Monday, December 17, 2007

Panya wengi hawachimbi shimo

na innocent munyuku

SIKU za maumivu zimeanza. Pilika zimezidi, watu wanakuna vichwa wakihaha kusaka neema ya matumbo na viwalo vya sikukuu.

Mzee wa Busati ni miongoni mwao. Kaya yake imemkodolea macho. Hana namna ya kukwepa kwani husemwa kwamba tembo hawezi kuona uzito wa mkonga wake. Kikombe hiki kitanywewa!

Kila mmoja kwa nafasi yake anajipanga ili mambo yasiende upogo. Nidhamu ya matumizi ya fedha imekuwa juu. Bajeti imeshapangwa na kinachosubiriwa ni siku zifike watu watafune vipapatio vya kuku kama si kwato za mbuzi.

Vibaka nao wanakwenda na wakati, mbinu zimekuwa za kisasa zaidi katika wizi wanaoufanya. Kwao hiyo ni ajira ingawa si halali. Lakini wafanyeje? Ndio staili yao ya maisha. Watakimbilia wapi? acha waendelee hadi siku wakikumbana na harufu ya moto wa petroli.

Hayo ndiyo mambo ya kila siku ukianza kuyafuatilia unaweza kuongeza uchizi, la maana ni kuyaacha yapite.

Huo ulikuwa utangulizi wa Mwandika Busati ambaye wiki hii katua kwenye safu yake ya kujidai akiwa na nguvu mpya. Mola kamwongezea misuli.

Lililo kuu juma hili ni suala la usukaji wa vipaji vya sanaa nchini. Wakati mwingine inashangaza kuona kwamba wapo watu kwa makusudi wameamua kupotosha vichwa vya sanaa.

Hao ni hodari wa kubuni mambo na kwa vile wako kwenye ardhi ya Wadanganyika, wanachokibuni na kukisema huonekana kuwa ni bora na chenye mwelekeo.

Mzee wa Busati angali akishangaa programu iliyoitwa ya kusaka vipaji vya muziki Tanzania. Hivi kweli nyota wa muziki anasakwa kwa staili hiyo? Huko ni kupotoka kwa kiwango cha hali ya juu.

Nyota wa muziki anapatikana kwa kumwangalia usoni? Ni lini mwanamuziki nyota akapimwa kwa umbo lake?

Ni lini nyota njema ya muziki ilipimwa kwa majaji ambao baadhi yao hawaujui huo muziki? Hivi ni vichekesho ambavyo kwa hakika vinaleta kichefuchefu cha kufungia mwaka.

Leo mwataka kuwa na kizazi kitakachowika kwenye anga ya muziki ndani na nje ya Tanzania. kwa mtindo huo wa kuangaliana usoni kama mpo kwenye gwaride la utambuzi wa wahalifu.

Wajuzi wa Kiswahili husema kwamba panya wengi hawachimbi shimo. Wanachomaanisha ni kuwa uwingi si hoja katika utekelezaji wa mambo muhimu.

Hao wanaojipanga kwa wingi wakinadi kusaka vipaji vya muziki nchini bila shaka ni wapotoshaji kutokana na ukweli kwamba staili inayotumika kuwasaka nyota wa muziki inakwenda isivyo.

Matokeo yake ni kwamba taifa lazidi kupoteza vipaji vya muziki kila uchao. Waandaaji wa shughuli kama hizo wengi wao wamekaa kwa ajili ya neema binafsi na si kweli kwamba wana mema kwa muziki wa Tanzania.

Matatizo ya aina hiyo ni mengi na ndio maana asilimia kubwa ya Wabongo wamesusa mema ya kwao.
Anachosema Mzee wa Busati ni kuwa wasanii wetu hasa wa muziki hawasaidiwi katika kuendesha maisha yao kwa thamani halisi ya kazi zao.

Leo hii Mwandika Busati angetaraji kuona mashabiki wa muziki wamevaa fulana zenye nembo za wanamuziki kama Msafiri Zawose au Vitali Maembe.

Hazipo mtaani kwani hata chache zinazochapwa zinasuswa na maelfu kukimbilia fulana na kofia za 50 Cent.

Hayo yote yanakuja kutokana na namna jamii ilivyojengwa kuanzia huko nyuma. Na ndio maana Mzee wa Busati anasema staili ya kusaka vipaji vya muziki iangaliwe upya.

Hizi kelele zinazopigwa na kuchezwa na wengi wakiamini kwamba kuna vipaji vinasakwa ni kudanganyana na ni kupotosha sanaa.

Huu ni ukomo wa Mzee wa Busati kwa wiki hii. Panapo majaliwa tukutane wiki ijayo kwenye Noeli. Kila lililo jema liwakute na fanaka tele.

Wasalaam,

Sunday, December 9, 2007

Hili la Dewji na mustakabali wa soka yetu

na innocent munyuku

NI jambo la kawaida katika mkusanyiko wa binadamu kuwa na mawazo tofauti.

Hii maana yake ni kwamba kama itatokea siku binadamu wote duniani wakafanana mawazo katika kila jambo basi si ajabu dunia ikasambaratika zaidi.

Mzee wa Busati wiki iliyopita alisikia habari kwamba kuna wapenda michezo wametangaza kuipa Kilimanjaro Stars zawadi nono katika mfumo wa fedha kama wataibuka na Kombe la Chalenji.

Alianza Mohamed Dewji kuwatangazia Wabongo kwamba yeye binafsi atawazadia wachezaji donge nono la Sh milioni 35 na Sh milioni 24 kama watashika nafasi ya pili.

Baada ya Dewji kutangaza hilo, mfanyabiashara maarufu nchini Alex Massawe naye akasema atawapa wachezaji Sh milioni 10 kama watafanikiwa kutwaa Kombe la Chalenji.

Wenye busara wakaanza kunong’ona kwamba wawili hao hawakuwa na nia njema ya kuifanya Kilimanjaro Stars kufikia kilele cha mafanikio.

Kwamba kama wamelenga kuifanya Tanzania iwike katika medani ya soka hawakuwa na haja ya kuibuka leo na ahadi kama hizo za danganya toto.

Mzee wa Busati anaamini kuwa kuendekeza ahadi kama hizo ni sawa na kuua medani ya soka nchini. Ni wazi kwamba Shirikisho la Soka Tanzania lina uhaba wa fedha. Dewji analifahamu hilo hali kadhalika Massawe.

Mwandika Busati alitarajia kuwasikia watu hao wakitoa fedha kwa ajili ya maandalizi kabambe na si kuiacha timu dhaifu iingie mashindanoni.

Anachokiona Mzee wa Busati hapa ni porojo na hadaa kwa Watanzania na katika hili wanasoka wamedhihakiwa. Haiingii akili kwa mtu makini na mwenye nia ya dhati ya kuinua soka asubiri timu iingie uwanjani ndipo atoe ahadi ya fedha nono.

Dewji na Massawe walikuwa wapi wakati Kilimanjaro Stars inahitaji fedha za maandalizi? Hivi ni kweli hawakujua kwamba kambi inahitaji fedha kwa ajili ya maandalizi?

Ukweli wa mambo ni kwamba huo ni mfano kwamba Watanzania walio wengi mbali na kuwa na uwezo wa kukuza michezo wanajificha kwa makusudi.

Ahadi kama hizo hazina maana nyingine zaidi ya kudidimiza michezo nchini. Vijana wanatakiwa waandaliwe na kama wamepata maandalizi ya kutosha hawana haja ya kuahidiwa mema kwani watakuwa tayari wana ubavu wa kufanya vema mashindanoni.

Tangu mwanzo Mzee wa Busati ameweka wazi kwamba binadamu lazima watofautiane katika mtazamo. Ndicho anachofanya hapa. Kuna waliokaa na kukenua wakifurahia ahadi hiyo ya fedha. Hiyo ni haki yao ya msingi na wana uhuru wa kufanya hivyo.

Lakini kwa mtazamo wa Mwandika Busati kinachofaa kufanywa kama kweli bongo inahitaji kuvuma katika soka basi ni maandalizi na si kupiga soga.

Kama wana nia ya dhati ya kuinua soka ni heri wajitokeze mapema wakati wa maandalizi kwa timu za taifa. Kutoa ahadi pekee si dawa ya Tanzania kuwa kichwa cha mwendawazimu.

Hii ni sawa na kwenda kwa jirani yako mwenye njaa halafu unamwambia akimbie mbio za nyika na kwamba akishamaliza atazawadia fedha za kujaza mifuko yake.

Hiyo ni hadaa kwani mwenye njaa hawezi kumudu mbio hizo. Ataanguka na kupoteza maisha kwani hana ubavu wa kumaliza mbio hizo.

Kama una mapenzi na jirani huyo basi ni vema ukampa lishe bora na hapo umweleze aanze mbio za nyika. Huo ndio uungwana!

Hizo ngwenje mnazoahidi fanyeni mpango wa kuwaweka wachezaji kambini. Walishwe vema wawe na stamina, wafundwe njia za kisasa katika soka ili wakitinga dimbani waonyeshe makali.

Kukaa mezani na kusema juu ya ahadi si njia mbadala ya kuendeleza soka. Muda wa kubembelezana kwa peremende bila shaka umepitwa na wakati. Badilikeni!

Mzee wa Busati ameona awe tofauti na hao wanaokenua wakichekelea ahadi ya fedha. Kwani naye anao uhuru wa kuwa na msimamo wa tofauti.

Vinginevyo busati kwa sasa halikaliki. Mzee wa Busati yu katika pilika za kila aina ili kulinda heshima ya kaya yake kwa majuma ya raha na karaha yajayo.
Wasalaam,

Miaka 46 ya uhuru twajivunia nini?

Na Innocent Munyuku

NIPATAPO nafasi ya kuketi vijiweni na Watanzania wenzangu hasa vijana nanasa mambo mengi ambayo natamani mtawala wa nchi pia angepata wasaa wa kuyasikia.

Bila shaka anayapata lakini kwa vile sina uhakika ni heri nitumie nafasi hii kuyasema baadhi ya masuala yanayojadiliwa kila wakati huko mitaani.

Leo hii Watanzania wanatimiza miaka 46 tangu wapate uhuru kutoka mikononi mwa Waingereza mwaka 1961. Ni sherehe kubwa na yenye simulizi nyingi; mbaya na njema.

Miaka 46 ya uhuru si lele mama. Hii maana yake ni kwamba kama ni maisha ya binadamu Tanzania tayari ni mtu mzima anayejitegemea kwa mambo mengi.

Lakini kwa bahati mbaya sana miaka hii ya uhuru ni dhahiri kwamba hakuna jema la kujivunia ukilinganisha na mataifa mengine yaliyopata uhuru baada ya Tanzania.

Kinachosemwa mitaani ni kwamba Tanzania licha ya kuwa taifa huru, maisha ya Watanzania yameendelea kuwa magumu kila uchao.

Watu wanalalama juu ya kupanda kwa bei ya bidhaa hasa zile zinazohitajika katika maisha ya kila siku. Hicho ndicho wanacholalamikia.

Lakini pia wanasema juu ya uwajibikaji mdogo wa watendaji wa Serikali. Wanazungumzia ubovu wa baadhi ya mawaziri, wakuu wa mikoa na wilaya.

Ingawa wengi wao hawana ubavu wa kupaza sauti, wanasema kwa kadiri wawezavyo kwamba hata watendaji katika ngazi ya vijiji ni waovu wasiopaswa kukalia viti hivyo.

Hawaishii hapo, wanakerwa juu ya ubovu wa huduma za afya. Kina mama na watoto, wazee na wahitaji wengine wa huduma hiyo wanakwazwa na utendaji wa wauguzi na madaktari.

Hili pengine halihitaji mjadala mrefu kwani hospitali na zahanati nyingi mambo si shwari kwa wagonjwa. Ni jambo la kawaida kwa wagonjwa kulala wanne kitanda kimoja. Hili si la ajabu.

Si jambo geni pia kuwakuta wagonjwa wamerundikana chini wakilalia mkeka. Watanzania wamezoea. Si kama wameridhika bali mfumo umewaweka hapo.

Muhuri wa Mtendaji wa Serikali za Mitaa nao siku hizi umekuwa mradi mkubwa kwa hao wenye dhamana ya kuushika. Karatasi haigongwi pasipo rupia mkononi.

Wananchi wamezoea kulipa fedha hata kwa yale ambayo wanapaswa wahudumiwe bure. Yanaonekana kama vile yameshakuwa sugu na yasiyoweza kufutwa.

Hayo ndiyo yanayojiri katika miaka hii 46 ya uhuru wa Tanganyika. Rushwa imeendelea na inazidi kushika kasi ya ajabu kutokana na ukweli kwamba mbinu za utoaji na upokeaji rushwa zinabadilika.

Watu wanakwenda kwa mtindo wa kisasa na kutokana na hali hiyo si rahisi leo hii kuwanasa wala rushwa kama ilivyokuwa miaka 10 iliyopita. Mbinu zinabadilika.

Pamoja na ukweli kwamba wananchi wana mchango mkubwa katika kukabiliana na rushwa, wanacholalamikia wao ni kwamba walio juu ndio viongozi wa jambo hilo.

Wanasema kama katibu mkuu wa wizara anadaka rushwa mwananchi wa kawaida afanyeje? Tule wote kwani huo ndio utaratibu uliopo.

Wengine wananong’ona kwamba kama mbunge fulani katinga bungeni kwa njia ya hongo diwani naye ataachaje kutetea nafasi yake kwa rushwa?

Haya si mambo ya siri yanasemwa lakini kwa bahati mbaya sana si rahisi kuyapatia ushahidi. Lakini ukweli wa mambo ni huo rushwa inanuka nchini.

Hii maana yake ni kwamba walio wengi hawapati huduma kwa kiwango kinachostahili. Kama ni ajira, matibabu na mengine hayapatikani mpaka utoe rushwa.

Ukikanyaga polisi utaambiwa hawana karatasi ya kuandikia maelezo ya mlalamikaji. Lakini kabla ya hilo kama utakuwa unahitaji kuwapeleka mahala alipo mtuhumiwa utaelezwa kwamba hawana gari na kama lipo watasema halina mafuta. Kodi tunazolipa zinatumikaje?

Hizo zote ni njia za kukufanya uwe mstari wa mbele kufungua pochi na kuwapa ulichonacho ili mambo yaende.

Hii ndiyo miaka 46 ya uhuru wa Tanganyika tunayoishi. Kwa uwazi ni kwamba maisha ya rushwa hayana maana nyingine zaidi ya kuendelea kukandamizana na kwa njia hiyo kuliangamiza taifa.

Kuna waliodiriki kusaini mikataba hafifu ya kimataifa ambayo leo hii taifa linaangamia kwa kukosa maarifa. Waliopewa dhamana wamekula cha kwao na hawana hofu ya maisha.

Anayepata taabu ni mlalahoi ambaye hajui aanzie wapi ili afikie kilele cha maisha bora. Amekwazwa na mfumo ambao hautaki mabadiliko.

Hayo ndiyo yanayosemwa vijiweni lakini hakuna shaka kwamba ndiyo hali halisi kwa maisha ya kila siku.

Je, katika miaka 46 ya uhuru Watanzania tunajivunia nini? Imani na utulivu wa kutoona mabomu yakilipuka mitaani? Pengine yapaswa kuwapo na tafakuri ya kina kwani kwa mtazamo wangu amani kamili maana yake ni kuwa na utulivu wa akili pia.

Kama matumbo hayana shibe sidhani kama mtu anaweza kutembea kwa matao akisema kuwa yu na amani ya kweli. Tusibweteke na miaka 46 ya uhuru tusake njia ya kujikwamua uwezo tunao.

Tuesday, December 4, 2007

Tusisubiri wawe watu wazima wa mitaani

Na Innocent Munyuku

HUSEMWA kwamba usipoziba ufa utajenga ukuta. Lakini wajuzi wengine wa lugha wakaja na msemo mwingine kwamba samaki mkunje angali mbichi.

Wapo wengine waliosema pia kuwa tohara ya Ijumaa huanza Alhamisi. Hii yote ni misemo ya hadhari kwa binadamu awe na hulka ya maandalizi.

Kwamba kama wahusika wa jambo wanafanya mambo pasipo maandalizi ni wazi kuwa suala walifanyalo halitakwenda sawia. Watavurunda na hivyo kuonekana waliokosa umakini.

Jamii yetu leo hii inahaha kufuta wimbi la watoto wa mitaani. Semina na warsha mbalimbali zinajadili suala hilo.

Sehemu za mijini watoto hao ni wengi. Tunapishana nao na la kusikitisha ni kwamba haieleweki ni nani anawajali watoto hao kwa dhati.

Wataambulia Sh 100 au Sh 500 ambazo kwa mtazamo wa kawaida haziwasaidii kuishi kwa uhakika.

Hii ni kusema kwamba maisha ya watoto hawa ni ya shibe ya leo. Wakiumwa na washindwe kujipanga mitaani kusaka fedha kutoka kwa raia wenye huruma basi hakuna shaka kwamba siku hiyo ni kama kiama kwao.

Zipo asasi zilizojiandikisha kuwa mstari wa mbele kuwatumikia watoto hao. Vipo vituo vinavyolea watoto hao wa mitaani lakini ukweli wa mambo ni kwamba mahitaji hayatoshelezi.

Hii ni kusema kuwa watoto waliopo vituoni ni wachache ukilinganisha na ujumla wa waliobaki kuzurura mitaani.

Lakini hoja yangu ni kwamba mtima wangu umejaa shaka juu ya mustakabali wa watoto hao ambao wengi wao ni wenye umri wa miaka kati ya miwili hadi 15.

Hawa wanaendelea kuomba lakini wakishavuka umri huo ‘wanajiajiri’ katika kazi nyingine. Katika miji mbalimbali nchini watoto hao wakishakomaa hujihusisha na kuosha magari ili wapate kuishi.

Wakati mwingine watoto wa aina hiyo hugeuka kuwa ‘walinzi’ wa muda wa magari hayo ingawa uzoefu unaonyesha ni hao hao wanaokwapua vioo vya magari au vipuri.

Kwa mtazamo wangu, hatua ya aina hiyo ni mbaya kwani wakishaanza kukwapua vipuri wataenda mbali zaidi kwa kujifunza uhalifu uliokomaa.

Hawana nafasi kwa elimu ambayo kwa hali ya kawaida ingewasaidia kusaka namna nyingine ya kuishi.

Kwa maana hiyo wataelekeza akili zao kutenda uhalifu zaidi kuliko wema ndani ya jamii.

Watafanya hivyo kutokana na ukweli kwamba hawana namna nyingine ya kujiingizia kipato. Wataosha magari na mwishowe watachoka.

Na ukizingatia kuwa watoto hao wako mjini ni wazi kuwa wanaishi katika mazingira ya kujifunza mbinu mbalimbali za kuyasukuma maisha.

Hawa sasa ndio hao ambao kwa mtazamo wangu sisiti kuwaita watu wazima wa mitaani.

Kwamba athari zake ni kubwa kuliko pengine sehemu kubwa ya jamii inavyofikiria. Madhara yake ni makubwa na hii maana yake ni kuwa tutakuwa na jamii yenye shaka daima.

Nani ataweza kuwadhibiti watu wazima hao wa mitaani ambao katika maisha yao ya awali wamekuwa katika dhiki na kukata tamaa?

Mamlaka gani inaweza kusimama na kujigamba kwamba inayo ubavu wa kuwadhibiti watu wazima hao wa mitaani?

Ukweli wa mambo ni kwamba tusitarajie kuwaona wakiwa na mema katika maisha kwani tayari wameshaathirika na mfumo wa maisha.

Mtu aliyeishi kwa mashaka katika miaka mingi si ajabu akawa na uamuzi wa kubomoa zaidi kuliko kuijenga jamii. Hebu fikiria tangu akiwa na umri wa miaka miwili anaishi mtaani unadhani akiendelea hivyo hadi miaka 25 atakuwa katika hali gani?

Hakuna shaka kwamba atajifunza njia mbadala ya kujikwamua na ugumu wa maisha na katika hili hatasita kujifunza njia yoyote atakayoona inafaa. Atafanya hivyo kwa sababu hana cha kupoteza.

Tusifikishane huko kwani jamii ya Watanzania inao uwezo wa kuwanusuru watoto wa mitaani. Tusisubiri waitwe watu wazima wa mitaani.

Safari hii jaribuni Miss Bantu

na innocent munyuku

YAMETIMIA! Hadithi imekuwa ile ile kwa Tanzania kuangukia pua kwenye mashindano ya urembo ya dunia.

Binti aliyelalamikiwa hadi koo kuwaka moto, Richa Adhia aliyeiwakilisha Tanzania katika Miss World amevurunda na wala hakupata nafasi ya kufurukuta.

Kilichosemwa na mrembo huyo ambaye rangi yake ilimweka mbali na mashabiki wengi wa urembo akasema kuwa Kamati ya Miss Tanzania imechangia yeye kuboronga.

Kimwana huyo akaweka wazi kwamba Kamati ya Miss Tanzania ilishindwa kuwahisha DVD yenye shughuli alizozifanya baada ya kuwa mrembo wa Tanzania katika Kamati ya Miss World.

Anacholalama Richa ni kwamba kama DVD yake ingewahi angekuwa na nafasi ya kushinda katika kipengele cha Urembo wa Malengo.

Hii ni bahati mbaya kwa mlimbwende huyo na wadau wa urembo nchini. Lakini yaweza semwa pia kuwa bado kuna kikwazo katika mchakato mzima wa kumsaka Miss Tanzania.

Mzee wa Busati alikuwa mmoja wa walionyesha shaka juu ya uwezo wa kimwana huyo katika uwakilishi wake katika mashindano hayo ya dunia.

Alichosema Mwandika Busati wakati huo ni kwamba ushindi wake ulijaa shaka na hata ndimi za mashabiki zimeendelea kuwa hivyo. Wengine wakasema pia kuwa kwani kulikuwa na ulazima gani wa kumvisha taji na kimwana huyo mwenye damu ya Kihindi?

Wanaojiita wanaharakati na watetezi wa haki za binadamu wakasema kuwa huo ni ubaguzi wa rangi. Lakini hoja ikabaki ile ile kwamba je, mrembo huyo anaujua vema utamaduni wa Kitanzania?

Pengine hoja hizo hazina nguvu tena kwani mambo yamekwenda na yamesikika sasa kilichobaki ni wenye mamlaka na urembo wajipange upya.

Lakini wakati wanajipanga upya Mzee wa Busati anawaza jambo moja ambalo laweza kuijengea heshima na Tanzania kwa ujumla wake.

Kwanini basi tusisitize kuwapo kwa Miss Bantu? Mashindano ambayo kwa hakika yanalenga moja kwa moja asili ya kina dada wengi hapa Bongo.

Kuwa Miss Bantu si jambo gumu kwa sababu kwa baadhi ya vigezo ambavyo Mwandika Busati anavielewa ni kwamba binti hahitaji kuwa mwembamba ili kupata sifa ya kupanda jukwaani.
Hiyo ndiyo burudani ya Miss Bantu. Kimwana na ‘minyama’ yake anakuwa huru kupanda jukwaani kusaka ushindi mbele ya majaji.

Hii maana yake ni kwamba mabinti washiriki hawabanwi kula na kunyaza miili yao. Inasemwa pia kuwa hata lugha si kikwazo, unanena Kiswahili utakavyo na wala hakuna haja ya kwenda inglishi kozi.

Mtazamo wa Mzee wa Busati ni kwamba kama mashindano ya Miss Bantu yatawekewa mkazo basi nasi siku moja tutaungana na Wakongo, Warundi, Waganda na Wakenya na kuanzisha mashindano ya kanda.

Wakifikia hatua hiyo ni wazi kuwa Afrika itakuwa na kitu chake manake matarajio ni kwamba yatapanuka hadi kwingineko.

Ndoto ya Mzee wa Busati ni kwamba ifike siku hata Wazungu na Wahindi vibonge nao waje washiriki mashindano hayo. Hata kama wao si Wabantu waruhusiwe kwa sifa yao ya ubonge.

Kwanini yatuwia vigumu kuamini mambo mema ya kwetu? Kwani lazima tufuate kila kitu kilichoanzishwa Ulaya? Bila shaka hakuna haja hiyo. Yawezekana mengine yakaanzia Afrika na kuwashangaza walioko nje ya Afrika.

Huo ni mtazamo tu na si lazima wote mkubaliane na Mwandika Busati leteni hoja zenu kwa mjadala na lengo liwe kufikia mwafaka.

Huenda ikasemwa kuwa Mzee wa Busati ni mwepesi wa kukata tamaa la hasha! Mwelekeo wetu katika mashindano hayo ya Wazungu si mwema na siasa za Miss World katu hatuziwezi.

Si mmesikia wiki iliyopita warembo kutoka Afrika walivyokuwa wakilalama? Walikuwa wakilalamikia ubaguzi. Walichosema wala si uzushi ni ukweli na wazi wa mambo.

Basi himizeni mashindano yenye kufanana na utamaduni wetu. Waacheni warembo wetu wa Kiafrika wawe na pahala pa kujitanua.

Msiwashindishe njaa eti ili waonekane warembo wenye sifa za kupanda jukwaani kuwania taji la Miss World. Waacheni wale matoke na maharagwe.

Vinginevyo kung’ang’ania hayo ya ughaibuni ni kuzidi kujaza nafasi na ghasia kwenye ardhi ya Wadanganyika.

Huu ndio ukomo wa Mwandika Busati kwa juma hili. Mwendo mdundo kwa kasi ya ajabu manake ujio wa Masiha unayumbisha fikra.

Ngwenje zinasakwa kwa kila mtindo, kihalali na kiharamu ili mradi mifuko yao ijazwe fedhwa kwa ajili ya Noeli na mwaka mpya.

Wasalaam,