Sunday, December 9, 2007

Hili la Dewji na mustakabali wa soka yetu

na innocent munyuku

NI jambo la kawaida katika mkusanyiko wa binadamu kuwa na mawazo tofauti.

Hii maana yake ni kwamba kama itatokea siku binadamu wote duniani wakafanana mawazo katika kila jambo basi si ajabu dunia ikasambaratika zaidi.

Mzee wa Busati wiki iliyopita alisikia habari kwamba kuna wapenda michezo wametangaza kuipa Kilimanjaro Stars zawadi nono katika mfumo wa fedha kama wataibuka na Kombe la Chalenji.

Alianza Mohamed Dewji kuwatangazia Wabongo kwamba yeye binafsi atawazadia wachezaji donge nono la Sh milioni 35 na Sh milioni 24 kama watashika nafasi ya pili.

Baada ya Dewji kutangaza hilo, mfanyabiashara maarufu nchini Alex Massawe naye akasema atawapa wachezaji Sh milioni 10 kama watafanikiwa kutwaa Kombe la Chalenji.

Wenye busara wakaanza kunong’ona kwamba wawili hao hawakuwa na nia njema ya kuifanya Kilimanjaro Stars kufikia kilele cha mafanikio.

Kwamba kama wamelenga kuifanya Tanzania iwike katika medani ya soka hawakuwa na haja ya kuibuka leo na ahadi kama hizo za danganya toto.

Mzee wa Busati anaamini kuwa kuendekeza ahadi kama hizo ni sawa na kuua medani ya soka nchini. Ni wazi kwamba Shirikisho la Soka Tanzania lina uhaba wa fedha. Dewji analifahamu hilo hali kadhalika Massawe.

Mwandika Busati alitarajia kuwasikia watu hao wakitoa fedha kwa ajili ya maandalizi kabambe na si kuiacha timu dhaifu iingie mashindanoni.

Anachokiona Mzee wa Busati hapa ni porojo na hadaa kwa Watanzania na katika hili wanasoka wamedhihakiwa. Haiingii akili kwa mtu makini na mwenye nia ya dhati ya kuinua soka asubiri timu iingie uwanjani ndipo atoe ahadi ya fedha nono.

Dewji na Massawe walikuwa wapi wakati Kilimanjaro Stars inahitaji fedha za maandalizi? Hivi ni kweli hawakujua kwamba kambi inahitaji fedha kwa ajili ya maandalizi?

Ukweli wa mambo ni kwamba huo ni mfano kwamba Watanzania walio wengi mbali na kuwa na uwezo wa kukuza michezo wanajificha kwa makusudi.

Ahadi kama hizo hazina maana nyingine zaidi ya kudidimiza michezo nchini. Vijana wanatakiwa waandaliwe na kama wamepata maandalizi ya kutosha hawana haja ya kuahidiwa mema kwani watakuwa tayari wana ubavu wa kufanya vema mashindanoni.

Tangu mwanzo Mzee wa Busati ameweka wazi kwamba binadamu lazima watofautiane katika mtazamo. Ndicho anachofanya hapa. Kuna waliokaa na kukenua wakifurahia ahadi hiyo ya fedha. Hiyo ni haki yao ya msingi na wana uhuru wa kufanya hivyo.

Lakini kwa mtazamo wa Mwandika Busati kinachofaa kufanywa kama kweli bongo inahitaji kuvuma katika soka basi ni maandalizi na si kupiga soga.

Kama wana nia ya dhati ya kuinua soka ni heri wajitokeze mapema wakati wa maandalizi kwa timu za taifa. Kutoa ahadi pekee si dawa ya Tanzania kuwa kichwa cha mwendawazimu.

Hii ni sawa na kwenda kwa jirani yako mwenye njaa halafu unamwambia akimbie mbio za nyika na kwamba akishamaliza atazawadia fedha za kujaza mifuko yake.

Hiyo ni hadaa kwani mwenye njaa hawezi kumudu mbio hizo. Ataanguka na kupoteza maisha kwani hana ubavu wa kumaliza mbio hizo.

Kama una mapenzi na jirani huyo basi ni vema ukampa lishe bora na hapo umweleze aanze mbio za nyika. Huo ndio uungwana!

Hizo ngwenje mnazoahidi fanyeni mpango wa kuwaweka wachezaji kambini. Walishwe vema wawe na stamina, wafundwe njia za kisasa katika soka ili wakitinga dimbani waonyeshe makali.

Kukaa mezani na kusema juu ya ahadi si njia mbadala ya kuendeleza soka. Muda wa kubembelezana kwa peremende bila shaka umepitwa na wakati. Badilikeni!

Mzee wa Busati ameona awe tofauti na hao wanaokenua wakichekelea ahadi ya fedha. Kwani naye anao uhuru wa kuwa na msimamo wa tofauti.

Vinginevyo busati kwa sasa halikaliki. Mzee wa Busati yu katika pilika za kila aina ili kulinda heshima ya kaya yake kwa majuma ya raha na karaha yajayo.
Wasalaam,

No comments: