabadiliko makubwa. Vinginevyo utabiri wangu hakika utatimia. Kwamba huu ni mwanzo wa mwisho mwa CCM. Bila shaka chama hicho sasa kinahitaji fikra pevu. Vijana wapewe nafasi, wazee wabaki kuwa washauri pale inapobidi.

Marehemu Profesa Haroub Othman aliwahi kusema kuwa ule mtandao wa CCM mwaka 2005 ulikuwa wa kihistoria lakini wahusika hawakujua nini cha kufanya mara baada ya kumweka mtu wao katika madaraka ya urais.

Kwa mujibu wa Profesa Othman, wanamtandao walileta mapinduzi ambayo katika Afrika hayakuwahi kutokea. Kwamba walijipanga vema kumwinua mgombea wao, wakamnadi kwa udi na uvumba na wakafanikiwa kumpeleka Ikulu. Lakini baada ya hapo wakaanza kugawana fito!

Kama mtandao ule ungekuwa na fikra pevu, leo hii Tanzania isingekuwa nchi ya kulia na matatizo haya yanayotukabili kama vile mgao wa umeme, shida ya maji, mfumko wa bei na mengi yafananayo na hayo.

Lakini tumefika hapa kwa sababu ya vurugu za wao kwa wao. Hawakujipanga kuleta mageuzi ya kudumu. Kila mmoja aliingia na lake jambo. Ulikuwa kama mchezo wa kuviziana.

Inashangaza sana leo mmoja wa wanachama anakemea vurugu na kuhimiza majadiliano kwa ajili ya maelewano halafu mtendaji wa chama anaibuka kusema kuwa CCM haihusiki na vurugu na kwamba hakuna haja ya majadiliano. Hili ni la kustaajabisha.

Hamkani tena kwamba ndani ya CCM leo hii, hakuna wa kumwamini mwenzake. Kila mmoja anakwenda kwa hadhari kubwa kwani hajui mwenzake ana silaha gani. Chai hainyweki kama zamani kwa sababu hujui mwenzako ana jambo gani moyoni.

Salamu sasa ni za mdomoni na wala si za kutoka rohoni kama enzi za Mwalimu Nyerere na Rashid Kawawa. Leo hii, CCM wanaogopana, wanaviziana. Kwa mtindo huo chama hakiwezi kufika mbali.

Narejea kusema kuwa huu ni utabiri wangu kwamba anguko la CCM haliko mbali. Siku za CCM kuitwa chama cha Upinzani ziko jirani ni suala la kusubiri tu.

Nihitimishe makala yangu kwa kuwatakia kila jema katika mwaka mpya wa 2011.

munyuku@gmail.com

No comments: