Na Innocent Munyuku
NIPATAPO nafasi ya kuketi vijiweni na Watanzania wenzangu hasa vijana nanasa mambo mengi ambayo natamani mtawala wa nchi pia angepata wasaa wa kuyasikia.
Bila shaka anayapata lakini kwa vile sina uhakika ni heri nitumie nafasi hii kuyasema baadhi ya masuala yanayojadiliwa kila wakati huko mitaani.
Leo hii Watanzania wanatimiza miaka 46 tangu wapate uhuru kutoka mikononi mwa Waingereza mwaka 1961. Ni sherehe kubwa na yenye simulizi nyingi; mbaya na njema.
Miaka 46 ya uhuru si lele mama. Hii maana yake ni kwamba kama ni maisha ya binadamu Tanzania tayari ni mtu mzima anayejitegemea kwa mambo mengi.
Lakini kwa bahati mbaya sana miaka hii ya uhuru ni dhahiri kwamba hakuna jema la kujivunia ukilinganisha na mataifa mengine yaliyopata uhuru baada ya Tanzania.
Kinachosemwa mitaani ni kwamba Tanzania licha ya kuwa taifa huru, maisha ya Watanzania yameendelea kuwa magumu kila uchao.
Watu wanalalama juu ya kupanda kwa bei ya bidhaa hasa zile zinazohitajika katika maisha ya kila siku. Hicho ndicho wanacholalamikia.
Lakini pia wanasema juu ya uwajibikaji mdogo wa watendaji wa Serikali. Wanazungumzia ubovu wa baadhi ya mawaziri, wakuu wa mikoa na wilaya.
Ingawa wengi wao hawana ubavu wa kupaza sauti, wanasema kwa kadiri wawezavyo kwamba hata watendaji katika ngazi ya vijiji ni waovu wasiopaswa kukalia viti hivyo.
Hawaishii hapo, wanakerwa juu ya ubovu wa huduma za afya. Kina mama na watoto, wazee na wahitaji wengine wa huduma hiyo wanakwazwa na utendaji wa wauguzi na madaktari.
Hili pengine halihitaji mjadala mrefu kwani hospitali na zahanati nyingi mambo si shwari kwa wagonjwa. Ni jambo la kawaida kwa wagonjwa kulala wanne kitanda kimoja. Hili si la ajabu.
Si jambo geni pia kuwakuta wagonjwa wamerundikana chini wakilalia mkeka. Watanzania wamezoea. Si kama wameridhika bali mfumo umewaweka hapo.
Muhuri wa Mtendaji wa Serikali za Mitaa nao siku hizi umekuwa mradi mkubwa kwa hao wenye dhamana ya kuushika. Karatasi haigongwi pasipo rupia mkononi.
Wananchi wamezoea kulipa fedha hata kwa yale ambayo wanapaswa wahudumiwe bure. Yanaonekana kama vile yameshakuwa sugu na yasiyoweza kufutwa.
Hayo ndiyo yanayojiri katika miaka hii 46 ya uhuru wa Tanganyika. Rushwa imeendelea na inazidi kushika kasi ya ajabu kutokana na ukweli kwamba mbinu za utoaji na upokeaji rushwa zinabadilika.
Watu wanakwenda kwa mtindo wa kisasa na kutokana na hali hiyo si rahisi leo hii kuwanasa wala rushwa kama ilivyokuwa miaka 10 iliyopita. Mbinu zinabadilika.
Pamoja na ukweli kwamba wananchi wana mchango mkubwa katika kukabiliana na rushwa, wanacholalamikia wao ni kwamba walio juu ndio viongozi wa jambo hilo.
Wanasema kama katibu mkuu wa wizara anadaka rushwa mwananchi wa kawaida afanyeje? Tule wote kwani huo ndio utaratibu uliopo.
Wengine wananong’ona kwamba kama mbunge fulani katinga bungeni kwa njia ya hongo diwani naye ataachaje kutetea nafasi yake kwa rushwa?
Haya si mambo ya siri yanasemwa lakini kwa bahati mbaya sana si rahisi kuyapatia ushahidi. Lakini ukweli wa mambo ni huo rushwa inanuka nchini.
Hii maana yake ni kwamba walio wengi hawapati huduma kwa kiwango kinachostahili. Kama ni ajira, matibabu na mengine hayapatikani mpaka utoe rushwa.
Ukikanyaga polisi utaambiwa hawana karatasi ya kuandikia maelezo ya mlalamikaji. Lakini kabla ya hilo kama utakuwa unahitaji kuwapeleka mahala alipo mtuhumiwa utaelezwa kwamba hawana gari na kama lipo watasema halina mafuta. Kodi tunazolipa zinatumikaje?
Hizo zote ni njia za kukufanya uwe mstari wa mbele kufungua pochi na kuwapa ulichonacho ili mambo yaende.
Hii ndiyo miaka 46 ya uhuru wa Tanganyika tunayoishi. Kwa uwazi ni kwamba maisha ya rushwa hayana maana nyingine zaidi ya kuendelea kukandamizana na kwa njia hiyo kuliangamiza taifa.
Kuna waliodiriki kusaini mikataba hafifu ya kimataifa ambayo leo hii taifa linaangamia kwa kukosa maarifa. Waliopewa dhamana wamekula cha kwao na hawana hofu ya maisha.
Anayepata taabu ni mlalahoi ambaye hajui aanzie wapi ili afikie kilele cha maisha bora. Amekwazwa na mfumo ambao hautaki mabadiliko.
Hayo ndiyo yanayosemwa vijiweni lakini hakuna shaka kwamba ndiyo hali halisi kwa maisha ya kila siku.
Je, katika miaka 46 ya uhuru Watanzania tunajivunia nini? Imani na utulivu wa kutoona mabomu yakilipuka mitaani? Pengine yapaswa kuwapo na tafakuri ya kina kwani kwa mtazamo wangu amani kamili maana yake ni kuwa na utulivu wa akili pia.
Kama matumbo hayana shibe sidhani kama mtu anaweza kutembea kwa matao akisema kuwa yu na amani ya kweli. Tusibweteke na miaka 46 ya uhuru tusake njia ya kujikwamua uwezo tunao.
Sunday, December 9, 2007
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment