Na Innocent Munyuku
WAMAKONDE wana msemo: “Chimfaa munu amaa mwene.” Kwa Kiswahili unaweza kusema kuwa ‘Kimfaacho mtu anajua mwenyewe mhusika.’
Kwamba usishangae mwanamume mwembamba kupenda mwanamke mnene au mwanamke mrefu akapenda mwanamume mfupi. Au mwingine akapendelea kula maharage mara kwa mara na kuacha kula nyama licha ya kuwa ana fedha za kutosheleza kitoweo. Hayo yote ni matakwa na ridhaa ya mhusika.
Uchaguzi Mkuu kwa mwaka huu umeshamalizika tangu Oktoba 31 na tayari Rais Jakaya Kikwete yupo Ikulu kutimiza kiapo cha kuwatumikia wananchi. Hali kadhalika wabunge na madiwani nao wameshajulikana.
Wakati wa kampeni, kila mgombea alikuwa akinadi sera zake kwa mgongo wa chama chake cha siasa. Wananchi wakasilikiliza kwa makini na hatimaye kufanya uamuzi wa nani apigiwe kura za NDIYO.
Walipokuwa majukwaani kueleza sera zao na kuomba kura, wapigakura kila mmoja kwa wakati wake alikuwa na chaguo binafsi. Kwamba kila aliyepiga kura naamini wengi wao lilikuwa suala binafsi.
Sidhani kama kuna aliyepigwa kura kwa shinikizo bali kwa ridhaa kwani aliamini kuwa mgombea atakayefaa kumwongoza ni fulani na hapo ndipo unapogota kwenye msemo kwamba kimfaacho mtu anajua mhusika mwenyewe.
Leo hii ukiwauliza wapigakura hao matarajio yao kwa mbunge watakupa mambo tofauti tofauti lakini hoja zao zote zitasimama katika lugha moja tu yaani maendeleo katika jamii husika.
Naam! Maendeleo kwani ndicho hasa kilichowasukuma wengi wakaamua kumpa mgombea fulani kura za NDIYO naye akapata kuwa mwakilishi wa jimbo kule bungeni.
Pamoja na ukweli kwamba kuna zumari lilipigwa kuhusu udini na ukabila, sidhani kama wagombea wengi walioibuka kidedea wanazama katika dimbwi hilo la kipuuzi. Ninachoamini ni kuwa wapigakura wengi waliamua kumpa fulani nafasi ya kuwa mbunge kutokana na sera zake.
Kama kuna waliompa kura mgombea kwa kigezo cha udini au ukabila hao ni mabahau. Mabahau wakati mwingine huitwa mazuzu. Kwa ujumla ni aina ya watu ambao ni sawa na majuha.
Mwishoni mwa Novemba mwaka huu, Rais Kikwete alitangaza Baraza la Mawaziri. Kabla ya kutangazwa kwa baraza hilo, kama ilivyo kawaida, wananchi wa kada mbalimbali walikuwa wakisubiri kwa hamu muundo wa baraza hilo jipya kwa maana ya nani atakuwa wapi.
Baadhi ya wabunge na mawaziri wa zamani wakawa tumbo joto kwani hawakujua hatima yao katika baraza lijalo. Hatimaye Rais Kikwete akavunja ukimya na kuyaweka hadharani majina ya mawaziri wake.
Baada ya baraza jipya kujulikana, mitaani kuna minong’ono kwamba baadhi ya wabunge hawajaridhika kwani walikuwa na matarajio makubwa ya kuwa miongoni mwa baraza jipya la Kikwete. Mbali na baadhi ya wabunge kusononekea mafichoni, wapo wapambe wao wanaoamini kuwa ‘mtu wao’ kafanyiwa hila!
Hili ni la kushangaza sana. Binafsi nashangaa hadi kuhisi kuchefuka. Nashangaa kwa sababu mbunge huyo au wabunge hawa walipokuwa wanapanda jukwaani kuomba kura sikupata kumsikia au kuwasikia wakiomba kura za kuwa mawaziri.
Walipanda jukwaani kuomba ridhaa ya kwenda kuwa wawakilishi kule bungeni ‘mjengoni’ mjini Dodoma. Kwanini basi leo hii msononeke kwa kutokuwamo katika Baraza la Mawaziri?
Mlikuja majimboni kwa unyenyekevu mkamwaga sera tamu za kuinua maendeleo ya wananchi. Mkapigiwa kura na baadhi yenu mmepita kwenye tundu la sindano. Leo hii mnaanza kulalamika kwa kukosa uwaziri. Je, huu si ndio uwendawazimu?
Ndiyo maana nikaona ni heri nitumie nafasi kuwatwanga swali kwamba hivi mlikuja majimboni kuomba kuwa wabunge au mawaziri?
Kama mlikuja kuomba kura za kuwa wabunge kwa maana ya wawakilishi wetu katika Bunge, basi timizeni majukumu yenu kwa mujibu wa makubaliano na wapigakura.
Makubaliano hayo ni mkataba au kitanzi chenu. Kwamba hakikisheni mnatimiza ahadi zenu. Kama uliahidi kumalizia ujenzi wa daraja fanya hivyo. Chakarika, tafuta fedha ziliko timiza ahadi yako.
Utakuwa mwakilishi wa ajabu sana kama utaendelea kulalama kwamba Rais Kikwete kakutenga. Ulikuja jimboni kuwa mbunge na wala hakuna siku ulitamka kuutaka uwaziri.
Tanzania yetu hii, kama nilivyosema katika safu hii juma lililopita, ni nchi tajiri lakini mbali na kuachwa huru na Waingereza mwaka 1961, taifa limekuwa likididimia. Kisa? Watendaji wakuu hawana uzalendo.
Mtu haoni soni kuingia mkataba mbovu ambao kesho yake unaliumiza taifa. Si mara moja au mbili tumesikia kuwa ‘mkubwa’ fulani katumia vibaya fedha za wafadhili ambazo kimsingi zililenga kuleta maendeleo kwa jamii.
Angalia leo hii matumizi makubwa serikalini. Walau Waziri Mkuu Mizengo Pinda anaonyesha njia. Ameshakataa kupewa gari jipya lenye thamani zaidi ya Sh milioni 200. Huyu ana moyo wa kizalendo.
Lengo langu ni kuonyesha kuwa kama kuna mbunge leo hii analalama kuachwa kwenye Baraza la Mawaziri, maana yake ni kwamba huyo hana nia ya dhati ya kuwatumikia wananchi. Huyo kwa vijana wa mjini ataitwa ‘mpiga dili’.
Kiongozi wa aina hiyo ambaye haguswi na umasikini wa watu wake na badala yake kuota ndoto za kuwa waziri ni wa kuogopwa. Naapa miaka mitano si mingi itafika siku naye ataliangalia Bunge kwenye video.
Nihitimishe kwa kusema kuwa huu si muda wa kulilia uwaziri, tenda uliyowaahidi wananchi kule jimboni kwako na huo ndio uungwana kwani hata wa kale walisema muungwana kwake ni vitendo. Timizeni ahadi.
munyuku@gmail.com
0754 471 920
Wednesday, December 29, 2010
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment