Wednesday, January 19, 2011

Damu ya CHADEMA haitakwenda bure

Na Innocent Munyuku

WIKI mbili zilizopita katika safu ya Mpembuzi Yakinifu ya gazeti hili niliandika makala yenye kichwa cha habari: ‘Anguko la CCM haliko mbali.’

Wenye chama chao wakapiga simu na wengine kutuma ujumbe wakisema kuwa utabiri wangu si lolote na kwamba eti nilikuwa nimetumwa na Upinzani.

Niliishia kucheka kwa kebehi kwa sababu walionikejeli hawakuwa na hoja za msingi na wala hawakukaribia kuwa na ubavu wa kujenga ukuta imara wa mapambano ya hoja. Nadiriki kusema kuwa hata baadhi yao naamini wameishia kula wa chuya baada ya uchaguzi mkuu kumalizika.

Hao wamebaki na fulana na kofia za kampeni huku wakiwa hawana la maana la kujivunia katika kujenga ustawi wa jamii yao. Sana sana watakuwa wanasubiri uchaguzi mwingine wapate wasaa wa kula na kunywa wakati wa kampeni. Baada ya hapo dhiki inabaki pale pale. Wamekuwa kama manahodha waliokula kiapo cha kuzama na meli inayokwenda mrama!

Wiki iliyopita, Tanzania imeshuhudia ukatili wa kutisha kutoka kwa Jeshi la Polisi nchini. Polisi bila huruma waliamua kumwaga damu baada ya kuyasambaratisha maandamano ya CHADEMA mjini Arusha.

Kabla ya kufanyika kwa maandamano yale, kulikuwa na majibizano baina ya polisi na viongozi waandamizi wa CHADEMA. Polisi kwa upande wake ilitangaza kutoyakubali huku CHADEMA wakisema kuwa lazima yatafanyika.

Kimsingi maandamano yale yalikuwa ya amani na kwa kuashiria hilo, siku ya tukio waandamanaji walivaa vitambaa vyeupe kuashiria kutokuwapo na mpango wa hamaki katika maandamano yale.

Binafsi niliamini kwamba walichotakiwa kufanya polisi siku ile ni kuyalinda maandamano yale na si kuwavamia waandamanaji na kuwafyatulia risasi na mabomu. Watu watatu wameripotiwa kupoteza maisha kutokana na kupigwa risasi na polisi siku hiyo. Wengine pia wamejeruhiwa vibaya.

Mkuu wa kaya, Rais Jakaya Kikwete ametoa kauli kwamba jambo kama lile kamwe halitarudiwa ndani ya ardhi hii. Alitoa kauli hiyo wakati akila mapochopocho na mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini katika hafla ya kuukaribisha mwaka mpya pale Jumba Jeupe, Ikulu ya Dar es Salaam eneo la Magogoni, Januari 7, mwaka huu.

Yaliyotokea Arusha ni ya kusikitisha na kwa mtazamo wangu, damu ya watu wale kamwe haitakwenda bure. Mungu yu pamoja nao ni suala la kusubiri tu.

Siku mbili kabla ya maandamano yale, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Said Mwema aliwaambia waandishi wa habari kwamba jeshi lake lilishapata taarifa za kiintelijinsia kwamba kungekuwa na hali ya kutokuwapo kwa amani.

Kwa maoni yangu, taarifa ile ya IGP haikuwa na uhakika wa kutokea kwa vurugu zozote kutoka kwa wafuasi wa CHADEMA. Kinyume chake, polisi ndio waliokuwa chanzo cha vurugu hadi kumwaga damu za raia wasio na hatia.

Nani alianza vurugu kama si polisi waliodiriki kuwabughudhi waandamanaji? Kwani polisi walihisi jambo gani baya kutokana na maandamano yale ambayo yangehitimishwa na mkutano wa hadhara?

Walichofanya polisi ni kufuata maisha ya mbuni ambaye kwa kawaida huficha kichwa chake na kuacha mwili mzima ukiwa nje. Kuyavuruga maandamano ya CHADEMA si dawa ya kuyazuia mawazo ya watu katika ulimwengu huu wa uwazi na ukweli. Ukweli sasa uko wazi na kwa haraka haraka naweza kusema kuwa polisi imeumbuka!

Bado natafakari kauli ya IGP kwamba kulikuwa na taarifa za kiintelijinsia. Matukio mangapi ya ajabu ya kihalifu yanatokea nchini bila wao (polisi) kuwa na taarifa sahihi? Nijuavyo mimi mtu akisema ana taarifa za kiintelijinsia ni kwamba kwa asilimia zaidi ya 70 ana uhakika na taarifa hizo. Hili la Arusha kweli lilikuwa na taarifa sahihi kwamba kungekuwa na fujo kutoka kwa waandamanaji? Jibu wanalo makachero.

Hatuwezi kuendesha nchi kwa staili hii. Huu ni ukandamizwaji wa demokrasia. Tanzania sasa huko ughaibuni haitajwi tena kuwa nchi ya amani. Sikiliza redio na televisheni za kimataifa utayasikia haya. Soma magazeti mbalimbali na mitandao ya intaneti haya yote yamo. Wanachosema wenzetu ni kwamba hapa si pahala pa kupakimbilia bali pa kupakimbia.

Zipo taarifa kuwa mji wa Arusha ambao ni maarufu kwa biashara ya utalii, kwa sasa hali ni tete. Watalii wanasita kuingia kwa sababu wangali na shaka ya vurugu. Tanzania aliyotuachia Mwalimu Nyerere inakwenda wapi?

Kuna chombo kimoja cha habari kimenikera katika moja ya taarifa zake kwa umma. Mwandishi wa chombo hicho anasema eti kulikuwa na mapambano baina ya polisi na waandamanaji wa CHADEMA. Yale hayakuwa mapambano bali, polisi walikuwa wakiwasulubu waandamanaji.

Angalia mabavu yaliyotumika na polisi kwa kuvunja vioo vya magari. Ile ni busara ya aina gani? Hivi hawa kweli ni polisi wenye mafunzo timamu? Nani mwalimu wao? Hawa ndio polisi wetu.

Nakumbuka zaidi ya miaka 10 nyuma nilikuwa mjini Mbeya kuripoti shindano la Miss Kanda za Juu Kusini. Baada ya kumalizika kwa shindano hilo nikaanza safari ya kurejea hotelini nilikofikia eneo la Uhindini. Ilikuwa imetimia saa saba usiku. Nilikodi taksi na nilipofika jirani na hoteli nikamwamuru dereva asimamishe gari kwa maelezo kwamba ningeweza kutembea kwani zilibaki kama mita 200 hivi.

Wakati natembea nikakutana na polisi waliokuwa kwenye lindo katika Benki ya NBC. Wakaniamuru nisimame na kisha nikae chini. Nilipohoji kulikoni, mmoja wao akasema anaomba bangi.

Nilishangaa sana, polisi huyu ni wa aina gani? Anamsimamisha raia bila kumhoji, wala kuomba utambulisho badala yake anaomba bangi? Nilikerwa na kitendo kile. Nikatoa kitambulisho (Press Card) na kuwapa. Wakaishia kunitaka radhi nikajiondokea huku nikiwa nimeghadhibika. Hawa ndio polisi wetu.

Siku nyingine nikiwa natoka kupata ‘moja moto, moja baridi’ nilisimamishwa na polisi usiku wa saa nne. Tukio hili ni la jijini Dar es Salaam. Wakaniuliza natoka wapi na naelekea wapi. Nikajieleza kwa ufasaha. Wakataka niwape kitu kidogo. Nikawauliza kwa kazi ipi? Mkononi nilikuwa nimeshikilia bia ya kopo ambayo tayari nilishaanza kuinywa. Bila aibu polisi mmoja akasema kwa vile nimeshindwa kuwapa fedha basi nimpe ile bia ainywe. Nilidhani ni dhihaka. Akaidaka kweli akainywa!

Nimetoa mifano hiyo kuonyesha namna baadhi ya polisi wanavyotakiwa kujengewa misingi imara ya kuheshimu kazi zao. Baadhi ya polisi hawastahili kuwamo kwani wanalitia fedheha jeshi. Utumiaji wa nguvu au ubabe, vitisho kupita kiasi sidhani kama ni tija.

Nahitimisha makala yangu kwa kusema kuwa nayaona mabadiliko makubwa yakija mbele ya Watanzania. Naiona Tanzania huru mbele yangu. Tanzania ambayo haitakuwa na uendawazimu kutoka kwa watu waliolewa madaraka. Inawezekana sitaiona siku hiyo, lakini vizazi ambavyo hata majina yao siyajui watafurahia uhuru wa kweli ndani ya ardhi hii tuliyopewa na Mwenyezi Mungu.

Wasalaam,
munyuku@gmail.com
0754 471 920

No comments: