Na Innocent Munyuku
BIBLIA Takatifu katika kitabu chake cha Waebrania mwanzoni kabisa inatoa maana ya neno ‘imani’. Kwamba imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana.
Katika Waebrania 11: 3 imeandikwa kuwa kwa imani twafahamu ya kuwa ulimwengu uliumbwa kwa neno la Mungu, hata vitu vinavyoonekana havikufanywa kwa vitu vilivyo dhahiri.
Kwa jumla sura yote ya 11 katika kitabu hicho cha Waebrania inaelezea imani ilivyofanya kazi kwa watumishi tele wa Mungu kama vile Nuhu, Henoko, Ibrahimu, Sara, Yakobo na Musa.
Aghalabu binadamu wengi kama si wote tuna imani na jambo fulani katika maisha yetu ya kila siku. Ndiyo maana pahala pengine husemwa kuwa imani inaweza kuhamisha milima.
Suala la imani wakati mwingine ni gumu sana. Kwa mfano, si rahisi kwangu binafsi kuniaminisha dini nyingine tofauti na ninayoiamini. Itamchukua mtu muda mrefu kunishawishi ili niingie katika kundi lake. Haya ni matokeo ya imani.
Binafsi naamini kwamba dunia na vyote vilivyomo vimeumbwa na Mwenyezi Mungu. Hata hivyo, wapo wengine hawaamini hivyo.
Hapo juu nimedokeza kuwa ni vigumu kwa mmoja kumshawishi mwingine kuamini anachokiamini yeye. Hilo ni jambo gumu na hushauriwa pia kuwa si busara kuingilia imani za watu wengine.
Hata hivyo, katika makala yangu haya leo naomba kuingilia imani za wengine si kwa shari bali kwa lengo la kujenga umoja na misingi bora ya maendeleo.
Katika miaka ya hivi karibuni, kumeibuka makanisa mbalimbali nchini. Kuibuka kwa makanisa hayo kumeibua pia watu wanaojipachika kuwa ni ‘manabii’, ‘maaskofu’, ‘mitume’ na ‘wachungaji’. Idadi yao ni kubwa na inaendelea kupanuka kila leo.
Mafundisho katika makanisa hayo, baadhi yanajenga na mengine yanabomoa ujenzi wa jamii huru ya Tanzania. Yapo makanisa yanayowalazimisha waumini wake kutoa sadaka au zaka kwa kiwango fulani cha fedha ili wabarikiwe na Mungu. Haya yanatendeka!
Mafundisho kama haya sidhani kama yanalenga kumwinua muumini huyo kutoka katika lindi la umasikini. Badala ya kuwekeza unatoa kila kilicho chako na kulala njaa kwa imani kwamba utashushiwa baraka kutoka juu.
Wengi wao pia wameacha kufanya kazi viwandani, ofisini na kazi nyinginezo za kujiingizia kipato na badala yake wameamua kushinda makanisani wakiamini kwamba kuna miujiza itashuka.
Naomba kusema kwamba tabia ya aina hii si ya kufumbiwa macho na kwa upande mwingine kuna haja kwa mamlaka za juu serikalini kuangalia mienendo ya makanisa haya.
Kuyafumbia macho ni hatari kubwa kwa taifa la Tanzania. Si ajabu siku moja yakatokea ya nabii wa uongo, Joseph Kibwetere wa Uganda ambaye kwa sasa ni marehemu.
Kibwetere aliitingisha Uganda mapema miaka ya 1990 baada ya kudai kuwa alikuwa akitokewa na Bikira Maria. Kibwetere kwa ushawishi mkubwa pamoja na Credonia Mwerinde wakaunda kanisa kubwa lililovuta watu wengi. Baadaye wakatangaza kuwa mwaka 2000 ulikuwa mwisho wa dunia. Kilichotokea ni kwamba mamia ya waumini hao waliangamizwa wakiwa katika kile kilichoitwa kuwa ni ibada takatifu.
Tukio hilo lililotokea Machi 17 mwaka 2000 katika Kijiji cha Kanungu nchini Uganda lilileta mpasuko wa roho kwa watu wengi.
Ninachojaribu kusema ni kwamba wimbi hili la kuibuka kwa makanisa linadhibitiwa vipi? Je, Serikali inafuatilia kwa makini mafundisho ya makanisa hayo? Hata kama Serikali haina dini, nadhani upo lazima wa kuweka udhibiti ili jamii ya wazalishaji isipungue.
Binafsi napata shaka kidogo ninapowaza kuibuka kwa mambo kama haya. Sisemi kwamba watu wasisali. La hasha! Ninachosema ni kwamba kuwe na mpango maalumu wa kufuatilia mafundisho na mienendo ya hao wanaojiita manabii.
Mfano hai, jijini Dar es Salaam, yupo kijana mmoja anayejiita ‘Nabii Tito’ anapita mitaani hasa sehemu zenye baa akihubiri na Biblia yake mkononi. Mafundisho anayoyatoa ni ya upotoshaji kabisa.
Kwa mfano hasiti kusema kuwa mwanamume sharti awe na wanawake wengi na kwamba wakati wa kujamiiana asitumie kondomu. Pia anahamasisha unywaji wa pombe kupita kiasi na uvutaji wa sigara. Je, mtu wa aina hii kwanini anaachwa akitamba na mafundisho ya kihuni namna hii?
Leo hii, Yesu amegeuzwa kuwa kitega uchumi. Mtu mmoja anaibuka asubuhi na kujitangaza kuwa ni ‘nabii’ na kisha kuwatia hofu waumini wao. Waumini hao wataacha kujenga familia zao na kukimbilia kujenga familia ya ‘nabii’.
Waumini hao kwa vile wameamua kuachana na kazi za kusaidia familia zao, wamebaki kama makinda ya ndege wakisubiri miujiza kutoka kwa Mungu. Imani ya aina hii ni hatari kwa ujenzi wa taifa letu.
Michango tele makanisani, njaa kali huko nyumbani. Huo ndio utamaduni wa sasa. Nadhani huu ni wakati wa mabadiliko. Tusiache Watanzania wakiyumbishwa katika imani ambazo mwishowe zitaligharimu taifa. Huu ndio mtazamo wangu.
munyuku@gmail.com
Wednesday, December 29, 2010
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment