Tuesday, September 25, 2007

Dk. Wilson na njozi za Shirikisho la Afrika Mashariki

JUMAPILI iliyopita tulichapisha makala yaliyotokana na
mahojiano maalumu na Dk. Edie Brown Wilson, ambaye ni
mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe. Katika
makala hayo yaliyoandikwa na Mwandishi Wetu INNOCENT
MUNYUKU, Dk. Wilson (70) alizungumzia mengi na kati ya
hayo, alielezea umuhimu wa kutumia maarifa kujenga nchi
na haja ya vijana kulipenda taifa lao. Hii ni sehemu ya
pili ya mahojiano hayo ambayo msomi huyo mzaliwa wa
Marekani na mwenye kibali cha ukazi Daraja A nchini,
anazungumzia umuhimu wa kuundwa kwa Shirikisho la Afrika
Mashariki.

KWA miezi kadhaa sasa, Watanzania kama walivyo wenzao wa
Kenya na Uganda, wanajadili kuundwa kwa Shirikisho la
Afrika Mashariki.
Mijadala imeendelea na tume ya kukusanya maoni ya
wananchi wa Afrika Mashariki ziliundwa kwa ajili ya
kutambua kama shirikisho hilo linahitajika.
Awali ilipangwa shirikisho hilo lianze mwaka 2013 lakini
kutokana na Watanzania wengi kutilia shaka uharakishwaji
wake ikakubalika na watawala wa Afrika Mashariki kuwa
Shirikisho hilo sasa lianze mwaka 2024.
Je, kwa upande wake Dk. Wilson analionaje suala hilo?
"Binafsi sioni kama kuna tatizo kama wananchi wameamua
hivyo. Ni jambo jema kabisa lakini nasimamia ukweli
kwamba kuna ulazima wa Afrika kuungana.
ÒLakini kwa vile Watanzania wengi walitawaliwa na hofu
ya kuanzishwa Shirikisho, basi kuundwe jukwaa huru, watu
waelimishwe waambiwe maana halisi.
"Nasema hivyo kwa sababu naamini kuwa kama watu
wataelimishwa kwa kiwango cha kutosha, muungano huu
utakuwa wenye manufaa.
ÒHakika utakuwa wenye manufaa kwa sababu ningali na
matumaini makubwa ya kuona Afrika ikiwa moja na bila
shaka hilo litatimia,Ó anasema Dk. Wilson.
Dk. Wilson anasema hofu ya Watanzania kujiunga na wenzao
imechangiwa na mambo mengi, mojawapo likiwa uchumi mbovu
wa taifa na hivyo kuona kuwa kuungana na wenzao kutazidi
kuwafunika.
"Hilo la kwamba uchumi wetu uko chini ni moja ya sababu,
lakini siku hizi Watanzania wana tabia nyingine
wameibuka nayo, wengi hawapendi watu kutoka nje ya nchi
yao," anasema Dk. Wilson.
Hata hivyo, kwa mtazamo wake Dk. Wilson, anasema kuna
mambo ambayo huwezi kuyakwepa hasa katika kipindi hiki
cha mabadiliko.
Anaeleza kuwa kama Watanzania hawataki mabadiliko hilo
ni jambo la hatari, kwani mabadiliko yatawageuka na
kuwabadili kwenda hali mbaya.
Dk. Wilson haishii kuzungumzia Shirikisho na ndoto yake
ya kuiona Afrika inakuwa kitu kimoja. Anaelezea mengi
kuhusu nafasi ya mwanamke, hasa katika kipindi hiki
ambacho wengi wanalilia usawa wa kijinsia.
"Nafuatilia mijadala mingi, makongamano ya wanaharakati
wanazungumzia kuhusu usawa wa kijinsia na nafasi ya
mwanamke katika uongozi.
"Mimi labda nitakuwa tofauti kidogo, suala la jinsia si
hoja kama kasoro za kubaguana zitakwisha. Kwa hiyo
kusema kuwa lazima tuwe na kiongozi mwanamke nadhani si
hoja sana. La maana tuondoe vizingiti vya kubaguana.
"Hoja ni je, ukandamizwaji umeondoka baina ya mwanamke
na mwanamume? Nadhani tujadili hili na si nani awe
kiongozi.
"Sawa tuseme kuwa lazima rais ajaye awe mwanamke, sawa
kabisa lakini je, ana vigezo? Au je, ana uwezo wa
kutuongoza?
"Tusiendeshwe tu na kampeni kwamba lazima awe mwanamke,
yatufaa tuseme kwamba kiongozi yeyote awe mwanamke au
mwanamume sharti awe na uwezo. Jambo la muhimu ni uwezo
katika masuala ya utawala.
"Sisemi kwamba hakuna mwanamke mwenye uwezo wa
kuliongoza taifa, ninachosisitiza ni kuwa suala la jinsi
ya mtu isiwe hoja bali uwezo wa kufanya kazi.
"Yawezekana mimi nisiwe mwanamke wa kudai sana usawa,Ó
anasema Dk. Wilson na kisha kuongeza kwa kicheko: ÒBado
ningependa mwanamume anihudumie kwa mambo mengine kama
ishara ya kunijali."
Dk. Wilson anazungumzia pia biashara, hasa bidhaa
zinazotoka Mashariki ya Mbali na kuingizwa nchini kwa
kishindo cha hali ya juu.
Anasema kujaa kwa bidhaa za China nchini kama vile
sabuni na dawa mbalimbali ni ishara kwamba kuna mwanya
fulani usio wa kawaida.
"Hizi bidhaa ni nyingi sana na zinatangazwa kwa kila
aina ya mtindo. Ukipanda baadhi ya mabasi kati ya
Morogoro na Dar es Salaam utashangaa kukutana na
Watanzania wakitangaza na kuuza bidhaa za Kichina.
"Mimi nashangaa kwa mambo mengi lakini kubwa ni kwamba
iweje Watanzania wawe wajasiri kutangaza mali za wengine
na kuacha za kwao?
"Unajua kwa asili Watanzania ni wenye aibu kidogo,
hawapendi kuropoka lakini katika hili wana bidii kweli
kweli kutangaza bidhaa hizo, hakika inashangaza.
"Siamini kwamba katika Tanzania hatuna bidhaa inayofaa
kutangazwa kwa mtindo ule, nadhani zipo na zimejaa,
lakini sielewi tatizo liko wapi hadi tuziache za kwetu,"
anasema Dk. Wilson.
Dk. Wilson mbali na kuwa mhadhiri mwandamizi, ni
Mkurugenzi Mtendaji na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya
Edie B Wilson Consult, yenye makao makuu yake mjini
Morogoro.
Ni mama wa watoto wanne; wawili wa kike na wawili wa
kiume wanaoishi Marekani.
Elimu yake yote ya darasani ameipatia nchini Marekani
alikohitimu shahada ya uzamivu (PhD) Machi mwaka 1976
katika Chuo Kikuu cha Morgan, Baltimore, Maryland katika
masuala ya utawala.
Shahada ya uzamili aliipata katika Chuo Kikuu cha
Goddard, Vermont Mei 1974, huku shahada yake ya kwanza
akiipata katika Chuo cha Columbia, Washington D.C.
Amewahi pia kufanya masomo ya utawala wa biashara katika
Chuo Kikuu cha Howard na vyuo mbalimbali nchini Marekani
katika kozi ya utumishi wa umma.
Ni mtafiti ambaye mbali na kufundisha masuala ya utawala
katika Chuo cha Mzumbe, ni mshauri wa masuala mbalimbali
ya kijamii.
Ni mjumbe na katibu katika Tume ya Mabadiliko ya taasisi
kuwa vyuo vikuu, akiweka mfumo wa utawala na maendeleo.
Kati ya Januari hadi Oktoba mwaka 2000 alikuwa
Mkurugenzi Mkuu wa Mradi katika Kituo cha Ajira jijini
Dar es Salaam.
Akiwa katika nafasi hiyo, baadhi ya majukumu yake
yalikuwa kujenga mazingira ya kuhamasisha ajira kama
njia ya kupunguza umasikini kupitia iliyokuwa Wizara ya
Kazi, Maendeleo ya Vijana na Michezo.
Tangu mwaka 1993 hadi leo hajaacha kuwa mkufunzi katika
kampuni na mashirika mbalimbali ndani ya nchi.
Baadhi ya sehemu alizopata kutoa mafunzo ya utawala ni
pamoja na Reli, Kampuni ya Sigara Tanzania, Utumishi,
USAID na IrishAID.
Mwaka 1989 hadi 1993 alikuwa mshauri wa Mkurugenzi wa
Maendeleo Mkoa wa Morogoro, akiwajibika kutoa ushauri
katika mipango ya mkoa na mafunzo.
Amepata kuwa Mjumbe wa Kamati ya Tamasha la Pili la Watu
Weusi na Utamaduni jijini Lagos Nigeria, Katibu na
Mratibu wa Mkutano wa Sita wa Pan African.
Ametoa machapisho kadhaa ya mafunzo, baadhi ni ÔConflict
Management and ResolutionÕ, ÔGender Issues in the Labour
ForceÕ, ÔPotential for Industrial Development Scheme in
Morogoro and IringaÕ, ÔAssessment of Training Needs in
Kilosa DistrictÕ na ÔGlobal Trends in High Performance
OrganisationsÕ.
Ni mwanachama katika Jumuiya ya Wakufunzi wa Maendeleo
ya Marekani, Mlezi wa Shule ya Msingi Mwere Morogoro na
amewahi kuwa mwenyekiti wa TCCIA tawi la Morogoro.
Ni mjumbe Chuo Kikuu cha Meru, amewahi kushika wadhifa
wa mwenyekiti wa mashirika yasiyo ya kiserikali mjini
Morogoro na ni mwenyekiti wa Klabu ya Rotary mjini
Morogoro.

No comments: