na innocent munyuku
JUMA limeanza vema kwa Mwandika Busati na bila shaka waungwana wengine mambo yao yanawaendea sawia. Hakuchi kumekucha.
Lakini kabla ya kuendelea na alichopanga kubwata leo hii Mzee wa Busati hana budi kuweka bayana kuwa kuwa ulingoni kwahitaji roho ngumu kama ya jambazi. Si utani mwanawane.
Manake kwa wiki nzima hii Mwandika Busati alitamani akitupilie mbali kilongalonga chake. Kisa? Madongo ya wasomaji wake waliojitambulisha kuwa ni wajuvi wa soka ndani na nje ya nchi.
Hao walifura kwamba Mzee wa Busati hakutakiwa kumtetea Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Marcio Maximo. Wakasema eti anastahili lawama kwa maelezo kwamba kocha huyo kutoka Brazil linakocheza samba haambiliki.
Watoa hoja wakatoa festi ileveni ambayo kama Maximo angeibeba basi safari ya Ghana kwenye fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika ingekuwa wazi.
Mzee wa Busati hakuwa na haja ya kubishana kwa kutoa misuli ya koo la hasha! Badala yake alijadiliana nao kwa hoja na kwa hakika Mungu mkubwa wengi wao wakaelewa kwamba Maximo anapaswa kupewa muda, kakuta soka ya bongo imeoza!
Hilo limepita. Wiki hii Mzee wa Busati kaja na jingine. Anazungumzia habari ya maandalizi ya Ligi Kuu Tanzania Bara itakayoanza kutimua vumbi wikiendi hii.
Ni kipindi cha neema kwa wadau mbalimbali wa soka. Bila shaka huu ndo wakati wa ‘makomandoo’ kubadili mboga na mavazi. Huu ni wakati wao wa kula mayai na viazi mbatata.
Lakini la kufurahisha ni kwamba pamoja na hayo yote ngoma iko katika maandalizi ya mpambano kati ya Simba na Yanga. Wengi wanasubiri hiyo Oktoba 24 mambo yatakuwaje?
Lakini wakati mkiendelea kusubiri kwa usongo, Mwandika Busati analeta chokochoko na safari hii anakuja na swali kwamba je, mtaendelea kwenda kwa sangoma Bwagamoyo au mtakimbilia Ngende msimu huu? (Ngende ni moja ya sehemu inayosifa kwa uchawi kusini mwa Tanzania.)
Ni swali na kizushi lakini ni bora likajibiwa kwa sababu msimu huu kuna hatari ya kuuana! Nani atakubali kudhalilishwa na hasimu wake?
Nani atakubali kusimangwa na wanachama eti kwa sababu alishindwa kutamba dimbani mbele ya mpinzani wake?
Kuna maneno mitaani kwamba msimu kama huu ukifika, tunguli nyingi zinapata wakati mgumu kwani kambi za Simba na Yanga zinahaha huku na kule kusaka njia ya ushindi.
Wanafanya hivyo eti kwa lengo la kupalilia uzuri wao wa mkakasi na kuwahadaa mashabiki kwamba wao ndio nambari wani. Mhhh huko sasa ni kuelekea motoni. Hirizi na soka wapi na wapi?
Kama ni wajuzi wa tunguli si bora basi mkae nyumbani na kuangalia shughuli nyingine, au mfungue ‘hospitali’ na kusaka wateja wataokuwa na matatizo mbalimbali ya kuhitaji tiba za jadi?
Pengine wengine wanaguna kwamba Mzee wa Busati kageuka mwendawazimu lakini huo ndio ukweli, mechi kama hiyo lazima wataalamu wameshaanza kupuliza ili mambo yaende sawa.
Kama mtaamua kwenda Ngende basi msihofu sana kwani mtapewa nauli ya kwendea huko na bajeti iko wazi. Na kwa waendao Bwagamoyo pia shaka ondoeni.
Leo hii mwaenda kwa sangoma kwa ajili ya kuwawezesha kushinda mechi wakati wenzenu wanacheza mpira wa kisasa. Mkishinda kwenda mechi za kimataifa mnapwaya kwani huko hakuabudiwi ndumba bali ufundi halisi uwanjani.
Hizi ni tetesi za mitaani lakini zina ukweli ndani yake. Hakuna urongo hapa. Wapo wanaolala makuburini kabla ya mechi. Badilikeni, chezeni mpira kwa kanuni za kisasa.
Leo hii mwaendekeza masuala ya uganga wa jadi katika soka mkichaguliwa timu ya taifa na kuboronga mwamtupia lawama kocha hivi kweli huu ni uungwana?
Mzee wa Busati anaelekea ukingoni kwa Jumanne hii akiamini kuwa wadau wake wanaendelea kumpa sapoti ya kila hali.
Jiji la Darisalama linaendelea kulipuka kwa raha zake ingawa vibaka nao wanaongezeka. Yote hayo ni maisha tutapambana hadi mwisho. Wakiingia anga za Mzee wa Busati anajua afanye nini kama ni kutembeza karate au masumbwi. Yote yanawezekana.
Husemwa kwamba waungwana huelezana mengi ya busara. Basi na Mzee wa Busati analo lake la kumalizia kwa watu wake kuhusiana na njia mpya za ukabaha jijini Darisalama.
Mkae mkijua kuwa jiji sasa limevamiwa. Wenye ndoa kaeni chonjo manake kuna sampuli mpya za machangudoa. Si wale wa Ohio na Barabara ya Shekilango la hasha! Siku hizi wanapita ofisini au baa kwa kigezo cha promosheni ya bidhaa ikiwemo miili yao.
Pengine hii ni taarifa njema kwa wakware. Vinginevyo chukueni tahadhari saa mbaya hii.
Wasalaam,
Monday, September 17, 2007
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment