na innocent munyuku
HERI ya mwaka mpya! Mzee wa Busati anawasabahi kwa furaha ya kuuona mwaka huu wa 2008. Yalopita si ndwele tugange yajayo.
Yawezakana mwaka uliomalizika jana ulijaa maumivu kwa wadau lakini hilo lisiwavunje moyo. Kazeni buti ili mambo yanyooke msimu huu.
Wiki hii pamoja na kuwa na furaha ya kuuona mwaka mpya, Mzee wa Busati anakenua meno baada ya kubaini kuwa katika kaya kumejaa mabahau na malimbukeni.
Hao hawataki kuguswa. Wakiguswa basi hufura kama moto wa volcano. Watapaza sauti zao kwa hasira na maneno machafu yawatoke kama vile hawakunyonya maziwa ya mama zao.
Juma lililopita Mzee wa Busati alitua kwenye safu yake akielezea umuhimu wa kumwacha huru Kocha Mkuu wa Taifa Stars Marcio Maximo.
Alichonena Mwandika Busati ni kwamba Maximo ambaye pia ni kocha wa Kilimanjaro Stars asiadhibiwe au kutupiwe lawama kupita kiasi.
Leo hii Maximo kwa wengine anaonekana adui mkubwa wa soka Tanzania. hawataki kumsikia wala kumwona usoni. Wanasema anaua soka Bongo.
Kimsingi alichokuwa anasema Mzee wa Busati ni kwamba kumtupia lawama kocha huyo ni jambo jema kama watupa lawama watakuwa na hoja mbadala.
Kwa bahati mbaya, hao wanaojiita wadau wa soka wakarusha makombora mazito kwa Mzee wa Busati. Wakatukana walivyoweza. Hapa akageuzwa Simon wa Kirene aliyemsaidia Yesu kubeba msalaba.
Wakasema hawana haja ya kuwa na Maximo eti kwa sababu analipwa mamilioni na hakuna analolifanya. Ameshindwa kazi! Hiyo ikawa kauli yao ya uhitimisho.
Wakaongeza kuwa kuna makocha wazawa ambao wakilipwa kama Maximo basi mambo yatakwenda sawia dimbani.
Lakini ukweli wa mambo ni bado kuna mengi ya kufanywa zaidi ya kulipwa vizuri katika kibarua cha ukocha. Lililo kuu ni maandalizi.
Juzi Mzee wa Busati kasikia mpango wa kujenga taasisi ya kukuza vipaji kwa vijana wenye umri usiozidi miaka 17.
Hayo ndiyo mambo ambayo yalipaswa kufanywa kabla hata Maximo hajaja. Yangeanza miaka tele nyuma leo hii tusingekuwa tunalaumu makocha gizani pasipo mbadala.
Leo kungekuwa na furaha kila kona kwani wachezaji waliopikwa wangekuwa tele na vipaji vyao viking’ara kimataifa.
Kelele hizi kwamba Maximo hafai wakati mwingine ni ufinyu wa fikra. Hao wanaopayuka leo hii hawana tofauti na wale wanaotamani kufika paradiso huku wakikataa kuonja mauti.
Miaka tele soka ya bongo ilitegemea tunguli na misimamo mibovu ya viongozi wa klabu na mamlaka zingine za soka.
Bila watu kulala makaburini timu isingeingizwa uwanjani. Bila mbuzi kuchinjwa na damu kupakwa wachezaji hakuna kutinga dimbani. Haya mambo si siri yamefanyika sana.
Hebu tusemezane kwa hoja. Hao makocha wazawa waliokuwapo kabla ya Maximo wamefanya jipya gani zaidi ya kukumbatia malumbano?
Mambo ya ulozi yamekuwa yakionekana kwa uwazi kabisa na ndio maana hivi karibuni Mkurugenzi wa Maendeleo ya Soka wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), Ashford Mamelodi alizitaka klabu kuachana na ndumba.
Mamelodi alitoa kauli hiyo wakati akifunga semina elekezi kwa timu za Ligi Kuu Tanzania Bara mjini Bagamoyo.
La maana linalopaswa kufanywa ni kuhakikisha kuwa kila anayejiita mdau na mkereketwa wa soka atambue majukumu ya kuendeleza soka kwa uongozi na ufundi.
Turejee kwa Maximo. Kocha huyo raia wa Brazil ametua nchini katika muda ambao Tanzania ilikuwa katika mlolongo wa migogoro katika klabu za soka.
Kwa bahati mbaya sana migogoro hiyo ingali ikiendelea kuzitafuna klabu. Klabu ambazo Maximo anastahili kubeba wachezaji kwa ajili ya timu ya taifa.
Hebu basi tuangalie mizizi ya soka yetu kabla ya kumtupia mawe Maximo. Bila shaka msimamo wake wafaa uheshimiwe, asipigiwe miluzi mingi. Huo ndio mtazamo wa Mzee wa Busati.
Vinginevyo Mwandika Busati anaomba mema yatue mwaka huu kwa wadau wake. Endeleeni kupanga yenye tija na kila mmoja awajibike kwa nafasi yake.
Wasalaam,
Wednesday, January 2, 2008
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment