Monday, December 17, 2007

Panya wengi hawachimbi shimo

na innocent munyuku

SIKU za maumivu zimeanza. Pilika zimezidi, watu wanakuna vichwa wakihaha kusaka neema ya matumbo na viwalo vya sikukuu.

Mzee wa Busati ni miongoni mwao. Kaya yake imemkodolea macho. Hana namna ya kukwepa kwani husemwa kwamba tembo hawezi kuona uzito wa mkonga wake. Kikombe hiki kitanywewa!

Kila mmoja kwa nafasi yake anajipanga ili mambo yasiende upogo. Nidhamu ya matumizi ya fedha imekuwa juu. Bajeti imeshapangwa na kinachosubiriwa ni siku zifike watu watafune vipapatio vya kuku kama si kwato za mbuzi.

Vibaka nao wanakwenda na wakati, mbinu zimekuwa za kisasa zaidi katika wizi wanaoufanya. Kwao hiyo ni ajira ingawa si halali. Lakini wafanyeje? Ndio staili yao ya maisha. Watakimbilia wapi? acha waendelee hadi siku wakikumbana na harufu ya moto wa petroli.

Hayo ndiyo mambo ya kila siku ukianza kuyafuatilia unaweza kuongeza uchizi, la maana ni kuyaacha yapite.

Huo ulikuwa utangulizi wa Mwandika Busati ambaye wiki hii katua kwenye safu yake ya kujidai akiwa na nguvu mpya. Mola kamwongezea misuli.

Lililo kuu juma hili ni suala la usukaji wa vipaji vya sanaa nchini. Wakati mwingine inashangaza kuona kwamba wapo watu kwa makusudi wameamua kupotosha vichwa vya sanaa.

Hao ni hodari wa kubuni mambo na kwa vile wako kwenye ardhi ya Wadanganyika, wanachokibuni na kukisema huonekana kuwa ni bora na chenye mwelekeo.

Mzee wa Busati angali akishangaa programu iliyoitwa ya kusaka vipaji vya muziki Tanzania. Hivi kweli nyota wa muziki anasakwa kwa staili hiyo? Huko ni kupotoka kwa kiwango cha hali ya juu.

Nyota wa muziki anapatikana kwa kumwangalia usoni? Ni lini mwanamuziki nyota akapimwa kwa umbo lake?

Ni lini nyota njema ya muziki ilipimwa kwa majaji ambao baadhi yao hawaujui huo muziki? Hivi ni vichekesho ambavyo kwa hakika vinaleta kichefuchefu cha kufungia mwaka.

Leo mwataka kuwa na kizazi kitakachowika kwenye anga ya muziki ndani na nje ya Tanzania. kwa mtindo huo wa kuangaliana usoni kama mpo kwenye gwaride la utambuzi wa wahalifu.

Wajuzi wa Kiswahili husema kwamba panya wengi hawachimbi shimo. Wanachomaanisha ni kuwa uwingi si hoja katika utekelezaji wa mambo muhimu.

Hao wanaojipanga kwa wingi wakinadi kusaka vipaji vya muziki nchini bila shaka ni wapotoshaji kutokana na ukweli kwamba staili inayotumika kuwasaka nyota wa muziki inakwenda isivyo.

Matokeo yake ni kwamba taifa lazidi kupoteza vipaji vya muziki kila uchao. Waandaaji wa shughuli kama hizo wengi wao wamekaa kwa ajili ya neema binafsi na si kweli kwamba wana mema kwa muziki wa Tanzania.

Matatizo ya aina hiyo ni mengi na ndio maana asilimia kubwa ya Wabongo wamesusa mema ya kwao.
Anachosema Mzee wa Busati ni kuwa wasanii wetu hasa wa muziki hawasaidiwi katika kuendesha maisha yao kwa thamani halisi ya kazi zao.

Leo hii Mwandika Busati angetaraji kuona mashabiki wa muziki wamevaa fulana zenye nembo za wanamuziki kama Msafiri Zawose au Vitali Maembe.

Hazipo mtaani kwani hata chache zinazochapwa zinasuswa na maelfu kukimbilia fulana na kofia za 50 Cent.

Hayo yote yanakuja kutokana na namna jamii ilivyojengwa kuanzia huko nyuma. Na ndio maana Mzee wa Busati anasema staili ya kusaka vipaji vya muziki iangaliwe upya.

Hizi kelele zinazopigwa na kuchezwa na wengi wakiamini kwamba kuna vipaji vinasakwa ni kudanganyana na ni kupotosha sanaa.

Huu ni ukomo wa Mzee wa Busati kwa wiki hii. Panapo majaliwa tukutane wiki ijayo kwenye Noeli. Kila lililo jema liwakute na fanaka tele.

Wasalaam,

No comments: