Sunday, May 25, 2008

Ni dansi au onyesho la vichupi?

Na Innocent Munyuku

BILA shaka mambo yanakwenda sawia. Mwandika Busati kama ilivyo kawaida yake yu safuni kujichanganya na wadau wake katika mijadala ya kila wiki.

Kwa juma hili hakuna shaka kwamba kila kitu kinakwenda vema manake kwenye viti virefu umati umejaa. Lugha zinagongana kwa tambo za kila aina.

Ukipita kwingineko pia watu wanaringa, wakipita kila mahala kwa matao. Utawaambia nini wakati mifuko imejaa shilingi? Muda wa mavuno umewadia na kwa walio wengi kila kitu kinawezakana kwa sababu fedha inaongea.

Mzee wa Busati kama kawaida yake kila siku kwake ni sikukuu. Si kama anazo nyingi bali amejiwekea mfumo usiohitaji makuu. Yeye na vitegemezi vyake hata wakila dagaa na dona yatosha. Vipapatio vya kuku ni majaliwa.

Siku chache zilizopita Darisalama ililipuka kwa burudani ya muziki wa dansi. Mbwembwe kila pahala, mashabiki wa Akudo Impact na FM Academia wakatambiana kila walivyoweza.

Miamba hiyo ya muziki wa dansi ikapiga maonyesho kwa siku moja. Mashabiki wakapagawa kama inavyokuwa kwa Simba na Yanga. Hata leo hii bado simulizi ya maonyesho hayo zinarindima.

Pamoja na mashabiki kupata uhondo huo, Mzee wa Busati ana lake jambo kuhusiana na maonyesho hayo. Jambo lenyewe ni nidhamu ya mavazi jukwaani.

Kilichotokea kwenye majukwaa wakati wacheza shoo wakifanya vitu vyao ni aibu ya mwaka. Mwandika Busati anazungumzia vichupi vya kina dada waliokuwa wananengua.

Hivi kweli huu ndio mfumo mliojiwekea? Wa kupanda jukwaani mkiwa nusu uchi? Akudo na FM Academia wanaweza kutoa jibu kwa swali hili.

Kibaya zaidi ni kwamba katika maonyesho hayo walikuwapo watendaji wa Serikali ambao walijumuika na mashabiki wengine kushabikia muziki uliokuwa ukiporomoshwa. Hakuna siri kwamba hata hao vichupi waliviona.

Je, wamechukua hatua gani juu ya hilo? Hivi muziki huo wa Kikongo hauchezeki hali kuonyeshana mipaka ya Ikulu?
Mzee wa Busati yu radhi aitwe mshamba, wa kuja na majina mengine lukuki lakini hili la kuonyeshana nyeti jukwaani hakika atalikemea. Raha i wapi basi kuonyeshana ya faragha?

Ipo siku wataingia na kuvamia jukwaa wakiwa uchi wa mnyama. Hilo litatokea kwa vile husemwa kuwa dalili ya mvua ni mawingu. Hawataona ugumu kufanya hivyo kwa sababu watakuwa wameshakuwa sugu na uovu wao.

Shingo zao zimeshaanza kuwa ngumu na ndio maana hawaoni soni kusasambua mbele ya hadhara na wanapopigiwa kofi akili zao hucharuka na kuwaka tamaa ya kuzidisha misasambuo.

Zi wapi mamlaka za kusimamia maadili katika sanaa? Hao nao wamekaa kimya. Wamejifungia kwenye vyumba wakijadili namna ya kula fedha za semina.

Hawana mawazo ya kukemea watu wanaokosa maadili jukwaani. Hivi muziki wa aina hiyo sharti wanawake wacheze kwa kuonyesha nyeti zao? Hii maana yake nini?

Au tuseme kwamba dunia ndivyo ilivyo? Kila mmoja yu huru kufanya atakalo ili mradi linaungwa mkono na hadhira. Mwandika Busati haelewi yanayoendelea zaidi ya kumuumiza kichwa.

Basi kama mmeamua kukaa kimya pasipo kukemea, Mzee wa Busati hatafumba mdomo atayasema kwani historia ndiyo yenye kutoa hukumu. Vijukuu vitaelezwa kwamba kibabu chenu hakikupenda mambo fulani.

Huu ndio mwisho wa hoja yake kwa juma hili. Kama ilivyo kawaida yake, Mzee wa Busati anaenda mafichoni kula raha. Ndio manake maisha haya ni mafupi linalowezekana leo lisingoje kesho.

Acha akajitafutie makazi ya faragha kwa kufanya tathmini wakati huu tunapokaribia nusu mwaka. Je, ahadi na mipango ya mwaka 2008 inakwenda sawia au inakwenda upogo?

Vinginevyo kila la heri. Baraka zikufikie hapo ulipo na tuonane juma lijalo tukiwa na siha njema.

Wasalaam,

Sunday, May 18, 2008

Chonde msimu huu msiyaige ya kifaurongo


Na Innocent Munyuku

ASIKWAMBIE mtu raha ya mjini sharti uwe na ngwenje kibindoni. Utakula unachotaka badala ya kula unachopata. Hayo ndo maisha ya mjini.

Lakini wakati mwingine raha hizo hugeuka karaha pale unapoona kuwa wenye kufanya matanuzi wengi wao wamezipata fedhwa kwa njia zisizo halali.

Hao ndio waliojaza miji miaka hii. Wanatumia fedha haramu kufanya matanuzi na kibaya zaidi ni kwamba wanatumia ngwenje hizo hizo zinazonuka kujitakasa.

Kujitakasa kwao kunakuja kwa njia ile wanayoiita eti misaada kwa yatima na wasiojiweza. Hivi kweli sadaka zenu zinakubalika kwa Muumba?

Kilio hiki cha Mzee wa Busati kimekuja baada ya kufanya kajitafiti kiduchu na kubaini kuwa katika maonyesho mengi ya burudani yanayopangwa na kukamilika, mpangilio mzima umejaa dhuluma.

Pengine mfano mdogo tu ni pale unapoona wajanja wa mashindano ya urembo nchini wanapomaliza kukusanya viingilio na kisha kujifanya kusaidia yatima.

Ukweli wa mambo ni kwamba ukiangalia mchakato mzima wa mashindano hayo hadi fainali kwa walio wengi wamepitia dhuluma. Watawalaghai wadhamini na washiriki pia. Hivi kweli huu ni uungwana?

Anachosema Mzee wa Busati ni kwamba dhamira ya misaada ya aina hiyo iendane na uhalisia wa wanaopewa misadaa katika jamii.

Mwandika Busati angali akielea hapo hapo katika ulimbwende kwa hoja kwamba misaada hiyo inayotolewa ni kweli kwamba inawasaidia walengwa? Pipi ni biskuti?

Hivi ni kweli kwamba yatima wanahitaji sana peremende na biskuti? Hiyo iwe ziada ila la msingi liwe kuwajali katika elimu ili maisha yao yawanyokee huko mbele ya safari.

Si waandaaji wa urembo tu wenye hulka ya kutenda hayo bali asasi nyingine za kijamii ambazo wakati mwingine hutumia yatima kujitangaza. Huku ni kupotoka.

Mzee wa Busati ameamua ayaseme haya mapema kwani kwa uzoefu wake watu wa aina hiyo kila mwaka wamekuwa wakiiga maisha ya kifaurongo.

Kifaurongo au pahala pengine hujulikana kama kiforongo ni mdudu ambaye kwa kawaida hupatikana katika kokwa ya embe na hujikinga kwa kujifanya amekufa pindi aguswapo.

Hivyo ndivyo walivyo hao wanaosemwa na Mwandika Busati. Wakiguswa kwa kuelezwa ukweli hukaa kimya na kujifanya hawasikii ama wamelala fofofo.

Hujifanya hamnazo kwa kutojali wanayoambiwa kuhusu mwendo wao katika jamii. Leo hii utakemea juu ya rushwa ya ngono, kesho wanayarudia na hivyo kwenda mbele miaka kibao ijayo.

Kwanini waendelee kuziba masikio? Au hawa si wenzetu katika jamii? Mitima yao i migumu kiasi gani? Mkiguswa leteni mshituko na si kujifanya mmekufa.

Mwandika Busati ataendelea kuyasema anayoyaona kuwa ni mabaya na hataacha kuyasifu yaliyo mema. Anafanya hivyo ili kutoihadaa dhamira yake.

Dhamira anayoisema ni ile ya kutumia vipaji mbalimbali kuwasaidia mambo ya msingi wasiojiweza na si kuwapa yanayoyeyuka kwa siku moja.

Hima uwe mshikamano, wasanii na wabunifu wa aina mbalimbali wajenge msimamo wa kuwasaidia kwa dhati yatima walio vituoni na wale wanaolala majalalani. Kama ni peremende basi viongwezwe na vingine vya kuwajengea maisha.

Mwandika Busati wakati anaelekea ukingoni atoe pongezi zake kwa Taifa Stars kwa kuinyamazisha Uganda Cranes. Basi na wakaze buti, wasiogope fangasi ili wakanuse ardhi ya Ivory Coast katika fainali za Kombe la Mataifa Afrika.

Mzee wa Busati atashangaa kama kutakuwa na porojo tena msimu huu. Amkeni na kasi iwe ya mbele kwa mbele.

Huu ndio ukomo wa Mzee wa Busati kwa juma hili. Wiki ya maumivu kwa walio wengi na mifano iko wazi tu. Idadi ya wanaoning’iniza miguu kwenye viti virefu imeshuka. Wametoweka kama ndui.

Mzee wa Kutibua na jopo lake pale Tabata Relini wameingia mitini. Simu zao zimezimwa kwa kuhofia madeni. Ila huziwasha usiku wa manane kwa ajili ya kusoma meseji. Poleni ila ipo siku mtajuta na kusaga meno.

Kama kwenye ule mlima mrefu kuliko yote barani Afrika hakuendeki basi ni heri mwende pachoto mkakusanye mabibo mtengenezee uraka ili mjidunge kwani hamkani fedhwa ya lager hamnayo!

Wasalaam,

Sunday, May 11, 2008

Bado tuendelee kuisubiri kastabini?

Na Innocent Munyuku

KUMEKUCHA! Ni Jumanne nyingine ambayo Mwandika Busati anatua kwenye anga zake za kujidai kwa ajili ya kuleta porojo zake.

Wiki imeanza vema ingawa siku kadhaa zilizopita mambo yamekwenda upogo. Ngwenje zimeanza kuyeyuka kwani kuna mengi ya kutekelezwa yamefuata mkondo. Suruali zimekuwa tupu.

Waliokuwa na ubavu wa chips na kuku wa kompyuta sasa wanalamba ugali na maharagwe ya Mbeya kwa sababu hata mkaa wa Msata haupatikaniki! Bei juu kwa kila kitu.

Hali inatisha wajameni na kama twafundwa juu ya kusoma alama za nyakati hii ni wazi kwamba Bunge la Bajeti nalo msimu huu litajaa maumivu. Kama vipi mlalahoi kapige debe upate mlo!

Mzee wa Busati wiki hii hoja yake kuu ni juu ya haya mashindano ya Kombe la Taifa yanayoendelea kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Maelfu wanakenua meno lakini kuna jambo haliko wazi.

Mzee wa Busati kasoma magazeti, kasikiza maoni ya wanaojiita kuwa ni wadau wa soka ingawa wanaonekana kujikita kwenye taarabu na muziki wa dansi. Eniwei wasihukumiwe kwa hayo kwani bongo husemwa kwamba hakuna spesholaizesheni.

Kila mmoja na lwake na ndio maana leo unaweza ukamwona Momburi akinywa Kilimanjaro badala ya Safari lager aliyoizoea anachojali ni ulabu wa kulipua ubongo wake ili kesho yake ahangaike kusaka ilipo supu ya mapupu.

Ni kwamba bongo hapa kila jambo linakwenda hata kama halikupangwa liwe hivyo. Na kwa mantiki hiyo usishange waziri fulani nyeti akienda kuwa mgeni rasmi kwenye Kipaimara.

Ataacha shughuli nyeti za kitaifa na kukimbilia huko. Huyo bila shaka anakuwa amesahau kuwa kuna yatima wanaosubiri japo mkono wake waushike nao wafarijike.

Waziri kama huyo amesahau kula na watoto wa mitaani ambao daima mlo wao uko jalalani. Hayo yote yamesahaulika na wakuu wetu wa kaya. Wamebaki kukumbatia urafiki na kwenda kuhudhuria ubarikio wa washikaji zao na kuwavuta wanahabari kama vile ni suala la kitaifa.

Hata hivyo, porojo za Mzee wa Busati hazilengi kuwashukia hao juma hili. Anawaweka kiporo wazidi kuharibu ili siku ikifika apate mengi ya kutema kwenye ndimi zake. Acha wawekwe kiporo.

Wiki hii anachosema Mwandika Busati ni kuhusu hayo mashindano ya Kombe la Taifa. Kwamba hivi lengo haswa ni nini?

Shirikisho la Soka Tanzania-TFF halina budi kuweka wazi maana halisi ya mashindano hayo kwani sasa washika kalamu na wadau wengine wa soka wamekuwa wakisagana kuhusu kiini cha michuano hiyo.

Ukikutana na nasoro utakwambia kuwa ni ya kusaka vipaji lakini wakati huo huo Mwakatobe atasema kuwa ni ya kusaka fedha za kuisaidia timu ya mkoa. Ukweli ni upi?

Mdau mwingine wa soka majuzi katanua msuli wa koo akasema eti mashindano hayo si ya kuibua vipaji na kwamba kama kuna michuano maalumu ya kufanya hivyo. Akaitaja kuwa ni Copa Coca Cola.

Lakini pamoja na mchanganyiko huo wa habari bado Mzee wa Busati anaamini kwamba mashindano hayo hayakupaswa kuwashirikisha wanasoka ambao tayari wamevuma Ligi Kuu Tanzania Bara.

Michuano hiyo ingabakishwa kwa ajili ya ndugu zetu wa Pachoto ama Kigoma ambao hawana mwanya wa kushiriki mashindano ya kimataifa kama hayo.

Hivi kweli kulikuwa na umuhimu kwa timu ya Mkoa wa Ilala kuwajaza nyota wa Simba na Yanga? Hii maana yake nini? Kwani ndani ya Ilala hakuna wanasoka chipukizi wa kuuwakilisha mkoa huo?

Anachokiona Mzee wa Busati ni kwamba michuano hiyo imebakwa na kuna haja ya TFF kujipanga na kuweka kanuni.

Kama Mwandika Busati angelikuwa na mwanya wa kupendekeza angelisema kwamba mashindano hayo waachiwe wanasoka wasiovuma ili miaka ijayo wanasoka waliofichika waongeze bidii watambulike katika ushiriki wao.

Kwa wajuvi wa Kiswahili, kastabihi husemwa kwamba ni chombo cha chuma au plastiki kinachowekwa kwenye ncha ya kidole cha shahada wakati wa kuingiza sindano katika kitambaa wakati wa kushona ili sindano isichome. Pahala pengine, kastabini huitwa subana ama tondoo.

Na ndio maana Mzee wa Busati anasema kwamba bado wadau wa soka wanapaswa kuwa na subira. Wasubiri ujio wa kastabini na waache wenye ubavu wa kupanga yasopangika waendelee na mambo yao.

Vinginevyo papara italeta yasiyoelezeka. Hadithi ya kupanda kwa soka itakuwa yenye ukakasi wa kimbunga na kilio cha kusaga meno.

Wasalaam,

Sunday, May 4, 2008

Hata walimbwende wanaulea ufisadi

Na Innocent Munyuku

USIOMBE kuzimika ghafla kwenye steji. Ni kama vile kifo cha penzi kinavyokuwa. Ni shubiri kwa kwenda mbele. Msosi hauliki mwanawane.

Mzee wa Busati kaleta kero, alitokomea gizani na mbaya zaidi ni kwamba hakuwa na uungwana wa kutoa neno la kwaheri. Yalomkuta ni siri yake ila ukweli ni kwamba kishapewa notisi yenye maelekezo machungu.

Watoa notisi ambao ni wadau wake wamemweleza wazi kwamba kama akirudia kutenda aliyoyatenda yaani kuzimika pasipo taarifa basi asubiri kumwagiwa upupu. Hakika ni adhabu kubwa.

Kwa hakika Mzee wa Busati anastahili adhabu kwani huo kwa kweli ni uhuni kama afanyavyo Mzee wa Kutibua ambaye yeye anaweza kuamua kulala popote hata kama kaunta kilevi kikimkolea. Ipo siku atajuta!

Tuachane na hayo, bila shaka wadau wameelewa somo kwani kuzimika kwa Mwandika Busati hakukuwa katika utani bali alikuwa akiwajibika katika masuala mengine ya kitaifa kule Idodomya kwenye jengo linalopitisha sheria. Mhh samahani wanasema ni jengo la watunga sheria.

Huko Mzee wa Busati kawa shuhuda wa mambo mengi, mema na mabaya. Ila alilofurahia Mwandika Busati ni kuona kuwa kumbe kuna majimbo ya uchaguzi ambayo ni kama hayana wabunge.

Kwamba yaliyo mengi yana wawakilishi bubu, hawasemi hawa, ndimi zao zimenasa wasipate kutoa sauti hata ya kuuliza suala mojawapo la jimboni kwake.

Mbaya zaidi ni kwamba kati ya wabunge hao ‘mabubu’ wanatoka sehemu ambako umasikini umekithiri. Cha ajabu ni kuwa wabunge waliotoka kwenye neema ndio wanaopaza sauti kudai tija kwa wapigakura wao. Hakika wonders will never cease.

Anyway hebu sasa turejee kwenye porojo zetu za kispoti na burudani. Hayo ya siasa hayafai manake unaweza ukijikuta unabadilishwa jina muda si mrefu. Wenye majimbo wasije wakatukimbiza mjini.

Pamoja na Mwandika Busati kuwa kimya kwa zaidi ya majuma mawili, ukweli wa mambo ni kwamba amekuwa karibu na kila jambo linalopita mjini.

Mojawapo ni haya maandalizi ya kusaka vimwana katika hatua za vitongoji na hatimaye kuingia kwa shindano la taifa la kigoli wa Tanzania.

Mawakala wa vitongoji wameshaanza kuingia mtaani kusaka fedha na mambo mengine ya kukamilisha mashindano. Mabingwa wa kuandika propozo za kuomba udhamini huu ni wakati wao wa kujidai.

Mabingwa wa kuongeza cha juu nao ni wakati wao wa kujaza matumbo kwani raha ya udhamini kwao nafasi zao ni kujaza fedha mfukoni ili mambo yawaendee sawia.

Hata hivyo, kwa mtazamo wa Mwandika Busati ni kwamba kuna ulazima wa kuweka mikakati ya makusudi katika maandalizi hayo hasa kutokana na historia ya mashindano hayo nchini.

Kila mwaka kero huwa ni zile zile; kashfa za ngono, upendeleo usio wa lazima katika kuwapata washindi na wakati mwingine utapeli kwa baadhi ya mawakala.

Ndimi za baadhi ya mawakala hujaa neema wanapotangaza mbele ya vyombo vya habari juu ya kuwapo kwa zawadi nono.

Watasema habari njema wakijitakasa kwamba msimu huu mambo ni shwari na zawadi ni za kutakata. Hata hivyo, kwa bahati mbaya huwa ndivyo sivyo.

Huu si mpango mzuri kutokana na ukweli kwamba kama ulaghai huu hautapigiwa kelele, ipo siku yatakuja mabaya zaidi na hivyo kuondoa maana nzima ya kuwa na michuano ya aina hiyo.

Lakini pendekezo la Mwandika Busati ni kwamba wakati mawakala wa urembo wenye damu ya kidhalimu wakipigiwa kelele, ni vema washiriki wakawa mstari wa mbele kusema kwamba kuna uvundo ndani yake.

Wakinyamaza na kuacha yapite maana yake ni kwamba mizizi itazidi kupata nguvu na hivyo kukomaza ufisadi katika sanaa hiyo.

Kina dada washiriki wawe mstari wa mbele kukataa udhalilishwaji kama utajitokeza kambini. Hali kadhalika wakinusa rushwa ya ngono wainue ndimi zao na kusema na wala wasikae kimya.

Na kwa kufanya hivyo, idadi ya wahuni katika urembo watapungua kama si kutokomea kabisa.

Mwandika Busati anafikia ukomo. Anajituliza akiangalia neema zinavyomshukia kama mvua za masika zinazoendelea.

Wanaosema kuwa huu ni mwaka wa shetani wafikirie mara mbili mbili. Wanaweza pia kujitakasa kwa maji ya bahari ili kuondoa nuksi.

Wasalaam,