Na Innocent Munyuku
HUSEMWA kwamba usipoziba ufa utajenga ukuta. Lakini wajuzi wengine wa lugha wakaja na msemo mwingine kwamba samaki mkunje angali mbichi.
Wapo wengine waliosema pia kuwa tohara ya Ijumaa huanza Alhamisi. Hii yote ni misemo ya hadhari kwa binadamu awe na hulka ya maandalizi.
Kwamba kama wahusika wa jambo wanafanya mambo pasipo maandalizi ni wazi kuwa suala walifanyalo halitakwenda sawia. Watavurunda na hivyo kuonekana waliokosa umakini.
Jamii yetu leo hii inahaha kufuta wimbi la watoto wa mitaani. Semina na warsha mbalimbali zinajadili suala hilo.
Sehemu za mijini watoto hao ni wengi. Tunapishana nao na la kusikitisha ni kwamba haieleweki ni nani anawajali watoto hao kwa dhati.
Wataambulia Sh 100 au Sh 500 ambazo kwa mtazamo wa kawaida haziwasaidii kuishi kwa uhakika.
Hii ni kusema kwamba maisha ya watoto hawa ni ya shibe ya leo. Wakiumwa na washindwe kujipanga mitaani kusaka fedha kutoka kwa raia wenye huruma basi hakuna shaka kwamba siku hiyo ni kama kiama kwao.
Zipo asasi zilizojiandikisha kuwa mstari wa mbele kuwatumikia watoto hao. Vipo vituo vinavyolea watoto hao wa mitaani lakini ukweli wa mambo ni kwamba mahitaji hayatoshelezi.
Hii ni kusema kuwa watoto waliopo vituoni ni wachache ukilinganisha na ujumla wa waliobaki kuzurura mitaani.
Lakini hoja yangu ni kwamba mtima wangu umejaa shaka juu ya mustakabali wa watoto hao ambao wengi wao ni wenye umri wa miaka kati ya miwili hadi 15.
Hawa wanaendelea kuomba lakini wakishavuka umri huo ‘wanajiajiri’ katika kazi nyingine. Katika miji mbalimbali nchini watoto hao wakishakomaa hujihusisha na kuosha magari ili wapate kuishi.
Wakati mwingine watoto wa aina hiyo hugeuka kuwa ‘walinzi’ wa muda wa magari hayo ingawa uzoefu unaonyesha ni hao hao wanaokwapua vioo vya magari au vipuri.
Kwa mtazamo wangu, hatua ya aina hiyo ni mbaya kwani wakishaanza kukwapua vipuri wataenda mbali zaidi kwa kujifunza uhalifu uliokomaa.
Hawana nafasi kwa elimu ambayo kwa hali ya kawaida ingewasaidia kusaka namna nyingine ya kuishi.
Kwa maana hiyo wataelekeza akili zao kutenda uhalifu zaidi kuliko wema ndani ya jamii.
Watafanya hivyo kutokana na ukweli kwamba hawana namna nyingine ya kujiingizia kipato. Wataosha magari na mwishowe watachoka.
Na ukizingatia kuwa watoto hao wako mjini ni wazi kuwa wanaishi katika mazingira ya kujifunza mbinu mbalimbali za kuyasukuma maisha.
Hawa sasa ndio hao ambao kwa mtazamo wangu sisiti kuwaita watu wazima wa mitaani.
Kwamba athari zake ni kubwa kuliko pengine sehemu kubwa ya jamii inavyofikiria. Madhara yake ni makubwa na hii maana yake ni kuwa tutakuwa na jamii yenye shaka daima.
Nani ataweza kuwadhibiti watu wazima hao wa mitaani ambao katika maisha yao ya awali wamekuwa katika dhiki na kukata tamaa?
Mamlaka gani inaweza kusimama na kujigamba kwamba inayo ubavu wa kuwadhibiti watu wazima hao wa mitaani?
Ukweli wa mambo ni kwamba tusitarajie kuwaona wakiwa na mema katika maisha kwani tayari wameshaathirika na mfumo wa maisha.
Mtu aliyeishi kwa mashaka katika miaka mingi si ajabu akawa na uamuzi wa kubomoa zaidi kuliko kuijenga jamii. Hebu fikiria tangu akiwa na umri wa miaka miwili anaishi mtaani unadhani akiendelea hivyo hadi miaka 25 atakuwa katika hali gani?
Hakuna shaka kwamba atajifunza njia mbadala ya kujikwamua na ugumu wa maisha na katika hili hatasita kujifunza njia yoyote atakayoona inafaa. Atafanya hivyo kwa sababu hana cha kupoteza.
Tusifikishane huko kwani jamii ya Watanzania inao uwezo wa kuwanusuru watoto wa mitaani. Tusisubiri waitwe watu wazima wa mitaani.
Tuesday, December 4, 2007
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment