Na Innocent Munyuku
SIMULIZI za ujio wa Rais wa Marekani George W. Bush zinaendelea. Mtawala huyo anayesemwa kuwa kinara wa dunia alitua nchini Jumamosi iliyopita kwa ziara ya siku nne ambayo inakoma leo.
Mzee wa Busati naye hakutaka kupitwa na jambo. Kwa nafasi yake alilazimika kujua walau machache yaliyomleta mtawala huyo.
Wengine wakaguswa na mbwembwe za ulinzi wa rais huyo. Hakuona wana wa Darisalama walivyokuwa wakiinua macho yao angani kushuhudia helikopta maalumu ya kinara huyo? Ina kitu na kwa wajuao umombo huiita Marine One!
Mwandika Busati hata hivyo kabla ya ujio wa Bush alikuwa na jambo jingine alilokuwa akisubiri kusemezana na wadau wake. Hilo si jingine bali ni pilika za Februari 14 ambayo huaminika kuwa ni Siku ya Wapendanao kote duniani.
Siku hiyo ni maalumu kwa watu kuonyeshana upendo wa dhati. Marafiki kwa marafiki, mke kwa mume au baba kwa mwana. Kwa ujumla ni siku ya kuonyesha kwamba unamjali mwingine.
Lakini mambo kwa wengi nchini hayakuwa kama ilivyonenwa hapo juu. Mtandao wa Mzee wa Busati umenasa mengi ya aibu siku hiyo.
Wengi wakaigeuza siku hiyo kuwa ni ya kula halimtumwa kwa kiwango cha hali ya juu.
Halimtumwa ni aina ya kiazi kitamu kilicho na rangi ya manjano ndani na kwa kawaida hupendwa sana na walaji kutokana na utamu wake huo.
Hivyo ndivyo walivyoigeuza Februari 14. Wakaifanya siku ya kula halimtumwa. Waking’ara na mavazi yao mekundu na mauaridi mkononi wakaamua kuifanya siku hiyo kuwa ni ya kufanya mapenzi.
Hawakujali kama wako salama au la. Walichoona wao kinafaa ni kula uroda kwa jina la Valentine! Hali hii kwa hakika imemtisha Mwandika Busati kwani kuigeuza siku kama hii kuwa ya kufanya mapenzi ni kuliangamiza taifa.
Nani kawalaani hawa kiasi hiki? Ni nani hasa alihusika na kupiga zumari la kuhamasisha ngono kwa watu hawa?
Lakini haya ndiyo madhara ya kukumbatia kila jambo kutoka ughaibuni. Tukiyaona ya Ulaya au Marekani basi huwa yenye kufyonzwa pasipo kujiuliza kama yanaeleweka.
Kinachomsikitisha Mzee wa Busati ni kwamba miaka inazidi kusonga mbele na hakuna dalili kwamba Wabongo wanaielewa maana halisi ya Februari 14.
Kwa walio wengi hiyo ni siku ya kujificha mahala kwa ajili ya ngono. Tena husikika pahala pengine kuwa wapo walionuna kwa vile wapenzi wao siku hiyo hawakutimizia haja zao za kimwili. Salaale...!
Hii boti ya Februari 14 isipoangaliwa itakimaliza kizazi cha Watanzania ambacho tayari kimefunikwa na maradhi mengine pamoja na umasikini.
Mzee wa Busati akisema ataonekana mwendawazimu lakini heri aseme ili waso mabahau wayachuje na kuyaweka sawia.
Kwamba kwanini basi wasijitokeze wadau na kutoa elimu kwa umma wa Watanzania kuhusu maana halisi ya Februari 14?
Waombe ngwenje kwa wafadhili waandae vijisemina waseme kwa uwazi kwamba siku hiyo si maalumu kwa ajili ya zinaa. Wasiigeuze Februari 14 kuwa kiazi aina ya halimtumwa.
Vinginevyo, miaka michache ijayo Tanganyika hii itajaa makaburi yalotokana na ulimbukeni kwa Februari 14.
Mzee wa Busati anajua fika kwamba kwa msimamo wake huu atakuwa amejijengea uadui na wamiliki wa nyumba za kulala wageni lakini ni heri aseme ili msije mkalaumu kwamba hamkuambiwa.
Mwandika Busati amefika tamati kwa juma hili. Tuombeane uhai ili tukutane tena wiki ijayo tupeane vionjo vingine.
Wasalaam,
Wednesday, February 20, 2008
Subscribe to:
Posts (Atom)